Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXVI: Utajjiri wa dunia hii na dhambi ya kutowajali wala kuwathamini maskini! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXVI: Utajjiri wa dunia hii na dhambi ya kutowajali wala kuwathamini maskini! 

Tafakari Jumapili 26 Mwaka: Mali & Dhambi ya kutowajali maskini!

Ujumbe wa leo unatukumbusha kuwa tajiri na masikini wote ni wana wa Mungu, wameumbwa kwa sura na mfano wake, kwa lengo la kumjua kumtumikia na mwisho wafike kwake, hivyo wanapaswa kusaidiana kuufikia ufalme wa Mungu mbinguni. Hii pia ni Siku 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, changamoto kubwa ni kujenga utamaduni wa ukarimu kwa wageni na wahamiaji.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa leo unatukumbusha kuwa tajiri na masikini wote ni wana wa Mungu, wameumbwa kwa sura na mfano wake, kwa lengo la kumjua kumtumikia na mwisho wafike kwake, hivyo wanapaswa kusaidiana kuufikia ufalme wa Mungu mbinguni. Somo la kwanza la Nabii Amosi linaendeleza ujumbe wa jumapili iliyopiata wa kukemea tabia ya kujilimbikizia mali kwa matajiri wasijilimbikizie mali na mishahara mikubwa na kuwaacha watu wanateseka kwa kukosa mahitaji muhimu ya kimaisha. na kuwanyanyasi maskini na wahitaji pia viongozi waliopewa kibali cha kuwaongoza watu, wawaongoze vizuri, kwa kuangalia misingi ya haki na amani. Hii ni wakati wa utawala wa Yeroboamu wa pili ambapo Israeli ilipiga hatua kubwa sana kimaendeleo ambapo matajiri waliwakandamiza watu fukara, waliwauza utumwani walioshindwa kurudisha madeni yao, kwa kutoa rushwa walishinda kesi mahakamani na walidanganya vipimo vya uzito waliponunua mazao.

Katika somo la pili kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timotheo, Paulo anamwonesha Timotheo jinsi inavyompasa kuishi kama mtumishi wa Mungu, yaani aungame imani yake na kumwiga Yesu katika maisha ya kila siku. Namna hii ya kuishi yadaiwa kwa kila mkristo. Kila mkristo anapaswa na anawajibu wa kuifuata haki, utawa, imani, kuwa na upendo, saburi na upole, kuushika uzima wa milele alioitiwa. Katika Injili kama iliyoandikwa na Luka, inamwonesha Yesu anaendeleza fundisho la namna ya kutumia mali za dunia hii ili kwazo tuurithi ufalme wa mbinguni. Katika fundisho hili Yesu ametoa mifano mingi. Kwanza mfano wa tajiri aliyejibidisha kujiongezea ghala za kutunzia mazao yake, akamsahau Mungu na hata jirani zake wahitaji, Mungu akamwambia mpumbavu wewe leo hii tunahitaji nafsi yako na mali hii itakuwa ya nani? Kijana tajiri aliyemuuliza mwalimu mwema nifanye nini niurithi ufalme wa mbinguni, aliondoka kwa huzuni baada ya kushauriwa auze alivyonavyo awape maskini, katika tendo la kutoa sadaka Yesu anamsifia mjane fukara aliyetoa vyote kuliko matajiri walitoa fedha nyingi katika ziada zao.

Leo katika mfano wa tajiri na Lazaro, Yesu anasisitiza jinsi ilivyo vigumu kwa matajiri kuyatimiza matakwa ya Mungu, hata kama wakihubiriwa na mtu aliyefufuka. Hukumu aliyopewa tajiri ya kutupwa kwenye moto mwa milele, si kwa kuwa alikuwa na mali, bali kwa sababu alitumia vibaya mali aliyopewa na Mungu kwa ubinafsi. Mtakatifu Clement wa Alexandria anasema; “utajiri si mbaya katika wenyewe, uadilifu wake unategemea katika matumizi yake. Mtu tajiri anayefanya matumizi mazuri ya utajiri wake kwa kufanya matendo ya huruma ni bora kuliko maskini ambaye katika maisha yake anatamani utajiri. Kumbe yote tuliyojaliwa na Mungu, tunapaswa kuyatumia kwa mafao ya wengine wenye kuhitaji tena kwa upendo. Matokeo ya kuziba masikio yetu kwa kilio cha wahitahi ni hukumu ya moto wa milele kama tajiri aliyetajwa katika injili.

Utajiri uliopatikana kwa hila, kwa kuiba au kuwanyang’anya wengine kwa nguvu au kwa ujanja, kwa kuua, kufanya biashara zisizo halali kama kuuza dawa za kulevya, biashara haramu za binadamu mfano utumwa na ukahaba, kuwadhulumu wajane na yatima urithi wao, ufisadi wa mali ya umma hasa unaofanywa na wenye vyeo, kutumia sheria zisizo na haki, kuiba haki za wanyonge kwa rushwa na ufisadi au kuuza mali za umma, utakuwa ni ushahidi wa hukumu ya mwisho ambapo hukumu yake ni moto wa milele. Lakini pia utajiri uliopatikana kwa njia halali, usipotumika kuwasaidia wahitaji utatumika kutuhukumu, ndiyo maana katika mfano wa tajiri na Lazaro, mali alizokuwa nazo tajiri hazikuwa za wizi wala hazikuwa na ubaya na wala hakumtendea ubaya wowote Lazaro; hakumfukuza kutoka kwakwe. Hukumu yake imetokana na kutokujali kwake mateso na kilio cha Lazaro.  Utajiri binafsi usipozingatia manufaa ya Umma nao utakuhukumu siku ya mwisho. Tutambue kuwa kila kilichoumbwa na Mungu ni kwa ajili ya manufaa ya umma. Ingawa tuna haki ya kumiliki mali binafsi tunapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya manufaa ya umma kwani mali binafsi ni mali ambayo mtu anachukua sehemu ya mali ya umma kihalali na kuifanya binafsi ili azalishe kwa manufaa ya umma.

Hivyo, kuwasaidia wahitaji si jambo la hiari ni wajibu. Ndiyo maana Mtakatifu Paulo VI katika barua yake kitume “Populorum progressio” anasema, “Hakuna mtu mwenye haki ya kutumia vitu vya ziada wakati wengine hawana hata mahitaji muhimu”. Mt. Ambrose naye anasema, "Unapompatia maskini si kwamba unamsadia bali unamrudishia vilivyo yake ulivyomuibia. Kumbe ni kosa na ni dhambi kwa kurundika mali au pesa ya ziada bila kuitoa kwa manufaa ya umma, kwa kuwasaidia wahitaji au kuiwekeza ili kutengeneza mali zaidi na kutoa ajira. Ni kosa na ni dhambi kujilimbikizia ardhi au mashamba makubwa bila kuyaendeleza kwa manufaa ya umma hata kama uliipata kihalali. Ni kosa na ni dhambi kujitafutia mali wakati unaharibu manzingira. Kila mmoja wetu anaweza kushiriki katika dhambi ya kutowajali maskini: Iwapo atawachagua viongozi kwa kujua kuwa hawana moyo wa kuwasaidia wanyonge lakini anafanya hivyo kwa upendeleo wa kikabila au kwa manufaa yake binafsi, kwa kushiriki au kutoa ushahidi wa uongo ili kumnyang’anya mtu iliyo haki yake. Tunashiriki pia kwa kutokufanya hata yale mambo madogo yaliyo ndani ya uwezo wetu mfano, kuwafariji wanaoteseka, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa, kuwafariji wafiwa, kuwasaidia wagonjwa na kuwatetea wanaodhulumiwa.

Mungu ni Mfariji wa Maskini. Kama u mhitaji au umenyimwa haki yako usikate tamaa. Umtegemee Mungu. Wimbo wa katikati unatuambia: “Bwana huwafanyia haki walioonewa.” Tambua kuwa maisha mazuri hayapo katika wingi wa mali au pesa bali katika kufanya unayopaswa kufanya maana hayo ndiyo yatakayokustahilisha uzima wa milele. Tambua mema uliyojaliwa yawe machache yawe mengi na umshukuru Mungu kwa kuyatumia vema. Uwe mtu wa kuridhika na usiwe na uchu wa mali. Paulo anasema “Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na Imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi” (1Tim 6:10). Lakini wewe mtu wa Mungu uyakimbie mambo hayo tufanye kazi halali na kujipatia mali zetu kwa njia halali. Mwisho kila mmoja wetu ajiulize kama mali ulizo nazo hazinuki damu ya mtu yeyote, kama pesa uliyo nayo haijaloana machozi ya mtu yeyote, kama utajiri ulio nao hauna uvundo wa njaa ya maskini, wajane na yatima na hauna lawama yoyote. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari J26
30 September 2019, 07:40