Ekaristi Takatifu ni masurufu ya njiani kuelekea uzima wa milele! Ni sadaka ya sifa na shukrani! Ni karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao! Ekaristi Takatifu ni masurufu ya njiani kuelekea uzima wa milele! Ni sadaka ya sifa na shukrani! Ni karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao! 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Kumbu kumbu na Shukrani!

Ekaristi Takatifu ni sadaka ya sifa katika shukrani kwa ajili ya kazi ya uumbaji na ukombozi iliyotendwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Ni sadaka ya shukrani na baraka kwa Mungu Mwenyezi. Kumbu kumbu na uwepo endelevu wa Kristo kati ya wafuasi wake, hadi atakaporudi kwa utukufu! Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu yaani Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ni: Kumbu kumbu ya sadaka ya Kristo Yesu na ya Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya sifa katika shukrani kwa ajili ya kazi ya uumbaji na ukombozi iliyotendwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu.  Ni sadaka ya shukrani na baraka kwa Mungu Mwenyezi. Kumbu kumbu na uwepo endelevu wa Kristo kati ya wafuasi wake, hadi atakaporudi kwa utukufu kuwahukumu wazi na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao!

Ni sherehe ya shukrani yetu kwa Mungu kwa uwepo wa Kristo kati yetu - upendo uonekanao katika Ekaristi. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kumbukumbu hii ni fumbo kubwa na lenye nguvu kwa maisha ya mwamini. Katika fumbo la ekaristi kuna nini? Ni kumbukumbu ya nini?Kumbukumbu hutokana na kilichoonekana, kilichosikika na kilichofanyika hasa utotoni na huhifadhiwa kwenye fuvu na huamka tena na tena au kwa msukumo wa ndani au mvuto wa nje. Bila kumbukumbu tungepoteza umimi wangu, kitambulisho changu. Waliopatwa na ugonjwa wa “amnesia” – hupoteza kabisa mwelekeo – hawajui walipo, hawana kumbukumbu ya jina lao na hata waishipo.

Kumbukumbu ikiungana na akili – inatoa msukumo kuelekea kitu au ikikamilika kabisa humwelekea mtu – mfano mama akimkumbuka mtoto wake, atamwona mtoto wake tu na mengine yote husahaulika. Tukumbuke silika ya mnyama kwa mtoto wake. Nguvu ya kumbukumbu huonekana pia katika maisha ya familia fulani, kabila fulani au taifa fulani. Huweza kukumbuka jambo fulani kwa pamoja. Utajiri wa watu haupimwi na wingi wa dhahabu bali kwa wingi wa kumbukumbu walizo nazo katika dhamiri na matendo yao. Kumbukumbu hizo zikiwekwa pamoja – kundi hufanyika. Ili kumbukumbu hizo ziendelee huunganishwa na mahali, tukio au sikukuu – na huadhimishwa hadharani. Sisi kama taifa la Tanzania huadhimisha sikukuu au kumbukumbu fulani kwa mfano sikukuu ya uhuru wa nchi, kumbukumbu ya mwalimu Nyerere.

Sisi kama Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Ekaristi n.k. Ni muhimu sana – hutukumbusha adhimisho la uzima - Ekaristi, Sakramenti ya uzima - Sherehe inatukumbusha hilo kinyume chake = kufuru - 1 Kor 11,29-30 – maana mwenye kula na kunywa bila kufanya tofauti kati ya mwili na chakula cha kawaida anajilia na kuinywea  hukumu. Kwa hiyo wengi wenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine wa kutosha wanafariki Hatari ya kumbukumbu – huweza kuwa tasa au "nostaligia" – ung’ang’anizi usiokuwa na maana sana wa mambo yaliyopita. Au kufanya kwa mazoea tu. Hupelekea kupokea Ekaristi kwa mazoea au kutokupokea kabisa Ekaristi – kwa sababu ambazo zinazojulikana kibinafsi.

Kwa nini Yesu atupatie Sakramenti hii? Kwa sababu aliahidi kuwa nasi mpaka mwisho wa nyakati – Mt. 28,20. Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani mwake. Katika ekaristi tunakutana naye,Yesu Kristo mzima. Hii ni kumbukumbu na uwepo wake chini ya maumbo ya mkate na divai. Yesu alisema nimekuja ili muupate uzima tena tele – Yoh. 20,20 – hivyo aulaye mwili wa Kristo na kunywa damu ya Kristo, hupata uzima wa milele na hutakiwa kuutoa uzima huo kwa wengine. Kumbukumbu ya sherehe ya uhuru au kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere au maaskari mashujaa – waliofia nchi yetu haiwezi kamwe kuwarudisha  hai – tunakumbuka lile tendo au kile kilichotokea na kutakiwa kuenzi na kufanyia kazi.

Imani ya Kikristo katika Sakramenti ya Ekaristi – hutupatia nafasi ya kumpokea Kristo aliye hai - katika Yoh 6: 53-54 – Yesu akawaambia. Amin, amin, nawaambieni, msipoula mwili wa Mwana wa Mtu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuiynwa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamufufua siku ya mwisho - hii lugha ya kisakramenti haikueleweka: tofauti ni kwamba chakula cha kawaida tulacho mwili wetu hukibadilisha. Ekaristi hutabadilisha na kutufanya mwili wa Kristo. Adhimisho la Ekaristi hutupeleka mbele zaidi, baada ya mageuzo twaitikia – tunatangaza kifo chako na kutukuza ufufuko wako mpaka utakapokuja. Mtakatifu Thomas wa Aquino katika antifona (O SACRUM CONVIVIUM) anaeleza Ekaristi kama Sikukuu takatifu ambayo Kristo anapokelewa, kumbukumbu ya mateso husherehekewa, roho zinajazwa na neema, nasi tunapata ahadi ya utukufu wa milele ijayo. Tumsifu Yesu Kristo.

17 June 2019, 14:43