Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Umuhimu wa kukesha na kusali ili kujiandaa kumpokea Masiha anayezaliwa tena katika maisha ya waja wake! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio: Umuhimu wa kukesha na kusali ili kujiandaa kumpokea Masiha anayezaliwa tena katika maisha ya waja wake! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza Majilio: Mwanga wa imani!

Tafakari: “Kesheni.” Yesu anatualika tuamue sasa kuipokea au kuikataa Injili mpya. Aidha, ili kuelezea kukesha au kufanya tafakari anatupatia mfano wa mwizi. Kwamba Injili mpya inaweza kukufika wakati usiotegemea. Maana yake, daima kukaa chonjo vinginevyo unaweza kupoteza fursa itakapofika. Kwa sababu ni vigumu kujua wakati gani Bwana arusi anafika kuungana nasi. KESHENI BASI!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Vatican.

Ili kuishi kwa amani na usalama ulimwenguni yabidi kufuata utaratibu alioupanga Mungu mwenye kuumba. Uvunjifu wa utaratibu aliouweka Mungu Muumbaji una machungu yake.  Historia inawaonesha wanadamu waliozivunja taratibu hizo na kuingiza sera zao. Ulimwengu ukageuka kuwa uwanja wa fujo, wa ukatili na ugandamizaji wa kila aina. Katika Kitabu cha Mwanzo juu ya Nuhu, neno ukatili linatajwa mara mbili. Mapato yake Mungu akaingilia kati na kufutilia mbali ulimwengu wa Nuhu na kuanza upya. Hata hivyo binadamu akaamua kumweka Mungu pembeni na kujitukuza mwenyewe. Hali hii ilijidhihirisha katika utukufu wa hekalu la Yerusalemu na ukuu waliokuwa nao makuhani. Mungu akawatuma manabii kuwaeleza kwamba atakuja mfalme mkuu atakayebadili mazingira hayo. Watu wengi hasa waliokereka na makuhani walisubiri kwa hamu mabadiliko atakayoleta mfalme huyo ajaye. Yesu anatoa makundi ya watu na namna wanavyopokea mabadiliko hayo:

Kundi la kwanza ni la watu wa maisha ya kawaida ya kula, kunywa na kuoana: “Kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, kabla ya gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina.” Watu hawa walizama kwenye maisha ya kawaida ya kula, kunywa na kuoana. Kumbe hata maisha ya kawaida yanaweza kukufunga macho usiweze kuona mabadiliko ya ulimwengu yanapotokea. Ndipo Yesu anapoleta picha ya gharika kuu.  Kisha tunaona mfano mwingine wa familia iliyofanya tafakari ya kina ya maisha ya kawaida yanayomtonya kwamba kuna mambo mapya yatakayotokea katika mazingira hayo ya kawaida. Ndiyo familia ya Nuhu pekee inaokoka: “hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina.” Kwa sababu binadamu tunaishi bila kutafakari maisha ya kawaida na hivi tunashindwa kufunguka macho kwa matukio yasiyo ya kawaida. Kwa hiyo gharika ni hukumu ya Mungu juu ya maisha ya kawaida ya kila mtu hapa duniani. Siyo kwamba Mungu anakuja kukuharibu, la hasha bali anatutahadharisha kwamba kama hatupokei ujumbe mpya utokao mbinguni, maisha haya ya kawaida yanaweza kwenda na maji.

Kumbe ni muhimu kufaidi maisha ya ulimwengu huu, lakini tunaonywa kutokurudia makosa yaliyowaponza wenzetu katika Biblia. Kundi la pili ni la wakulima na wale wenye kazi za kitaaluma na za ufundi: “Watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atatwaliwa, na mmoja ataachwa.”  Watu hao wapo katika hatari ya kujikita katika kazi na kuiona kuwa ndiyo kipeo cha mwisho cha maisha yao. Mapato yake mmoja anatwaliwa na mwingine anaachwa. Neno hili kutwaliwa kwa lugha ya Kigiriki ni paralambanetai, kwa Kiingereza ni “being taken along” maana yake kujikita katika kazi kadiri ya mapendekezo ya Injili ya upendo. Yaani ya mtu anayetumia utaalamu wake kikamilifu na kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine. Kumbe mtu mwingine ataachwa yaani aphietai. Mtu huyo ataachwa hapohapo "aphietai" kwenye kazi yake, tungeweza kusema “Kalagabao.” Mathalani, tajiri mwenye fikra za ulimwengu wa kale atashughulika zaidi katika kujilimbikizia fedha, mali na utajiri, na mafanikio bila kuwafikiria wengine.

Kundi la tatu ni la wafanya kazi muhimu za nyumbani: “Wanawake wawili watakuwa wanasaga, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” Kwa kawaida wanawake walikuwa wanasaga unga wa ngano na kutengeneza chakula. Kumbe kila mmoja anatakiwa aandae chakula kwa ajili ya ndugu. Aidha shughuli ya kuandaa chakula cha maisha. Chakula hicho si lazima kiwe cha kushibisha tumbo tu, bali chaweza kuwa pia chakula cha kiakili cha cha utu, cha upendo na cha kuwafurahisha wengine. Mtu huyo atakuwa amepokea ulimwengu mpya. Lakini mtu mwingine ataachwa katika ulimwengu wa ubinafsi. Hali ya kufanya tafakari juu ya malengo ya shughuli hizo muhimu uzifanyazo ndiyo inayooneshwa hapa kwa neno hili: “Kesheni.” Aidha isieleweke kwamba sasa inabidi kuogopa hukumnu kali ya Mungu. La hasha, Yesu anatualika tuamue sasa kuipokea au kuikataa Injili mpya. Aidha, ili kuelezea kukesha au kufanya tafakari anatupatia mfano wa mwizi. Kwamba Injili mpya inaweza kukufika wakati usiotegemea. Maana yake, daima kukaa chonjo vinginevyo unaweza kupoteza fursa itakapofika. Kwa sababu ni vigumu kujua wakati gani Bwana arusi anafika kuungana nasi.

Kwa namna nzuri ya kukesha ni kufanya fikara au tafakari. Leo ulimwengu kuna mambo mengi yanayoweza kutuchanganya akili. Kwa hiyo tunahitaji ukimya ili kuweza kukuza thamani zile zinazoweza kutusahaulisha mambo makubwa ya Injili. Hivi yabidi kukesha (kutafakari) ili kutokuyumbishwa na matangazo ya biashara, ya madawa, ya maadili, ya siasa, yanayopeperushwa na ushabiki waandishi wa habari. Kama hatutafakari hatuwezi kuuona muda ambao Kristo anataka kutuingiza katika ulimwengu mpya. “kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.” Mfano huu unatudai sote kujilinda daima kwani mwizi anaweza kufika wakati wowote ule usiotabirika. Hapa yaonekana kama vile Mungu ni mwizi anatuibia mali zetu. Ukweli wa mambo mali yote ni ya Mungu, isipokuwa sisi ndiyo wevi tuliojimilikisha mali ya Mungu. Tunajidhani kwamba kazi zote ni zetu, utalamu tuliona nao ni wetu na maisha yote unayofaidi ni mali yetu.

Hivi tunaona kama vile tunaibiwa na tunafirisiwa na kunyang’anywa na mwizi. Kumbe, Mungu siyo mwizi bali ni wewe hukuviona vitu hivyo kwa mtazamo utakiwao. Yesu anatuambia: “kesheni, mkijiandaa kumpokea Masiha. Katika kila kazi tunayofanya, tuangalie tunaishije mahusiano yetu na hali halisi ya ulimwengu huu kwani wakati msiodhani Mwana wa mtu hufika, si ujio wa mwisho wa dunia, bali sasa. Pokeeni ujumbe mpya unaokujia.

29 November 2019, 15:41