Vatican News
Kristo Yesu anaendelea kuwaita wafuasi wake, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu pamoja na jirani zao! Wito una ugumu, masharti na changamoto zake! Kristo Yesu anaendelea kuwaita wafuasi wake, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu pamoja na jirani zao! Wito una ugumu, masharti na changamoto zake! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XIII: Wito na changamoto zake

Kristo Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu ili kutimiza maisha na utume kwa mateso, kifo na hatimaye ufufuko wake, anatoa changamoto kwa wale wanaotaka kumfuasa kuhakikisha kwamba, wanaambatana naye, ili hatimaye kujifunza kutoka kwake. Anawataka wafuasi wake kuwa na msimamo thabiti wanapoamua kuacha yote kwa jili ya huduma kwa Mungu na jirani zao!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma

Katika Pwani ya kusini ya Ziwa Tanganyika lipo Kanisa moja na katika mimbari iliyopo kanisani, kipo kibao cha bati ikionesha kumbukumbu ya mmisionari mmoja kwa jina James Lawson. Huyu alijitoa kwa maisha ya umisionari na baada ya majiundo yake alitumwa Afrika. Pamoja na maandalizi yake yote ya maisha ya umisionari na changamoto alizokutana nazo za lugha, mila na desturi, mazingira mapya n.k baada ya mwaka mmoja wa umisionari pale Kigoma alifariki dunia. Katika hali ya kawaida ni hasara kubwa. Lakini sivyo ukristo unavyotafsiri kifo hicho. Katika kibao hicho cha kumbukumbu yake kuna maneno haya – ‘siyo kile ulichofanya ila kile ulichohangaikia au kutamani kufanya’. Pengine hiki ndicho kipimo cha ukristo wetu, umisionari wetu kama wabatizwa. Pengine mfano huu wa maisha ya ushuhuda ungetosha kukamilisha mahubiri yetu ya leo. Kinachobaki ni sisi kuweka katika matendo. Lakini basi tuongezee machache kwenye tafakari yetu ya leo.

Ndugu zangu, wito wa Mungu si kitu ambacho kinaenda kwa mpangilio maalumu kadiri ya uelewa wa kibinadamu. Angalia jinsi ilivyo katika somo la 1, jinsi nabii Eliya anavyomtupia Elisha vazi lake la kinabii ikimaanisha wito wake kumtumikia Mungu. Elisha alikuwa katika shughuli zake. Hakutegemea kuitwa namna hiyo katika maisha yake. Kwa kupakwa mafuta, anakuwa mfuasi wa Eliya na mrithi wake. Na tangu siku hiyo maisha yake yanachukua mtindo mwingine kabisa. Mipango na harakati zake zote zinachukua mkondo mpya. Anamtumikia Mungu. Katika Injili ya leo twaona jinsi mwinjili Luka anavyoonesha mwenendo mzima wa maisha ya Yesu – toka sura hii ya 9 na kuendelea -  kwamba ni njia endelevu kwenda Yerusalemu, ambapo atapata mateso, kifo lakini pia ufufuko wake.

Akiwa safarini anawafundisha wafuasi wake. Kwa ustadi mkubwa anawaita wafuasi wake na anawataka kuwa makini na wavumilivu. Pia anawakumbusha juu ya nguvu ya maamuzi – au kumfuata yeye au kumkataa. Anawaalika kuwa waangalifu na nguvu au vifungo binafsi, familia na hali yo yote ile inayoweza kuzuia kumfuata. Anaonesha wazi kuwa ufalme wa Mungu una thamani kubwa zaidi (absolute value) kuliko hali zetu, chaguzi zetu na yote tuliyonayo au tutamaniyo kufanya. Swali la kawaida kabisa la kibinadamu linalofuata ni hili – je yawezekana kumfuata Bwana? Jibu anatoa mtume Paulo katika somo la 2. Ni roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo.

Maisha ya umisionari ya Dr. David Livingstone yaweza kutusaidia kuelewa neno la Mungu siku ya leo na namna ya kuitika na kuishi wito huu. Huyu alikuwa mmisionari, mvumbuzi na tabibu. Alifanya kazi na kufariki maeneo ya Afrika Mashariki na Kati. Stanley alisikia habari zake na alifunga safari toka ulaya kumtafuta mtu huyu maarufu duniani. Walikutana Ujiji na tangu hapo Stanley akabaki naye. Stanley alishiriki utume wa Livingstone na maisha yake ya kila siku. Stanley hakuwa mkristo na anashuhudia mwenyewe kuwa jinsi Livingstone alivyotumia muda wake kuwasilikiliza watu na kuwatibu na kuwapa nafasi ya kutambua upendo wa Mungu, ilitosha kuomba kubatizwa. Hakuhitaji kufundishwa katekisimu. Huu ni ushuhuda tosha wa maisha ya wito wa kikristo.

Ndugu wapendwa, tukumbuke kuwa hatuwi wakristo kwa hiari yetu bali ni neema ya Mungu inayofanya hilo liwezekane. Hata maendeleo yetu ya ukristo wetu hayategemei nguvu zetu wenyewe. Ni upendo wa Mungu unaotujalia nguvu. Ni uwepo endelevu unaofanya mageuzi na uongofu uwezekane kila siku. Sisi nafasi yetu ni kusikia sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi yake – Mt. 7: 21-29. Mtu mmoja alimwuliza Padre ni jinsi gani ajitolee maisha yake kwa Mungu, jinsi gani afanye ili apate kuongoka. Yule padre alitoa karatasi nyeupe isiyoandikwa cho chote na kumwambia inatosha kuandika jina lako na kuweka saini chini/sehemu ya chini ya karatasi na kumwacha Mungu ajaze mapenzi yake sehemu iliyobaki wazi. Nasi pia hatuna budi kumwachia Mungu aandike upya ukurasa wa maisha yetu.

Hilo ndilo dai la maisha ya ufuasi. Sisi tunamtaka Mungu katika maisha yetu lakini tunataka kutimiza kwanza mapenzi yetu wenyewe. Haiwezekani kumwekea Mungu masharti. Tunaalikwa tuyapokee na kuishi mapenzi yake. Yesu ameweka wazi katika injili ya leo. Yesu kwanza. Je, katika kushiriki kwetu katika ujenzi wa taifa la Mungu tukoje. Kama wale Wasamaria? Au yule aliyetaka kumfuata au yule aliyeitwa lakini anataka kwanza akazike mfu wake au yule aliyetaka kwanza kwenda kuaga familia yake ndipo aje amfuate Bwana? Yesu anaweka wazi taratibu za ufuasi. Nasi tuombe daima neema na baraka ya roho wake ili tuwe waaminifu katika kumtumikia yeye. Tumsifu Yesu Kristo,

01 July 2019, 09:34