Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani ni chachu ya nguvu ya mabadiliko katika maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani ni chachu ya nguvu ya mabadiliko katika maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake! 

Tafakari Jumapili 27 Mwaka C: Mwenye haki ataishi kwa imani!

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Imani ni zawadi ya Mungu, fadhili ya kimungu inayomiminwa naye. ili kuishi imani hii, mwamini anahitaji neema ya Mwenyezi Mungu inayomtayarisha na kumsaidia, pamoja na misaada ya ndani ya Roho Mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayefungua macho ya roho na kuwapa wote utamu wa kukubali na kusadiki ukweli.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayaangalia na kuyatafakari masomo ya dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa. Dhamira kuu katika masomo haya ya leo ni nguvu ya imani katika maisha ya mwamini. Yanatuonesha kuwa imani ina nguvu ya kuleta mabadiliko katika maisha ya  mwamini na katika maisha mazima ya jamii inayomzunguka. Tena kuwa imani inaweza kuyabadilisha hata yale ambayo uzoefu wa kibinadamu unayaona hayawezekaniki.

Somo la kwanza (Hab 1:2-3, 2:2-4 ) ni kutoka katika kitabu cha Nabii Habakuki. Habakuki anauanza utume wake wa unabii katika namna ambayo kidogo ni tofauti na manabii wengine. Tumezoea kuwasikia Manabii wakianza utume wao kwa kubeba ujumbe wa Mungu na kuwapelekea watu. Hababuki yeye anaanza kwa kumhoji Mungu. Anaanza utume kwa kupaaza sauti na kilio kwa Mungu kwa sababu anaona nchi yake imejaa udhalimu, uharibifu, magomvi na uovu.  Habakuki anahoji iko wapi haki yake Mwenyezi Mungu! Mungu anamjibu. Na anamwambia jibu lake hilo aliandike lisomeke vizuri. Lakini anamwambia jibu lake hilo Mwenyezi Mungu litafika kwa wakati ulioamriwa na hata kama litakawia alingojee. Na jibu lenyewe ndilo hili “mwenye haki ataishi kwa imani yake”.

Kumbe, jibu la Mungu kwa Habakuki si kwamba watu wavute subira na wakae wakisubiri ujio wa Mungu kuja kuwatoa katika hali mbaya ya udhalimu, uharibifu, magomvi na uovu. Jibu la Mwenyezi Mungu ni kuwaalika warudi katika imani: warudi katika uaminifu, uadilifu na haki,  nao wataishi. Unabii huu tunaousikia katika somo hili la leo unatufundisha juu ya nguvu ya imani. Imani inayo nguvu ya kubadilisha si tu maisha ya kiroho lakini pia hata maisha ya kijamii. Mtume Paulo katika Waraka kwa Warumi 1:17 na katika waraka kwa Wagalatia 3:11 anaunukuu unabii huu katika kukazia mafundisho yake juu ya imani.

Somo la pili (2 Tim 1:6-8, 13-14) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo.  Katika somo hili, Mtume Paulo anamhimiza Timoteo juu ya wajibu wa kitume alionao. Kwanza anamkumbusha kuwa amepokea karama kwa njia ya kuwekewa mikono, yaani alipopewa daraja takatifu. Karama hiyo anapaswa kuichochea. Kwa maneno mengine Paulo anamwambia Timoteo asiuzime moto wa karama hiyo aliyopewa, alikumbuke hilo na aliweke akilini daima. Karama hiyo, anaongeza Paulo, asili yake si Paulo bali ni Roho wa Mungu na Roho huyo si roho wa woga bali ni Roho wa nguvu na wa upendo wa kiasi hivyo asione haya kuwa shuhuda wake. Anachomkumbusha Mtume Paulo ni kuwa utume alioupokea Timoteo umempa mwelekeo mpya wa maisha. Mwelekeo ambao unaweza kumuondoa Timoteo katika ukawaida wa maisha ya watu na kwa namna moja au nyingine Timoteo anaweza kujikuta anaona haya kwa kuwa tofauti.  Hapo Paulo anampa mfano wake mwenyewe ambaye kwa kuuishi ushuhuda huo amefikia hata kufungwa gerezani. Anamuimarisha adumu katika uvumilivu kwa ajili ya Injili na kwa kadiri ya nguvu ya Mungu.

Injili (Lk 17:5-10) Katika injili ya dominika ya leo ambayo ni kutoka kwa Mwinjili Luka, Mitume wanamwomba Yesu awaongezee imani. Katika swali hili ni muhimu kuona kuwa walichoomba Mitume sio kupewa imani bali ni kuongezewa imani. Kupewa, hupewa yule asiye na kitu na kuongezewa, huongezewa yule aliye nacho hata kama ni kidogo. Kwa swali lao hilo Mitume walijitambua kuwa tayari wana imani ila imani hiyo inahitaji kuongezwa. Jibu la Yesu ni kama linawaambia kuwa hawana hata imani hiyo ndogo waliyodhani wanayo, kwa sababu kama wangekuwa na imani kiwango cha punje ya haradali, punje tunayoweza kuilinganisha na mbegu ya mchicha, wangeweza kuuambia mkuyu “ng’oka ukapandwe baharini” nao ungewatii.

Yesu anapowajibu hawaambii hatawapa na wala hawakaripii ila yeye anaenda mbele zaidi ya kile wanachoomba. Anawaonesha nguvu na thamani ya hicho wanachokiomba. Anawaonesha ni nini imani inaweza kufanya katika maisha yao. Mti wa mkuyu ambao Yesu anawatolea mfano ni mti wenye tabia ya pekee. Kwanza ni mti mrefu sana unaoweza kufikia urefu hadi wa mita 40.  Na pia mkuyu ni mti wenye mizizi inayoweza kwenda mbali sana ardhini. Kuung’oa mti huu sio kazi rahisi. Ni kama haiwezekani.  Hapo Yesu anawaonesha kuwa mtu akiwa na imani hata ile ndogo kama mbegu ya mchicha anaweza kuuambia mkuyu ung’oke na ukang’oka. Imani inaweza kufanya ndani yao mambo makubwa hata yale ambayo kwa uzoefu wao hayawezekaniki.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo yetu haya ya leo yanatufafanulia kitu juu ya nguvu ya imani tuliyonayo kwa Kristo. Imani ni fadhila ya kimungu. Na kwa kuwa ni fadhila ya kimungu, asili yake ni Mungu mwenyewe. Yule ambaye Mungu anamjalia fadhila hii na yule ambaye anakubali kuipokea huishi katika muungano na Mungu mwenyewe. Kwa imani hii mtu huyaona na kuyaishi maisha yake katika mwono ule ule wa kimungu. Tunachokiona na kukitafakari katika masomo haya ya leo ni kuwa imani hii aliyonayo mtu haimbadilishi mtu au haimwokoi kwa sababu tu anayo. Anapaswa kutekeleza madai ya imani hiyo. Anapaswa “kuisikiliza” inamwambia nini katika mazingira halisi ya maisha yake, anapaswa kuzingatia inamtaka afanye nini katika mazingira hayo halisi ili azidi kukua na kuufikia wokovu uwe wa kimwili au wa kiroho.

Tumeona katika Somo la kwanza Mwenyezi Mungu alichomjibu nabii Habakuki: “mwenye haki ataishi kwa imani”. Mungu anamwambia Habakuki kuwa suluhisho la udhalimu, uonevu na maovu anayoyaona katika jamii ya watu wake ni kurudi katika imani. Na kurudi huku katika imani ni kufuata matakwa ya imani katika maisha halisi. Mungu atujalie neema hii ya kuisikiliza imani yetu na kuyafuata maelekezo yake ili tuione nguvu ya utendaji wa imani hiyo katika kuyabadili maisha yetu. Amina.

Liturujia J27
04 October 2019, 17:53