Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu na ukarimu kwa maskini Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu na ukarimu kwa maskini 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 22 ya Mwaka C: Unyenyekevu!

Unyeyekevu ni fadhila na fadhila ni kuwa na mazoea na mwelekeo thabiti wa kufanya mema Fadhila ni tabia ya kudumu ya akili, dhamira au vionjo ambayo kwayo mtu aweza kutenda analotakiwa kimaadili katika nafasi fulani, au kutenda kwa njia sahihi, yaani akiwa na msukumo wa kufaa. Hivyo fadhila hutusaidia kutenda mema kwa wepesi, kwa urahisi, kwa kudumu na kwa furaha zaidi.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 22 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yamebeba ujumbe wa unyenyekevu, fadhila ambayo kwayo mtu hujitambua kuwa hajitoshelezi bali anamhitaji binadamu mwenzake ili amsaidie kujikamilisha na zaidi sana anamhitaji Mungu aliye ukamilifu wote. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua bini Sira latufundisha kuwa unyenyekevu upo katika kujua kuwa Mungu peke yake ni mkubwa na mwenye nguvu na ndiye ukamilifu wote. Mtu mnyenyekevu hajikuzi mbele ya wengine bali yupo tayari kuwahudumia wote wanaohitaji msaada wake ndiyo maana anasema, mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarimu. Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana ni kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu.

Somo la pili kutoka waraka kwa Waebrania linalinganisha Ufunuo wa Agano Jipya na Agano la Kale. Agano Jipya halikufanyika kwa vitisho kama lile la Kale bali katika utii na unyenyekevu wa Bwana wetu Yesu Kristo, utii na unyenyekevu hata mauti ya msalaba. Agano hili halikufanyika hapa duniani bali lilifanyika patakatifu mbinguni, kati ya Mungu Baba na Yesu Kristo, Mjumbe wetu; na tena sisi wakristo tumekwisha kushiriki maisha ya Kimungu na heri ya Watakatifu kwa Agano hilo. Injili ya leo ilivyoandikwa na Luka imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatufundisha kwamba tukitaka kuufaidi ufalme wa Mungu lazima tuwe wanyofu, wanyenyekevu na tutegemee msaada wa Mungu. Kristo anatuasa tusijikweze ili tusijedhiliwa, bali tuwe wanyenyekevu ili katika unyenyekevu wetu tuweze kukwezwa. Na sehemu ya pili inatuambia kuwa mapendo ya kweli ni kuwasaidia wale ambao hawawezi kutulipa kitu chochote. Tukifanya wema kwa maskini, vilema, viwete na vipofu ambao hawana uwezo wa kutulipa tunakuwa na heri ya kulipwa katika ufufuo wa wenye haki, yaani kuuridhi ufalme wa mbinguni.

Unyenyekevu ni nini? Unyeyekevu ni fadhila na fadhila ni kuwa na mazoea na mwelekeo thabiti wa kufanya mema. Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema fadhila ni tabia ya kudumu ya akili, dhamira au vionjo ambayo kwayo mtu aweza kutenda analotakiwa kimaadili katika nafasi fulani, au kutenda kwa njia sahihi, yaani akiwa na msukumo wa kufaa. Hivyo fadhila hutusaidia kutenda mema kwa wepesi, kwa urahisi, kwa kudumu na kwa furaha. Kuwa mwenye fadhila humaanisha kujisahau mwenyewe kwa ajili ya upendo wa Mungu unaojimimina kwetu.  Ni kuiga upendo wa Kristo, kujikana nafsi kabisa na kuwa mwanga wa upendo kwa Mungu na jirani. Mtume Paulo anapowaandikia Wafilipi anasema, ndugu zangu jazeni fikira zenu kwa mambo mema na yanayostahili kusifiwa, mambo ya kweli, bora, haki safi, ya kupendeza na ya heshima" (Wafil. 4:8). Ili kudumu kuwa mkristu mwema lazima kuamua kwa makusudi kujijengea mazoea yanayoendana na imani.

Mazoea hujenga tabia, mazoea yanayotokana na kurudiarudia hali, mwenendo au matendo safi na maadilifu. Mazoea yanayoendana na Injili huitwa fadhila. Kama fadhila nyingine zilivyo unyenyekevu unajengwa kwa matendo mema madogo madogo yak ila siku pasipokutegemea sifa na mtu yuko tayari kukosolewa anapokosea na kujirekebisha, mtu huyu daima anajitafakari kila mara juu ya udhaifu wake, anajikosoa na kujirekebisha na pia yuko tayari kusifia mafanikio ya wengine wala hajikwezi daima. Faida za kuwa mnyenyekevu. Unyenyekevu ni mama wa fadhila zote, humfanya mtu kuwaheshimu wengine na kumtegemea Mungu. Unyenyekevu unampatia mtu kibali cha kuonekana wa maana na wa muhimu na hivyo kupewa sifa na majukumu zaidi. Ni katika namna hii Yesu anasema, kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11. Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi. Kiburi ni kupenda makuu, kuwa na dharau, kujiona bora kuliko wengine, kupenda ufahari.

Mwenye kiburi hujikweza hata kwa sifa asizokuwa nazo na kuwadharau wengine, ana majivuno kuwa yeye ni bora kuliko wengine wote. Mwenye kiburi hayuko tayari kuwa chini ya Mungu au kuwa chini ya wenye mamlaka halali au wale wanaotawala na kuongoza kwa niaba ya Mungu katika mambo muhimu na halali (Rum 1:29-32). Yakobo anasema, mwenye kiburi humpinga Mungu na Mungu anampinga mwenye kiburi (Yak 4:6) daima anajiona mkamilifu mbele za wat una mbele za Mungu kama Mfarisayo aliyeenda hekaluni kusali (Lk 18:11-12). Athari za kuwa na kiburi ni kukosa unyenyekevu. Kiburi ni mzizi mkuu wa dhambi, kwani mwenye kiburi ukaidi hamuachi salama. Mwenye kiburi hawathamini wengine, mwenye kiburi hamtegemei Mungu, mwenye kiburi hujiona anajua yote, yeye ndiye kipimo cha ukweli, hivyo hawezi kutii sheria yoyote. Jamii yenye kiburi, inajiona kuwa inajitosheleza katika yote, inamwondoa Mungu kuwa ndiye chanzo cha ukweli hasa kuhusu maadili, inajifanya yenyewe ndiyo chanzo na kipimo cha maadili, inamwondoa Mungu kuwa ndiye lengo la maisha.

Jamii yenye kiburi haitambui kwamba furaha tunayoihitaji kama binadamu itakamilishwa kwa kumwona Mungu, kwa kuwa watu wake daima wanaitafuta furaha ndani mwao, kwa ajili ya hiyo watu wake hawawezi kutenda mema kwa sababu jamii imeondoa chanzo cha mema. Jamii ya namna hii haiwezi kuwa na furaha watu wake daima wanaishi katika kilindi cha huzuni. Ndiyo mtakatifu Agustino baada ya kuikosa furaha ya kweli katika viumbe alimwongokea Mungu na kusema, ee Mungu umetuumba kwa ajili yako na roho zetu hazitatulia kamwe mpaka pale zitakapotulia ndani mwako. Yoshua bin Sira anatuambia kuwa, “Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, mche wa uovu umepandika ndani yake,” YbS 3:28. Kushindwa kwa wengi katika maisha na hata kile walicho kadiri ya wito na nafasi zao hutokana na kiburi. Mshahara wa kiburi ni anguko lako mwenyewe. Kumbe nisichoke kuiomba hekima ya Mungu kila siku ili iniongoze katika busara. Na “moyo wa busara utatambua mithali, na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu,” YbS 3:29. Unyenyekevu utatuinua pale tunapojishusha pasipo shuruti kwani Yesu anasema, “kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11. Basi tumwombe Mungu atajalie fadhila ya unyenyekevu ili kwayo tuweze kutambua ukuu wake na kumtegemea yeye.

Jumapili 22 Mwaka C

 

27 August 2019, 15:45