Mababa wa SECAM kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa SECAM wametoa Wosia unaopawa kuzingatiwa na familia ya Mungu Barani Afrika. Mababa wa SECAM kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa SECAM wametoa Wosia unaopawa kuzingatiwa na familia ya Mungu Barani Afrika. 

SECAM: Wosia kwa familia ya Mungu Barani Afrika: Muhimu!

Mababa wa SECAM wanasema, Kanisa Barani Afrika halina budi kuwekeza zaidi katika Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Maadili, Malezi ya Maisha ya kiroho. Waamini waendelee kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa, ili kusaidia mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yamefikia kilele chake Jumapili tarehe 28 Julai 2019 kwa Ibada ya Misa iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Mababa wa SECAM katika Ujumbe wao kwa Watu wa Mungu Barani Afrika na Madagascar wanakazia umuhimu wa Jubilei kama muda wa kushukuru, muda wa kujenga umoja na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa! Ujumbe kwa familia ya Mungu Barani Afrika unaoongozwa na kauli mbiu “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh. 13:3: 10:10).

Mababa wa SECAM wameambatanisha pia mwaliko kwa familia ya Mungu kujizatiti zaidi katika imani, kwa kuendeleza toba na wongofu wa ndani. Mababa wa SECAM wanaendelea kuboresha “Hati ya Kampala” itakayotoa dira na mwelekeo wa Kanisa Barani Afrika kwa siku za usoni! Mababa wa SECAM wametoa wosia unaopaswa kuzingatiwa na familia ya Mungu katika ujumla wake kwa kukazia mambo yafuatayo! Mababa wa SECAM wanasema, Kanisa Barani Afrika halina budi kuwekeza zaidi katika Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Maadili, Malezi na Majiundo ya Maisha ya kiroho kwa waamini Barani Afrika. Waendelee kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa, ili kusaidia mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Watakatifu na mashuhuda wa imani kutoka Barani Afrika, wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa kujikita katika imani yao bila kuyumbishwa “kama daladala iliyokatika usukani”. Waamini wa Kanisa Katoliki wawe makini na sera na mikakati inayosigana na imani, kanuni na maadili ya Kanisa Katoliki. Mababa wa SECAM wanawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ambazo ni utambulisho wa Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika. Waamini wahamasike kujiunga na vyama na mashirika ya kitume, ili kulea na kukuza imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, na kama sehemu ya ushiriki wao mkamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Utume wa familia unapaswa kuvaliwa njuga na Kanisa Barani Afrika, ili kweli familia ziweze kuwa ni chombo na shuhuda wa unabii katika jamii.

Kuna haja kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kujizatiti zaidi na zaidi katika majiundo ya watu wa Mungu: kitaaluma, kimaadili na katika maisha ya kiroho kwa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanarithishwa tunu msingi za kiinjili, kimaadili na utu wema, kuanzia kwenye familia zao, ili kuwakinga na uwezekano wa kutumbukizwa katika misimamo mikali ya kidini na kiimani; fujo na ghasia mbali mbali. Familia ya Mungu Barani Afrika inahimizwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko pamoja na kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kutumia kwa umakini mkubwa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Mababa wa SECAM wanakumbusha kwamba, hata njia za mawasiliano ya jamii zinapaswa kuinjilishwa pia!

Mababa wa SECAM wamegusia umuhimu wa uekumene: wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa watu wa Mungu Barani Afrika sanjari na majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kanisa Barani Afrika halina budi kuendelea kushirikiana na kushikamana na viongozi wa kisiasa, kuwasaidia kuwajibika zaidi, ili kutafuta na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika uwe ni kwa ajili ya kuchochea mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu yanayowaambata watu wote, daima misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, ikipewa kipaumbele cha kwanza.

Serikali Barani Afrika hazina budi kujipanga kikamilifu ili kukabiliana na mambo yanayosababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Sera na mikakati hii isaidie pia kuzuia na kudhibiti biashara ya binadamu na utumwa mamboleo Barani Afrika. Mababa wa SECAM wanalitaka Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika, COMSAM, kuishi kweli za wito wake, kwa kuwa ni chombo na shuhuda wa uinjilishaji. Katika Majimbo ambayo kuna uhaba mkubwa wa Mapadre hasa Kaskazini mwa Bara la Afrika, uwepo utaratibu wa kupeleka wamisionari watakao jizatiti kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, jambo la msingi yawepo mawasiliano na Kanisa la Kiulimwengu! Mababa wa SECAM wamekazia kwa namna ya pekee malezi na majiundo ya wakleri na watawa Barani Afrika, ili kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya karibu na Kristo Yesu.

Mababa wa SECAM wanawataka waamini kukazia ukomavu wa maisha ya kiroho, kiutu. Wajenge na kudumisha ndani mwao ari na mwamko wa huduma kwa watu wa Mungu; daima wakiwajibika mbele ya Mungu na Kanisa. Waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake Barani Afrika. Waamini walei wanakumbushwa kwamba, wameitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya tunu msingi za kiinjili. Nyenzo msingi wanazopaswa kuwa nazo ni Biblia Takatifu, Katekesimu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki. Makanisa mahalia yaendelee kujibidisha kutoa malezi na majiundo makini kwa wafanyakazi wa umma pamoja na wanasiasa, ili kusimama kidete kupambana na rushwa, ufisadi wa mali ya umma pamoja na mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema. Kanisa liendelee kukazia misingi ya utawala bora pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali na utajiri wa nchi husika.

Wakristo Barani Afrika wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; washirikiane na kushikamana kupambana na: magonjwa, umaskini na ujinga maadui wakubwa wa maendeleo Barani Afrika. Huduma ya kichungaji na maisha ya kiroho kwa wafanyakazi wa sekta ya afya bado ni muhimu sana. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wataalam na wasomi Barani Afrika waendelee kufanya tafiti na kuzichapisha kuhusu: Dini asilia Barani Afrika, Uislam, Madhehebu ya kidini yanayoendelea kuibuka kila kukicha, jamii za kisiri pamoja na matatizo na changamoto zinazoibuliwa na imani za kishirikina. Mwishoni, Mababa wa SECAM wanawataka wadau mbali mbali wa vyambo vya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, wanasaidia kueneza uelewa wa SECAM katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Tamko la Kampala, likisha kutolewa litakuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Hati hii ikisha kutolewa basi iendelee kusambazwa sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

SECAM: Wosia

 

31 July 2019, 15:22