Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria 2019: Sr. Magdaline Sidi ameadhimisha Jubilei ya Miaka 75 ya maisha ya wakfu; tarehe 21 Agosti 2019 akafariki dunia. Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria 2019: Sr. Magdaline Sidi ameadhimisha Jubilei ya Miaka 75 ya maisha ya wakfu; tarehe 21 Agosti 2019 akafariki dunia. 

Sr. Magdaline Sidi, Jubilei ya Miaka 75 ya Utawa! Kisha kifo, Mombasa!

Katika Sherehe za Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Sr. Magdaline Sidi wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa, Kenya aliadhimisha Jubilei ya Miaka 75 ya maisha yake ya kitawa kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Na katika mkesha wa Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa mbinguni, Sr. Madgaline Sidi, tarehe 21 Agosti 2019 akafariki dunia huko Mombasa.

Na Sr. Bridgida Samba Mawasi- Mombasa & Pd. Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti, Bikira Maria anawafundisha watu wa Mungu kumwadhimisha Mwenyezi Mungu kwa sababu amewatendea mambo makuu. Bikira Maria anawaalika watu kumwadhimisha Mungu kutokana na ukuu, uzuri na wema wake katika maisha yake. Waamini pia wanahamasishwa katika maisha, kuhakikisha kuwa, wanatafuta mambo makuu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao, kwani Mungu peke yake ndiye aliye mkuu vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wanazama na kutopea katika mambo madogo madogo ya maisha. Haya ni mambo ambayo wakati mwingine hayana mvuto wala mashiko! Hili ni tukio muhimu sana la imani kwani ndani mwake, waamini wanamwona Bikira Maria aliye palizwa mbinguni, mwili na roho.

Huyu ndiye yule Mama Bikira Maria aliyethubutu kushiriki katika Fumbo la Pasaka, na sasa anashiriki pia utukufu wa Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, ndiye Eva mpya na Kristo Yesu ni Adamu Mpya; kielelezo makini cha faraja na matumaini kwa wasafiri ambao bado wako huku bondeni kwenye machozi. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, lakini zaidi ni faraja kwa wale wanaoteseka; watu wanaohuzunika kiasi cha kupondeka moyo na hawana tena nguvu ya kuweza kunyanyua uso wao kwa matumaini. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondoa wasi wasi na hofu nyoyoni mwao, na wala tena hakuna umbali unaoweza kuwatenga kwani mbinguni kuna Mama Bikira Maria anayewasubiri kwa mikono miwili.

Ni katika muktadha wa Sherehe za Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, Sr. Magdaline Sidi wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa, Kenya aliadhimisha Jubilei ya Miaka 75 ya maisha yake ya kitawa kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyomkirimia katika maisha yake kama mtawa. Na katika mkesha wa Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa mbinguni, Sr. Magdaline Sidi, tarehe 21 Agosti 2019 akafariki dunia. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa ndiye aliyeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 ya maisha ya wakfu kwa Sr. Magdaline Sidi pamoja na watawa wengine  7 waliokuwa wanaweka nadhiri zao za daima. Wengi wao ni wale waliokuwa wanakumbukia Jubilei za nadhiri zao za miaka 25 na 60. Askofu mkuu Kivuva amelipongeza Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa kwa kuendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma, upendo na mshikamano wa watu wa Mungu unaomwilishwa katika huduma za maisha ya kiroho, katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii ndani na nje ya Kenya.

Hayati Sr. Magdaline Sidi ni kati ya watawa wa kwanza kabisa kujiunga na Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa hapo tarehe 8 Desemba 1940 na kuweka nadhiri zake za daima mwaka 1959, haikuwa rahisi sana kwa wakati huo! Sr. Magdaline Sidi ameitupa mkono dunia, akiwa na umri wa miaka 97 tangu alipozaliwa. Ndiyo maana alikuwa na kila sababu ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyomkirimia maishani mwake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Malkia wa mbingu na Malkia wa Mabikira. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde amemwelezea Marehemu Sr. Magdaline Sidi kwamba, kwa hakika alikuwa ni “mwanamke wa shoka” aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zake. Alikuwa ni shuhuda na chombo cha furaha ya Injili kutokana na ucheshi pamoja na upendo na mshikamano na watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao mbali mbali.

Ni mtawa pekee aliyepewa neema ya kushuhudia watawa wa kwanza wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa wakiweka nadhiri zao za mwanzo, matendo makuu ya Mungu. Marehemu Sr. Magdaline Sidi anazikwa kwenye makaburi ya nyumba mama ya Shirika la Masista wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa, Jumatano tarehe 28 Agosti 2019. Tukio hili linatanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Hospitali ya "Voi Shelter of hope", baadaye kutakuwa na mkesha hapo tarehe 27 Agosti 2019. 

Sr. Magdaline Sidi
26 August 2019, 12:27