Sr. Mariana Nyakunga Mdemu alizaliwa mwaka 1973. Tarehe 13 Oktoba 2010 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 14 Oktoba 2019 akafariki dunia na kuzikwa tarehe 19 Oktoba 2019 nchini Italia. Sr. Mariana Nyakunga Mdemu alizaliwa mwaka 1973. Tarehe 13 Oktoba 2010 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 14 Oktoba 2019 akafariki dunia na kuzikwa tarehe 19 Oktoba 2019 nchini Italia. 

Sr. Mariana Nyakunga: Mbegu ya umisionari toka Tanzania!

Sr. Mariana Nyakunga Mdemu alizaliwa tarehe 20 Februari 1973. Mwaka 2002 akatumwa nchini Italia ili kuanza malezi na majiundo yake ya kitawa na hatimaye, kuweka nadhiri za daima tarehe 13 Oktoba 2010 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 13 Oktoba 2019 akaugua ghafla na hatimaye kufariki dunia tarehe 14 Oktoba 2019. Amezikwa tarehe 19 Oktoba 2019, Italia.

Na Padre Angelo Shikombe na Shemasi Karoli Amani Joseph - Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, kutokana na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kifo cha Kikristo kimepata maana nzuri zaidi, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anakufa pamoja na Kristo kisakramenti, ili kuishi maisha mapya, na kwa sababu wanakufa katika neema ya Kristo Yesu. Hii ni kwa sababu kwa njia ya kifo, uzima wa waamini hauondolewi ila unageuzwa tu! Na Makao ya hapa duniani yakishabomolewa, wanapata makao ya uzima na maisha ya milele mbinguni. Kifo ni mwisho wa safari ya mwanadamu hapa duniani, ni wakati wa kupata neema ya huruma ya Mungu inayoratibisha maisha ya mja wake hapa duniani mintarafu mpango na mustakabali wa maisha yake. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu wa Shirika la Wafranciskani wa Bwana, aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba na kuzikwa huko Caltanissetta, Sicilia, Kusini mwa Italia, Jumamosi tarehe 19 Oktoba 2019.

Askofu Mario Russotto wa Jimbo Katoliki la Caltanissetta, Ijumaa, tarehe 18 Oktoba 2019, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya “Signore della Citta" kwa ajili ya kumwombea Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu. Ibada hii imehudhuriwa na watu wa Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Caltanissetta, lakini jambo ambalo limewashangaza wengi ni umati mkubwa wa mapadre na watawa wanaoishi na kufanya utume wao Kusini mwa Italia, walivyohudhuria kwa wingi. Askofu Mario Russotto katika mahubiri yake amemtaja Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu kuwa ni shuhuda na ua la kitanzania lililopamba bustani ya Shirika la Wafranciskani wa Bwana na Kanisa la Kristo katika ujumla wake. Ni mtawa aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma iliyomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani. Alikuwa ni mshauri mwema kwa watawa wenzake. Katika maisha yake, alionesha uchangamfu wa pekee, ushuhuda wa furaha ya Injili unaowagusa watu na kuacha chapa ya kudumu.

Sr. Mariana ameonesha ule Uso wa furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Katika maisha na utume wake kama mtawa alifanikiwa kuunganisa “Sala na Kazi” (Ora et Labora”. Sr. Mariana amejitahidi kuwa mtawa msikivu wa Neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa Maria, Neno ambalo amelimwilisha katika huduma ya upendo kama alivyofanya Martha, walipomkaribisha Kristo Yesu kwenye familia yao. Sr. Mariana alionesha bidii na udumifu katika sala na tafakari ya Neno la Mungu! Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, nchini Italia, Alhamisi tarehe 17 Oktoba 2019, walipata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kutoa heshima zao kwa Sr. Mariana Nyakunga Mdemu kabla ya kusafirishwa kwenda Caltanissetta kwa mazishi. Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Katika mahubiri yake aligusia kuhusu ushiriki wa wito wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia ambao kwa mwaka huu unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika Umisionari Duniani”. 

Padre Mjigwa amesema, Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Sr. Mariana Nyakunga Mdemu, ameyamimina maisha yake kama sehemu ya ushiriki wake katika mradi mkubwa wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ili kuendelea kuwasha moto wa imani, kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaboresha maisha yao kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama alivyofanya Sr. Mariana katika maisha na utume wake kama mtawa. Padre Mjigwa, ametumia fursa hii kuwashukuru wamisionari waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili nchini Tanzania, takribani miaka 150 iliyopita. Leo hii imani inaendelea kuchanua na matunda yake yanaonekana ndani na nje ya Tanzania.

Mama Kanisa anaposherehekea na kuwakumbuka wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Barani Afrika, wakleri na watawa kutoka Tanzania, wakumbuke kwamba, sasa ni zamu yao kujisadaka bila ya kujibakiza. Makaburi ya wamisionari waliolala katika usingizi wa amani Bagamoyo, Pugu na kwingineko ni ishara kwamba, sasa ni zamu yao pia kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na pengine, hata wazazi, ndugu na jamaa zao hawatapata kaburi kwa ajili ya kuwaombolezea kutokana na umbali! Makaburi ya Bagamoyo yawakumbushe sadaka ya umisionari na utume kwa ajili ya Kanisa. Wakati huo huo, Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora katika salam zake za rambi rambi kwa Masista wa Shirika la Wafranciskani wa Bwana, amesema, Jimbo kuu la Tabora limeguswa sana na taarifa za msiba wa Sr. Mariana aliyeishi na kukulia Parokia ya Ipuli, Jimbo kuu la Tabora. Kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora, Sr. Mariana ataendelea kung’ara kama nyota angavu ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni ushuhuda wa wito na utume wake katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Kwa sasa familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora inamwombea huruma ya Kristo Mfufuka, ili aweze kupokelewa miongoni mwa wateule wake huko mbinguni!

Kwa upande wake, Mheshimiwa George Kahema Madafa, Balozi wa Tanzania nchini Italia, kwa namna ya pekee kabisa, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia fursa ya kuweza kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Sr. Mariana Nyakunga Mdemu katika safari yake ya mwisho hapa duniani. Wameupokea msiba huu kwa majonzi makubwa, kwani walimfahamu, wakampenda kutokana na busara, hekima na upendo, ucheshi na ukarimu wake. Muktadha wa kifo chake cha ghafla, umeongeza simanzi zaidi. Lakini, binadamu wanakumbushwa daima kwamba, hapa duniani ni wasafiri na kwamba, haya maisha “wamekopeshwa na Mungu”. Kumbe, anayo uwezo wa kuyatoa na kuyatwaa kadiri anavyopenda. Huu ni msiba ambao umewaumiza watawa wenzake, lakini umewagusa na kuwatikisa watanzania kwa sababu alikuwa mtanzania. Ubalozi wa Tanzania umefanikisha mchakato mzima wa kutafuta na hatimaye, kupata nyaraka za kusafiria kwa Nelson Mgumba, mwakilishi wa familia ya Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu aliyewasili mjini Roma, Jumamosi asubuhi na kwenda moja kwa moja Caltanissetta, Sicilia, Kusini mwa Italia na kushiriki katika Ibada ya mazishi iliyofanyika Jumamosi, tarehe 19 Oktoba 2019.

Sr. Mariangela kwa niaba ya Jumuiya ya Masista Wafranciskani wa Bwana, Roma, amemwelezea Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu kuwa ni alikuwa ni mtu wa watu, aliyekirimiwa kipawa cha kusikiliza na kushauri; kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani, lakini kwa wahitaji zaidi. Alibahatika kuwa na kipaji cha akili ya kuzaliwa na wala si akili ya kusoma vitabuni. Alibahatika kuwa na hekima ambayo kimsingi ilikuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu naye akaitumia barabara. Kwa miaka yote ya malezi na maisha yake kama mtawa amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Kama mshumaa, amezimika “ghafla bin vu” ili aendelee “kuteketea kwa sala” mbele za Mwenyezi Mungu. Ni matumaini ya watawa wenzake kwamba, ile furaha na ucheshi wake utamwezesha kuwa karibu sasa na Kristo Yesu, mchumba wake aliyejiaminisha kwake!

Naye Mheshimiwa Sr. Priscilla Dutra Moreira, Mama Mkuu wa Shirika la Wafranciskani wa Bwana, amewashukuru na kuwapongeza watanzania wote walioshiriki kikamilifu katika kumsindikiza Sr. Mariana katika usingizi wa amani. Kana kwamba, ilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya kifo chake, Sr. Mariana alipata nafasi ya kushiriki katika kongamano la kimsionari kwa mwezi Oktoba, akapata nafasi ya kusali kwa kitambo mbele ya kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi! Akapewa zawadi ya mshumaa uliokuwa unateketea, mshumaa ambao Sr. Mariana alisema, ilikuwa ni zawadi kubwa sana maisha mwake! Amekuwa kweli ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili kutoka Tanzania, wengi wataendelea kumkumbuka kutokana na ukarimu na ucheshi wake!

Hatimaye, Padre Paschal Ighondo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma, kwa niaba yao, amedadavua kwa kifupi kabisa kuhusu Fumbo la kifo katika maisha ya mtawa na umuhimu wa maadhimisho ya Ibada ya Misa kwa ajili ya kuwaombea Marehemu waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele. Amewashukuru viongozi wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Francisko wa Bwana, kwa kuwapatia watanzania nafasi ya kumlilia na kumwombolezea Sr. Mariana Nyakunga Mdemu katika imani inayokita mizizi yake kwenye Fumbo la Pasaka. Sala na sadaka ya Misa Takatifu ni zawadi na kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa unaoweza kutolewa na waamini kwa kuwakumbuka na kuwaombea marehemu ndugu, jamaa na rafiki zao! Mheshimiwa Padre Franz Refalo, Paroko wa Parokia ya “San Liborio” Jimbo kuu la Roma, ndiye aliyeongoza Ibada buriani kwa Marehemu Sr. Mariana Nyakunga Mdemu, kabla ya safari ya kuanza kuelekea huko Caltanissetta, Sicilia, Kusini mwa Italia, kwa Ibada ya mazishi yaliyofanyika, Jumamosi tarehe 19 Oktoba 2019.

Sr. Mariana Nyakunga
19 October 2019, 15:56