Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya XVIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jilindeni na choyo pamoja na roho ya "korosho" Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya XVIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jilindeni na choyo pamoja na roho ya "korosho" 

Tafakari Jumapili XVIII: Jilindeni na choyo na ubinafsi!

Mama Kanisa kwa njia ya Liturujia ya Neno la Mungu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kubadili namna ya kufikiri na kutenda mintarafu mali na utajiri wa dunia hii. Anawataka waamini kuwekeza zaidi mali, utajiri na karama zao katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Mali na utajiri vyote vyatoka kwa Mungu!

Na Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Moyo wangu u katika vitu au utu na heshima ya mtu? Mali na utajiri na pesa na mambo kama hayo yanaweza kuwa chanzo cha kutuunganisha kama ndugu lakini pia yaweza kuwa chanzo cha magomvi na mafarakano hata kati ya ndugu wa damu, au marafiki walioshibana ikiwa mioyo yetu itajishikamanisha kiasi cha kuona thamani katika vitu na si mtu. Wapi naweka moyo wangu kwa watu au katika vitu, ni mwaliko katika Dominika ya leo kila mmoja wetu kuona ni nini kinaujaza moyo wake. Tunaweza kuwa na mifano mingi hasa ya ndugu waliofarakana kwa sababu za urithi kama ambavyo sehemu ya Injili ya leo tuliyoisikia.

Yesu anatualika kubadili namna zetu za kufikiri: Yesu alichukuliwa kama mtu mwenye hekima na busara au kama Rabi Mwalimu mwenye haki kati ya makutano, kwani katika mazingira ya mitafaruku ya namna ile wayahudi walisaka ushauri wa kutatua matatizo kwa mtu waliyeamini mwenye hekima na busara. Na ndio mtu mmoja anakwenda kwa Yesu kuomba aongee na ndugu yake ili aweze kumgawia sehemu ya urithi inayomwangukia kadiri ya Sheria ya Musa. Kwa mshangao tunaona Yesu hatoi jibu au ushauri kama alivyoombwa na mtu yule na badala yake anamuuliza ‘’Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?’’ Tunaona mmoja anadhurumiwa sehemu ya urithi wake na bado hatuoni kama Yesu anaguswa na tatizo hilo, hapo tunabaki na maswali kama sio kutokumuelewa vema Yesu kama mtu wa haki.

Mtu wewe ni mimi na wewe: Yesu anamuita, mtu wewe bila kumtaja jina ndio kusema hali ile si tu ilimkuta na kumuathiri yeye peke yake bali kila mwanadamu. Ni hali inayotugusa na kutukuta sisi sote bila kujali tofauti zetu mbali mbali na ndio Yesu anatumia fursa hii kututoa katika mzizi wa tatizo yaani uchoyo na ulafi wa mali. Hakika Yesu angeliweza kumpa ushauri wa kutatua tatizo la kugawanya urithi lakini mzizi haupo hapo bali ni ndani kabisa ya nafsi na mioyo yetu kama wanadamu.

Tujilinde na Prainoksia: ‘’Angalieni’’, Yesu anatualika kuwa macho, kuwa makini na mantiki ya ulimwengu huu na hivyo kutualika kubadili vichwa kwa maana ya kubadili namna zetu za kufikiri, kwani uzima wetu hautegemei mali au vitu tunavyokuwa navyo. Anatutahadharisha na choyo, na ndio tamaa mbaya ya mali na utajiri tunayokuwa nayo kiasi cha kutojali wengine, ni umimi na ubinafsi kwa kila kitu bila kuwafikiria wengine. Neno la Kigiriki ni prainoksia, ndio ile tamaa kali na mbaya kabisa inayokuwa ndani mwetu ya kutaka yote yawe yangu bila kujali wengine.  Ni ugonjwa wa ubinafsi na umimi, kuwa bwanamakusanya, yote yawe yangu na kujikusanyia mengi au vingi kadiri niwezavyo.

Utajiri na vyote tulivyonavyo ni mali ya Mungu: Ni tamaa hiyo mbaya inayotupelekea kusahau na kufikiri kuwa mali au vitu tulivyo navyo ni mali yetu binafsi, na hapo kusahau kuwa mema yote ninayokuwa nayo ni MALI YA MUNGU, hivyo mimi ni mlinzi tu, ni mwangalizi tu wa mali ile, ni kijakazi tu wa mali hiyo ya Mungu na hivyo sina budi kuisimamia vema kwa kumwangalia na kumjali mwingine. Ni katika muktadha huo tunajikuta kuwa badala ya kuwa wasimamiaji wa mali ya Mungu tunageuza mali zile kuwa miungu, na hapo tunaanza kuabudu mali badala ya Mungu. Na ndio Yesu leo anatualika kubadili vichwa kwa maana ya mtazamo na mantiki zetu mintarafu vitu au viumbe.

Upumbavu wa mkulima tajiri: Yesu anatumia mithali ili kutufundisha zaidi na ndio anatumia mfano wa mkulima tajiri aliyepata mavuno mengi.  Shamba la mkulima tajiri lilikuwa limezaa sana, na kwa hakika alipata mavuno mengi kwa sababu ya uchapakazi wake na hivyo si kwamba aliiba au alidhurumu mtu, bali alifanyakazi kwa bidii na ustadi mkubwa, alitoka jasho haswa. Kwa Tanzania ya Hapa Kazi tu, basi mtu huyu anabudi kusifiwa na kupongezwa kwa uchapakazi wake mzuri. Ila bado Yesu anamtambulisha mkulima huyu tajiri kama mpumbavu, hapo tunabaki na maswali kwa nini awe mpumbavu na sio wale wavivu na maskini hohehahe waliobaki bila mavuno kwa kuwa hawakufanyakazi kwa bidii na ustadi mkubwa?

Katika mithali tunaona wahusika wakuu ni Mungu, mkulima tajiri na mazao yake mengi.  Si tu tuna haki ya kushangaa kwa nini Yesu anamuita mpumbavu, bali hata tunajiuliza, je mkulima huyo tajiri hakuwa na familia, mke au watoto, au majirani, au marafiki, au ndugu au wajuani au hata vibarua wake shambani?  Hakika alikuwa nao na hasa wafanyakazi wake kwa hakika, kama sio majirani na watu wa familia yake. Anaishi na watu ila mbele yake haoni watu bali anaona mali zake. Ndio ile tamaa kali na mbaya tunayoitambua kama prainoksia, ni tamaa inayoleta upofu na uziwi hivyo huwezi kuona mtu mwingine yeyote zaidi ya mali zako, inayokuja kwa nafasi ya kwanza ni mali na si mtu au Mungu. Ni mtu anayekosa muda, hata fikra, au maneno au nafasi kwa ajili ya wengine kwani kwake ni mali tu iwe akiwa macho au hata alalapo.

Hata yeye mwenyewe anapoteza utu wake kwani amekuwa ni sawa na mashine kwa ajili ya kuzalisha tu na si mtu anayeakisi sura na mfano wa Mungu na hivyo kuguswa na watu wanaomzunguka. Anageuka kuwa kitu, ni sawa na mashine kwani kuwaondolea wengine utu nasi mwishoni tunaishi bila huo utu. Hivyo si tu inaleta madhara kwa kukosa kuona utu kwa wengine bali hata nasi tunabaki bila thamani na utu kama wanadamu. Mkulima tajiri anakuwa naye ni maskini na mtu wa kuonewa huruma kwa kupoteza si tu utu na thamani ya wengine bali hata na utu wake mwenyewe.  Katika maneno yake anayojiongelesha yeye mwenyewe, maana hana nafasi hata ya kuongea na mwingine bali anakuwa na ubinafsi hata katika maongezi, ni yeye tu anayeishi na hivyo lazima kujiongelesha yeye mwenyewe. Leo tukikutana na mtu anayejiongelesha mwenyewe tunaanza kusema amechanganyikiwa, na ndio maana Yesu anamtambua kama mpumbavu.

Hata katika kujiongelesha yeye mwenyewe anatumia mara 14 maneno kama mimi, mali yangu, vitu vyangu, ghala langu, nafsi yangu na mengine kama hayo yanayomuhusu yeye tu. Ni yeye na mali yake tu, kwa hakika ni mpumbavu! Ghafla anaingia sasa muhusika wa tatu ambaye ni Mungu. Si kwamba Mungu anatenda kwa namna hiyo bali Yesu anatualika mimi na wewe leo kubadili namna zetu za kufikiri na kuenenda katika maisha mintarafu mali na vitu. Ni kutukumbusha kuwa vyote tulivyo navyo si mali yetu bali ni zawadi kutoka kwa Mungu iwe ni vipaji vyetu mbali mbali, elimu na ujuzi na utaalamu wetu, iwe ni vitu au mali, vyote ni mali ya Mungu na ni kwake tu tutatoa hesabu ya mwisho kwa jinsi tulivyovitumia tungali hapa ulimwenguni. Narudia Mungu daima ni mwema na anatujalia mema mengi hata tukiwa sio wakarimu kwa wengine, sio kwa sababu anatujaribu ila kwa sababu wema wake haujui kubagua au kutenga wengine kwani ametujalia ndani mwetu na ndivyo tulivyoumbwa uwezo wa kumpenda jirani.

Si lengo la Mungu tangu kuumbwa ulimwengu kuwa mwanadamu aishi katika umaskini na kupungukiwa, bali mali na vitu tunavyokirimiwa katika maisha hatuna budi kukumbuka daima ni mali yake na hivyo sisi tunabaki kuwa wasimamizi tu. Mkulima tajiri anaitwa mpumbavu sio kwa sababu alifanya kazi kwa bidii na kupata mavuno mengi bali kwa kujifikiria yeye mwenyewe tu na kukosa kuwa mkarimu. Ni mwaliko hata nasi tunapojaliwa mema kuwashirikisha wengine wanaokuwa hawana au kutojaliwa kama sisi. Kila mkate wa ziada ndani mwangu unikumbushe ndugu wengi wanaolala na njaa leo, hivyo kila mara hatuna budi kuwafikiria na wengine. Duniani leo kuna watu wangapi wanakufa na njaa au kukosa dawa au kwakosa makazi ya kuishi na wangapi kati yetu tunaishi kwa ziada bila kuguswa, na mbaya hatuguswi hata na wanafamilia wetu au ndugu zetu wanaokuwa katika uhitaji mkubwa hata na wale tunaoishi nao?

Utajiri na mali daima vitukumbushe wajibu wetu kwa wengine na pili nafasi ya Mungu katika maisha yetu kuwa ndiye mtoaji wa mema yote kwani yatoka kwake. Hivyo tusiabudu mali bali Mungu pekee, mali na utajiri ni zawadi kutoka kwa Mungu na hivyo hatuna budi kutumia mali kwa shukrani na upendo kwa Mungu na jirani ili tusiwe kama yule mkulima tajiri mpumbavu aliyefikiria juu yake tu na mali zake bila kuona wengine au nafasi ya Mungu. Yesu anatuonya dhidi ya choyo na ulafi wa mali na hali hii haitegemei tu mpaka mtu awe tajiri kwani hata wengine katika madogo tunayokuwa nayo daima tunaalikwa kuwa wakarimu kwa wengine. Wapo watu wenye utajiri mkubwa na bado wanatumia mali zao kwa ukarimu kuliko wale wanaokuwa maskini kwani yawezekana sina utajiri ila hata kile kidogo siwezi kumshirikisha jirani yangu au mwingine, ni hali ya namna hiyo Yesu leo anatuonya kuwa macho. Namalizia kwa kurudia maneno ya Yesu katika Injili ya leo, ‘’Jilindeni na choyo’’. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

03 August 2019, 14:38