Vatican News
Tarehe 17 Novemba 2019 wameadhimisha sherehe ya miaka 10 ya Jimbo la Kayanga Tanzania pomoja na kutimiza miaka 10 ya kuwa Askofu wa Jimbo hilo Almachius Rweyongeza. Tarehe 17 Novemba 2019 wameadhimisha sherehe ya miaka 10 ya Jimbo la Kayanga Tanzania pomoja na kutimiza miaka 10 ya kuwa Askofu wa Jimbo hilo Almachius Rweyongeza. 

Jimbo Katoliki Kayanga:waamini muwe na msimamo imara wa imani kwa Yesu!

Tarehe 17 Novemba 2019 Askofu Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga ameongoza misa Takatifu ya kumshukuru Mungu katika kilele cha kutimiza miaka 10 ya Jimbo hilo na miaka 10 ya Uaskofu wake.Misa imuudhuriwa na Askofu Mkuu Nyaisonga,Rais wa TEC,maaskofu:Rwoma Jimbo la Bukoba,Banzi Jimbo la Tanga,Ntahondereye wa Jimbo la Muyinga-Burundi,Mons.Matata Orest Jimbo Kabungo-Rwanda na watu wote wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Na Patrick P. Tibanga - Radio Mbiu & Sr. Angela Rwezaula – Vatican 

Wakristo wakatoliki wawe na  msimamo imara na kusimika imani katika Yesu pamoja na kuwa na subiri katika imani hasa  pale watakapochukiwa na watu wote kwa kutetea imani yao kwani subira huponya, huvuta baraka na subira hung'oa milima. Wakristo lazima kuzingatia kuzingatia na kufuata kanuni na misingi ya imani ya Kanisa Katoliki. Hayo yamesemwa na Askofu Almachius Vicent Rweyongeza, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kayanga Tanzania, Jumapili tarehe 17 Novemba 2019 wakati wa mahubiri yake ya misa Takatifu ya kumshukuru Mungu katika kilele cha kutimiza miaka 10 ya Jimbo la Kayanga na miaka 10 ya Uaskofu wake ambapo pia iliambatana na uzinduzi wa nyumba ya kiaskofu ya jimboni Kayanga Tanzania.

Wakristo wa kweli wasifuate sauti za udanganyifu

Askofu Rweyongeza katika mahubiri yake akiangaziwa na masomo ya siku yaliyosomwa amesema kuwa mkristo mkatoliki kamwe hatakiwi kuwafuata wanaokuja na kuwadanganya kwa kuwalaghai kwa fedha, magari na mali za kupita hapa duniani. Mkristo anatakiwa kuwa na subira, uvumilivu pamoja na  kuwa na imani thabiti ambayo itasaidia kung'oa visiki na milima na kufuata kanuni msingi za Kanisa katoliki.

Onyo dhidi makanisa yanayoibuka na wachungaji wa miujiza fake

Hata hivy akibainisha juu ya ulaghai wa madhehebu ameonya dhidi ya madhehebu yanayoibuka kama uyoga na hivyo  Akofu Rweyongeza amesema kuwa “wahubiri fake huwahubiria watu tusiowafahamu, na wale wenye magonjwa sugu ambao tunawafahamu, hawawafuati kuwaponya katika mahospitali  na wanatuletea watu fake ambao siyo wa kweli  na nyinyi mnawafuata”. Je  wangekuwa waponyaji kweli kwa nini wasingeenda kuponyesha kwenye hospitali? Anawachangamotisha Askofu Rweyongeza na kuongeza kusema, hawa wanaokuja wanajifanya wanatenda miujiza kwa jina la Yesu, lakini wanashindwa kuelea juu ya maji kama Yesu, hawawezi kutenda kwa kuwafufua wafu kama Yesu, lakini  Yesu anasema wengi watakuja kwa Jina la lake”. Askofu Rweyongeza Akitoa mfano amesema wapelekeeni maji ya beseni  hao (…)

Wakristo wawe na moyo wa shukrani

Aidha Askofu Rweyongeza katika mahubiri yake ameweka msisitizo zaidi huku akiwataka wakristo wakatoliki kuwa na moyo wa shukrani kwamba: “Tunayo kila sababu ya kumshukuru Yesu Kristo kwa kutufikisha kutoa shukrani kwa Mungu kwa kushiriki adhimisho Takatifu la misa, kwa sababu ni tendo kuu la shukrani kwa Mungu, hivyo basi niwaalike tuendelee kushiriki na kuadhimisha misa Takatifu kwa uchaji ili tuweze kupata heri ya milele huko mbinguni na kuwa na moyo wa Shukrani kwa yale yote tunayotendewa na Mungu pamoja na jirani zetu”. Amesema hayo kufautana na miaka kumi ya kutimiza katika jimbo hilo akiwa Askofu wa kwanza na pia juu ya ujenzi wa nyumba ya Askofu ambayo kwa dhati ni kutokana na majitoleo na sadaka ya waamini na watu wa Mungu wenye mapenzi mema.

Pongezi kutoka kwa Askofu Mkuu Nyaisonga, Rais wa TEC

Kwa upande  wa Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga  Rais wa Baraza la maaskofu Katoliki Tanzania amempongeza Askofu Rweyongeza kwa kuadhimisha miaka kumi ya Jimbo, Miaka 10 ya uaskofu pamoja na ujenzi wa nyumba ya kiaskofu. Na zaidi ameomesha kuvumilia kwa kipindi chote tangu Jimbo lilipokuwa change vile vile amemia fursa hiyo kuwapongeza maaskofu, mapadre na  waamini kwa kudumu katika imani na mshikamano. Askofu Mkuu Nyaisonga amesema: “Tunatoa hongera nyingi kwa Askofu wa kwanza wa Jimbo kwani amevumilia uchanga wa Jimbo na sasa anaendelea vyema kuliongoza Jimbo na kwa macho, na  tunaona mafanikio makubwa yaliyo bora na tunawashukuru watawa na mapadre wa Jimbo hili kwa mshikamano, na utii kwake”.

Waamini waendelee kuunga mkono jitihada za maendeleo

Kwa huhitimisha Askofu Mkuu Nyaisonga amesema,“Ninawapongeza kwa maendeleo yote yanayotambulika kwa jimbo na mkoa wa Kagera kwa ujumla, mwendelee kuunga mkono jitihada za dhati zinazoungwa mkono maendeleo kwa watu wote, mwendelee kuwa mstari wa mbele kusimamia amani, mshikamano na ustawi wa taifa la Tanzania.”

Maaskofu kutoka ndani na nje ya nchi wameudhuria misa 

Katika misa hiyo ya kusherehekea miaka 10 ya Jimbo la Kayanga na miaka 10 ya Uaskofu pamoja na  uzinduzi wa nyumba ya kiaskofu, pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya Askofu mkuu Gervas Nyaisonga pia walioudhuria misa Yakatifu ni Askofu Desderius Rwoma wa Jimbo la Bukoba, Askofu  Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, pamoja na Askofu Joachim Ntahondereye wa Jimbo Katoliki la Muyinga nchini Burundi, Monsinyo Inchi Matata Orest wa Jimbo la Kabungo nchini Rwanda, wawakilishi wa majimbo ya jirani ndani na nje ya Tanzania, mapadre, watawa na watu wote  wa Mungu jimboni Kayana.

Viongozi wa Serikali na vyama 

Licha ya viogozi wa Kanisa pia kulikuwa na viongozi wa serikali ambapo mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa ni Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mbunge wa Wilaya ya Karagwe, Tanzania Bwana Innocent Bashungwa, aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marko Gaguti pamoja na mkuu wa Wilaya ya Karagwe na vingozi wengine wa Serikali nchini Tanzania.

ASK.ALMACHIUS RWEYONGEZA
19 November 2019, 09:06