Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Furahini katika Bwana! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Furahini katika Bwana! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 3 ya Majilio: Furahini katika Bwana!

Tunaalikwa kufurahi kwa kuwa ukombozi wetu umekaribia. Tunadaiwa tuwe na fadhili ya uvumilivu inayofumbatwa katika imani ambayo katika Maandiko Matakatifu inajionesha kwa kumtumainia Mungu na Neno lake, akisadiki kuwa yeye ndiye ukweli na wema wote na chemchemi ya pekee ya wokovu. Msingi wa imani ni Mungu asiyeweza kudanganga; Mungu ambaye daima ni mwaminifu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya majilio mwaka A wa Kanisa. Maneno ya, “furahini katika Bwana nasema tena furahini kwa kuwa Bwana anakuja” yanafungua na kuweka bayana ujumbe wa dominika hii ya tatu ya majili, yaani ujumbe wa furaha. Tunaalikwa kufurahi kwa kuwa ukombozi wetu umekaribia. Lakini furaha yetu yatudai tuwe na fadhili ya uvumilivu inayofumbatwa katika imani ambayo katika Maandiko Matakatifu, inajidhihirisha kwa tendo la mtu kumtegemea Mungu na neno lake, akisadiki kuwa yeye ndiye ukweli na wema wote na chemchemi ya pekee ya wokovu. Msingi wa imani ni Mungu asiyeweza kusema uwongo, anayetimiza yote anayoahidi Lk 1:20, 45, Rm 3:3, Ebr 10:23. Katika Somo la kwanza Nabii Isaya anawaambia waisraeli, furahini kwani Bwana karibu anakuja kuwakomboa katika taabu zao zote akisema, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.

Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na faraja, huzuni na kuugua zitakimbia. Nabii Isaya anawaalika Waisraeli wafurahi, anawafariji kutokana na huzuni iliyosababishwa na majeshi ya Babiloni yaliyouteka mji wa Yerusalemu na kuuteketeza, wakawapeleka uhamishoni. Hekalu liliharibiwa na mlima ambao Yerusalemu ilijengwa juu yake uligeuzwa kuwa kama jangwa. Kule utumwani Babeli, waisraeli walinyanyaswa, wakaonewa na kutumikishwa kazi ngumu na wababeli. Waisraeli wakamlilia Mungu awaokoe. Ni katika hali hii ndipo nabii Isaya anapowatabiria waisraeli kuwa Bwana karibu atakuja kuwaokoa kutoka katika hali hii ya mateso na taabu. Kwa hiyo wafurahi.

Wafurahi kwa kuwa karibu watarudi nyumbani toka utumwani. Adha ya ukimbizi imekwisha. Watakuwa na makazi, ardhi ya Kilimo, watalijenga upya Hekalu ambamo watamwabudu Mungu wa kweli kwa kuimba zaburi na tenzi za moyoni, vipofu wataona, viziwi kusikia, vilema kutembea, maskini kuhubiriwa habari njema, na bubu wataongea. Ujumbe wa Nabii Isaya unajidhirisha wazi katika Injili ambapo Yesu anawaambia wafuasi wa Yohane wakamwambie wanayoyaona na kuyashuhudia kuwa vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema ya wokovu. Kwetu sisi Wakristo Furaha iletwayo na Kristo ni nguvu yetu katika mateso, taabu na mahangaiko ya dunia hii. Hatuna budi kufurahi kwa kuwa ukombozi toka Utumwa wa Dhambi na Nguvu za giza umekaribia. Heri na fanaka vitatawala. Furaha ni tunda la amani, upendo, utulivu, wema, haki na usitawi. Furaha hii inahusu watu na viumbe hai. Furaha ya kweli inatokana na kumjua Mungu, kumpenda, kumtumikia na mwisho kushiriki maisha ya umilele katika ukuu wake. Inatokana na kumjua Kristo ndiye mwokozi wetu. Hii ndiyo habari njema anayotuletea Masiha.

Mtume Yakobo anasisitiza juu ya uvumilivu kama wa mkulima kwa kutarajia mambo yajayo kwa imani. Yakobo anasema tunapongoja kuja kwake Bwana, tuwe na subira kama ya mkulima anayengoja matunda ya kazi yake akisema, nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Mara nyingi tunashindwa kuonja huruma na wema wa Mungu kwasababu hatuna uvumilivu na imani yetu ni hafifu.  Kosa ambalo mara nyingi tunafanya ni kumpangia Mungu lini na namna gani atutimizie shida zetu. Masomo ya leo yanatukumbusha tuwe wavumilivu, tuvuta subira kwa kuwa Mungu atatimiza ahadi zake kwetu kwa wakati na namna yake mwenyewe. Sisi tuseme tu “mapenzi yake yatimizwe”. Mchanganyiko wa imani tulionao unafifisha imani na uvumilivu wetu kwa Mungu wetu wa kweli. Nabii Isaya anasema tusiwe na hofu kwa maana mambo yote yanayotutisha katika ulimwengu huu si kitu mbele ya Mungu.

Yeye atatuokoa kama tutakuwa wavumilivu kumngoja. Matatizo yanayotukabili yasitukatishe tamaa na kutukosesha uvumilivu kama Yohane mbatizaji, bali tuige mfano wa mkulima, ingawa wakulima tulionao siku hizi wengi wao ndiyo wanaoongoza kwa kuyumba kiimani, kufanyakazi za shamba siku za dominika na sikukuu. Kumbe tukumbuke kuwa bila Mungu mambo yote tunayofanya pamoja na maisha yetu kwaujumla ni “ubatili mtupu”. Kama Waisraeli walivyofurahi wakingojea siku ya ukombozi nasi pia tunapaswa kufurahi wakati tunapongojea kuja kwake masiya mara ya pili. Tunapaswa kufurahi kwa sababu atakapofika taabu, mateso na mahangaiko yaliyoletwa na dhambi yatakwisha na heri na furaha vitatawala. Yeye anakuja kutuokoa, anakuja kufanya yote upya anakuja kuukamilisha ufalme wa Mungu aliouanzisha hapa duniani na katika ufalme huu, furaha, amani na upendo vitatawala. Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili 3 ya Majilio
13 December 2019, 18:14