Vatican News
Sherehe ya Watakatifu Wote: Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Sherehe ya Watakatifu Wote: Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. 

Sherehe ya Watakatifu Wote: Wito wa Utakatifu na ushuhuda!

Kwa kuadhimisha siku za kuzaliwa mbinguni “Natus in cieli” kwa watakatifu, Kanisa linatangaza Fumbo la Pasaka linaloonekana katika watakatifu walioteswa pamoja na Kristo na kutukuzwa pamoja naye; linawaonesha waamini mifano yao inayovutia wote kwa Baba kwa njia ya Kristo. Linawaombea fadhili za Mungu kwa njia ya mastahili yao. (Rej. SC. 104. ) Iweni watakatifu!

Na Padre Reginald Mrosso, - Dodoma.

Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mtakatifu, Nafasi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo amejisadaka kwa ajili ya utakatifu wa Kanisa lake. Akajiunganisha nalo kama sehemu ya mwili wake na kulijalia kipaji cha Roho Mtakatifu. Utakatifu huu ni endelevu. (Rej. LG. 39).  Kwa kuadhimisha siku za kuzaliwa mbinguni “Natus in cieli” kwa watakatifu, Kanisa linatangaza Fumbo la Pasaka linaloonekana katika watakatifu walioteswa pamoja na Kristo na kutukuzwa pamoja naye; linawaonesha waamini mifano yao inayovutia wote kwa Baba kwa njia ya Kristo. Linawaombea fadhili za Mungu kwa njia ya mastahili yao. (Rej. SC. 104. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Novemba anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Wote, wito na mwaliko kwa watu wote kuchuchumilia watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kumwilisha Matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yao sanjari na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawataka waamini kujitoa kwa moyo wote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma ya jirani! Kanisa lililopo duniani na kanisa linaloteseka (toharani) huungana na Kanisa mshindi lililo mbinguni. Leo tunasherehekea tunayoungama kila Jumapili za mwaka - imani yetu katika ushirika wa watakatifu.  Sherehe hii ilianza kusherehekewa karne ya nne (4) katika Kanisa la Mashariki kwa ajili ya kuwakumbuka mashahidi (katika kitabu cha ufunuo, Mashahidi wanaitwa watakatifu) Ufu. 5:8 tunasoma hivi; hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato ambayo ni maombi ya watakatifu) – wa kwanza wa kanisa na baadaye ikawahusisha pia hata wasio mashahidi - hii ikihusisha pia kanisa la Magharibi. Inawahusisha wote wanaofahamika na wasiofahamika ambao wamefikia utukufu wa mbinguni.

Sherehe hii; Inaamsha pia wito wetu na haja ya kuutafuta utakatifu. Inatukumbusha kwamba kwa neema ya Mungu, tunaendelea kutafuta kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na katika jina la Bwana Yesu Kristo uzima wa milele. Inatukumbusha kuwa siyo tu tunaitwa kuwa watakatifu bali sisi ni watakatifu - 2 Kor. 1:1 na Ef 1:1 Paulo Mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kwa watakatifu walioko Efeso wanaomwamini Kristo Yesu.  Kol 1,2  na 4,12. Ndugu zangu wapendwa, ubatizo umetuingiza katika mwili wa Kristo. Hapo dhambi zetu zilifutwa tukawa jiwe la msingi - tukakubali kujengwa juu yetu nyumba ya kiroho, ukuhani mtakatifu na kutoa sadaka hai zinazompendeza Mungu - 1Pt 2.5 Katika harakati zetu za kusaka utakatifu tunategemea maongozi ya Roho Mtakatifu kutuongoza, kutufundisha na kutukumbusha yote aliyosema Bwana - Yoh 14:26. Roho Mtakatifu anatufundisha kusali, anatusaidia katika unyonge wetu – Rum 8:26-27 Katika kipaimara tumeunganisha na kukomazwa katika neema ya ubatizo katika kuweza kumuita Mungu ABA - Rum. 8, 15, kutuimarisha katika Kristo, kuongeza mapaji ya Roho Mtakatifu ndani yetu, kutakatifuza mahusiano yetu na kanisa - LG. 11, hutupatia neema ya pekee ya kueneza na kulinda imani yetu kwa maneno na matendo katika kumshuhudia Kristo, kuliungama jina la Bwana na kuulinda msalaba - Mtaguso wa Florence 1439, DS 1319, LG 11, CCC 1309.

Katika masomo yetu: Ufu. 7:14 – tunasoma, nikamjibu, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, hawa wanatoka katika dhuluma kubwa, wamefua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo - hawa ndo watakatifu tunaowakumbuka leo. Somo laonesha hali ya mwisho ya wale waliomtumaini Bwana. Hawa waweza kuwa wazazi wetu, mababu zetu, ndugu na jamaa - mavazi yao yameoshwa katika damu ya mwanakondoo. Walimtumainia Bwana hata kama hawakupata kumjua jinsi tunavyomjua sisi. Sikukuu hii yaweza kuitwa sikukuu ya watakatifu wasiofahamika nasi. Leo sisi tunasheherekea kile tunachosoma katika somo hili – Ufu 7,9-10 - baada ya hayo nikaona na tazama mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa na lugha wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele za mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao, wakillia kwa sauti kuu wakisema, wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi na mwanakondoo. Somo la pili latukumbusha juu ya upendo mkubwa wa Mungu aliyechagua kutuita sisi wana.

Roho Mtakatifu anatutakatifuza ili tufanane na Kristo - 1Yoh. 3,2. Kwa vile tunatakatifuzwa - wale wa ulimwengu hawajui bado hili. Matazamio yao na yetu ni tofauti kabisa. Somo laonesha matumaini ambayo wamwaminio Mungu wanapaswa kuwa nayo. Sisi ni watoto wa Mungu na tunasubiri bado kumwona Mungu uso kwa uso. Katika somo la Injili twaona kuwa furaha yetu i mbinguni - Mt. 5,12 - tuwe na imani basi kwa Mungu na tubebe msalaba pamoja na Kristo, tuishike imara imani yetu tukaze macho yetu kwa Bwana. Na katika 1Thes. 3,13 na 2Thes. 1,10 yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabia katika wote waliosadiki katika siku ile, kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu. Yesu ni mwalimu wa habari njema na mwalimu wa ufalme wa Mbinguni na utimilifu wa dahari. Maisha yetu ya Kikristo ni safari iendayo mbinguni, kudumu kwetu katika Kristo kutatufikisha mbinguni - ukamilifu wa matumaini yetu. Katika yeye tunaishi na tunatumaini kufa. Sisi tu wasafiri kwenda mbinguni. Njia ipo katika heri nane na mwisho wake ni mbinguni.

Katika sherehe hii tunasheherekea kilele cha matumaini yetu. Watakatifu hawa tunaowasherehekea leo ni wanaume na wanawake kama sisi. Siyo malaika. Waliishi na kuwepo tulipo sisi hapa leo na walipo sasa ndo tunatarajia kuwepo siku moja. Sisi wanadamu (wakristo) tunajua kuwa historia ya maisha yetu huanza hata kabla hatujazaliwa - bado tukiwa tumboni mwa mama zetu na inaendelea hata baada ya kifo chetu. Baada ya maisha yetu hapa duniani. Mtakatifu Theresia wa mtoto Yesu alizoea kusema anaishi mbingu akitenda mema hapa duniani. Katika macho yetu hatumwoni sasa, lakini tunashiriki matunda ya maisha yake anayoyaishi sasa kiukamilifu huko mbinguni. Tunapaswa kujua kwamba kufika mbinguni siyo jambo rahisi pia, ingawa inawezekana kabisa ila hatuna budi kutoka jasho. Neno hili la Mungu litupe changamoto - Mt. 6:21 tunasoma hivi; kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Na pia katika Mt. 7:21 tunasoma hivi si kila mtu aniambiaye Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Ni namna gani basi tuishi na kutimiza mapenzi ya Baba wa mbinguni hapa duniani ili tuweze kuzirithi mbingu? Tazama Injili ya leo Mt. 5:1-12 heri nane. Hapa Yesu anatupatia ramani ya matembezi yetu hapa duniani katika kuuendea uzima wa milele. Hawa tunaowasherehekea leo walipitia njia hii ya heri. Leo nasi tunaitwa na kupewa tena changamto na kukumbushwa kuifuata hiyo ramani. Hizi heri zatuonesha njia ya mbinguni. Twaitwa tuwatambue na tujitambue na wale walio maskini wa hali na mali, wanaolia, wapole, wenye njaa, wenye kiu ya haki n.k. zatumihiza tuwahurumie wengine, tuwe safi rohoni na kuwa watu wa amani kati ya mtu na mtu, na familia zetu katika jamii hata kama kufanya hivyo hakutupatii faida yoyote kwa sasa. Huku ndiko kuwekeza mbinguni. Watakatifu wetu hawa walifanya kadiri ya mapenzi yake Mungu. Sote twajua huwezi kupata bila kutoa, bila kuwekeza. Mtaka cha uvunguni sharti ainame.

Tutafakarishwe na mfano huu; bibi mmoja aliyekuwa tajiri hapa duniani, alipofariki akapata bahati ya kufika mbinguni. Malaika akampokea na akaanza kumwongoza kumpeleka mahali ambapo aliandaliwa kukaa. Akawa anakatiza mitaa ya mbinguni na kuona fahari zake na uzuri wake. Walipofika mahali alipopangiwa kukaa, akaona vitu vichache visivyo na uzuri na thamani ya pekee. Akamwambia yule malaika, mbona unaniweka hapa na vitu vilivyopo si vingi na vizuri kama walivyonavyo wenzangu? Malaika akamwambia bibi mpendwa ridhika na ulichopata. Vifaa vya ujenzi ulivyotuma toka duniani vilitosha tu kuandaa kibanda hiki. Malaika akamwacha akaenda zake. Nasi, Je, ni kitu gani na jinsi gani tunawekeza mbinguni?

29 October 2019, 14:07