Patriaki Bartolomeo wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika ujumbe wake kwa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, amekazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Patriaki Bartolomeo wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika ujumbe wake kwa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, amekazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. 

Sherehe: Watakatifu Petro & Paulo: Dhana ya Sinodi katika Kanisa!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo kwa mwaka 2019, amekazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Makanisa haya mawili. Mitume hawa walikuwa kweli ni mashuhuda, kiasi hata cha kuvishwa taji la kifo dini, mwanga angavu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Uekumene ni kujenga umoja katika utofauti. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza viongozi na waamini wa Makanisa mbali mbali kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, ili kushirikishana na kuhudumiana ili hatimaye, kuvunjilia mbali hofu na mashaka yasiyokuwa na mashiko, tayari kujenga umoja wa Kanisa. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu! Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa  Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, uliohudhuria Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba wa imani, hapo tarehe 28 Juni 2019.

Baba Mtakatifu katika kilele cha maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Jumamosi, tarehe 29 Juni 2019 ametambua uwepo wa ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, mwendelezo wa mapokeo kwa Makanisa haya mawili kufanya hija ya pamoja. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza  hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko!

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo kwa mwaka 2019, amekazia umoja, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Makanisa haya mawili. Mitume hawa walikuwa kweli ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kiasi hata cha kuvishwa taji la kifo dini ambalo ni mwanga angavu wa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye ni mwanga angavu na utukufu wa Baba wa milele unaoburudisha nyoyo za waja wake.

Huu ni mwaliko kwa Makanisa haya kuanza kujielekeza zaidi, ili hatimaye, kukumbatia na kuambata upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Haya ndiyo matumaini makubwa yanayooneshwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kama kiini na lengo kuu la majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili. Umoja katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kati ya majadiliano ambayo yamedumu kwa takribani miaka arobaini kwa sasa. Mchakato wa ujenzi wa umoja; udugu sanjari na uekumene wa sala na huduma ya Injili ni changamoto kubwa kwa Makanisa haya mawili kujielekeza katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kutunza na kudumisha amana ya ukweli na imani. 

Ni wajibu wa Makanisa haya mawili kuendeleza Mapokeo ya Kitaalimungu, Maisha ya kiroho na Sheria za Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mitume na Mitaguso ya Kiekumene, kama chemchemi rejea katika mchakato wa ujenzi wa umoja kamili wa Kanisa, umoja unaosimikwa katika utofauti! Tume ya Kiekumene ya Majadiliano ya Kitaalimungu Kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox imekwisha kupiga hatua kubwa na hatimaye, kuchapisha Nyaraka muhimu kuhusu “Ukuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Dhana ya Sinodi kadiri ya Karne ya Pili na Umuhimu wake katika Ulimwengu mamboleo”.

Tume hii ya Kimataifa inaendelea kuboresha muswada wake ili hatimaye, kujenga na kudumisha umoja wa Makanisa haya pacha. “Dhana ya Sinodi” inaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kama chachu ya umoja na mshikamano wa Kanisa; ili kukuza na kudumisha utakatifu wa watoto wa Mungu ambayo kimsingi ni sadaka safi mbele ya Mwenyezi Mungu! Hapa kuna umuhimu wa kukazia “Ukatoliki wa Kanisa”. Ukuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa unaozingatia amani na utulivu wa ndani.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya umoja na upendo wa Kristo kwa Kanisa lake na utambulisho wa Kikristo. Umoja huu unaendelea kujengeka katika uekumene wa sala kama ilivyojionesha tarehe 7 Julai 2018 kwa viongozi wa Makanisa kuungana pamoja kwa ajili ya Siku ya Sala ya Kiekumene huko Bari, Kusini mwa Italia, kwa ajili ya kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”. Ilikuwa ni fursa ya kusali na kuombea amani na upatanisho.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus, Bari, linahifadhi masalia ya Mtakatifu Nicholaus anayeheshimiwa sana na Makanisa ya Mashariki. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, amani ya kweli kamwe haijengwi kwa mtutu wa bunduki, bali kwa njia ya Injili ya upendo ambao hautafuti mambo yake kama anavyobainisha Mtakatifu Paulo katika utenzi wake kuhusu upendo. Mafuta ya imani yatumike kuganga na kuponya madonda ya kihistoria na kamwe waamini wasiwashe tena moto wa chuki na uhasama. Matatizo na changamoto za Makanisa haya mawili zitatuliwe ili kweli umoja wa Kanisa uweze kuwa na mvuto na mashiko!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza

 

02 July 2019, 15:01