Vatican News
Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Askofu Method Kilaini: Chimbuko na umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo katika maisha na utume wa Kanisa Tanzania na Afrika Mashariki. Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa Walei Tanzania: Askofu Method Kilaini: Chimbuko na umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo katika maisha na utume wa Kanisa Tanzania na Afrika Mashariki. 

Jubilei Miaka 50: Utume wa Walei Tanzania: Jumuiya Ndogondogo

Jumuiya Ndogo Ndogo ni sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji uliobuniwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni shule ya Neno, Sakramenti na matendo ya huruma: Ni chachu ya ujenzi wa ujirani mwema; Uinjilishaji wa kina; chemchemi ya maisha ya kiroho na sehemu ya muundombinu ya Kanisa!

Na Askofu Methodius Kilaini, - Da re Salaam, Tanzania.

Mwamko uliounda Halmashauri ya Walei ndio huo huo uliounda Jumuiya Ndodo Ndogo za Kikristo. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ulisisitiza sana juu ya muundo wa umoja wa walei ambao ungelishirikiana kwa karibu na Wakleri, na watawa katika nyanja zote za kanisa.[1] Kwa upande mwingine Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulisisitiza sana Kanisa liwe familia ya Kristo na liishi kama familia kwa mfano wa kanisa la kwanza la mitume. Mitume walijenga familia moja hata kwenda mbali kushirikiana siyo tu mambo ya kiroho bali hata mali zao. “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate na katika kusali”(Mdo: 3:42)

Baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa lilianza kutafuta njia bora ya kuishi kama familia ya Mungu. Kanisa lilijaribu kupata maisha mfano wa karibu iwezekanavyo kurudia maisha ya kanisa la mwanzo la mitume Yerusalemu. Katika Amerika ya Kusini waliunda ‘Jumuiya za msingi za Kikristo’[2].  Kule Kongo Kinshasa chini ya Askofu Malula hata kabla ya Mtaguso Mkuu wa Vatikano II walikuwa tayari wanatafuta njia za Kiafrika za kuishi maisha hayo. Ikumbukwe pia kwamba Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ulisisitiza juu ya kuchimbia kanisa katika utamaduni wa watu mahalia.  Baada ya Mtaguso katika nchi za AMECEA semina na utafiti ulifanywa kutafuta namna ya kuishi maisha haya ya kanisa kama familia ya Mungu na kuweka hayo katika matendo.

Hata hapa Tanzania kwa namna ya pekee kituo cha Kichungaji cha Bukumbi kilichoanzishwa na Askofu Blomjous, baadaye kikahamishiwa Kipalapala chini ya Baraza la Maaskofu na kuitwa TAPRI kilifanya kazi kubwa sana.  Machimbuko yalingamua kwamba jamii ya Wabantu kimsingi imejengwa juu ya mfumo wa ukoo. Watu wa ukoo wanajiona ukaribu na kama ukoo ulikuwa mkubwa sana uligawanyika lakini ule wa awali ulibaki kama ukoo mama. Kwa njia hii familia kamwe haikuwa na upweke, bali ilikuwa ni sehemu ya ukoo na ukoo uliipa, hifadhi ya jamii ikiwemo uhakika wa maisha ya heshima na kulinda maadili ya jamii. Nje ya ukoo kulikuwa hakuna matendo ya kijamii. Hivyo kanisa iwe kama ukoo.

Kati ya nchi za AMECEA wa  kwanza kuchukua  hatua madhubuti alikuwa Askofu Patrick Kalilombwe, mmisionari ya Afrika (WF) akiwa askofu wa Lilongwe Malawi, yeye alifanya Sinodi ya jimbo (1973 – 75) ambayo ilianzisha mpango wa kichungaji wenye msingi katika JNNK[3]. Hapa Tanzania baadhi ya viongozi wa kanisa walipenda itikadi ya Ujamaa, na maarufu kati yao alikuwa Askofu Christopher Mwoleka[4] wa jimbo Katoliki la Rulenge ambaye siyo tu aliunga mkono ujamaa bali alikwenda kuishi na kushiriki kikamilifu katika kijiji cha ujamaa. Kutokana na uzoefu alioupata huko alikuwa msitari wa mbele katika kuhamsisha na kuunda Jumuiya Ndogo Ndogo.

Mwishowe katika Afrika ilikuwa ni AMECEA ambayo ilikuja na mpango mkakati madhubuti wa kuunda ‘Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo’. Kuanzia Mkutano Mkuu wa AMECEA mwaka 1973 Maaskofu walianza kusisitiza juu ya mpango wa kujikita kwenye JNNK. Mwaka 1976 katika Mkutano Mkuu uliofanyika mjini Nairobi, Kenya maaskofu walitangaza rasmi kwamba "Mfumo wa kuunda Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristu, ndio mkakati rasmi wa uinjilishaji katika kanisa la Afrika ya Mashariki na utapewa kipaumbele katika miaka ijayo” Tangu wakati huo Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo zimekuwa agenda ya kudumu katika mikutano ya AMECEA. Katika azimio la mwaka 1992 kule Zambia walisema “ Jumuiya Ndodo Ndogo sio za hiari katika kanisa, ila ni kitovu cha maisha ya Imani na utume wa uinjilishaji.” Hii ndiyo sababu katika kukaribisha mkutano mkuu wa Amecea Dar es Salaam mwaka 2002 katika kuadhimisha miaka 25 ya Jumuiya Ndogo Ndogo, wajumbe walikaribishwa na mabango yaliyosema "Karibu AMECEA, Mama wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo."[5]

JUMUIYA NDOGO NDOGO KATIKA TANZANIA

Tanzania ilikuwa na bahati, Rais wa kwanza Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitumia mfumo wa jadi katika kuanzisha muundo wa utawala wa Ujamaa. Alianza kutumia shina la nyumba kumi kumi kama msingi wa mfumo wake wa utawala. Kila familia 10 ziliunda shina ambalo lilijitegemea kiutawala na kiuchumi. Hii iliongeza ushiriki wa watu katika utawala na maamuzi. Tangu mwaka 1976 kanisa Tanzania ilichukua kwa umakini mkubwa uamuzi wa maaskofu wa AMECEA kwamba JNNK ni kipaumbele katika uinjilishaji. Mwaka 1977 semina ya taifa aliitwa kujifunza jinsi ya kutekeleza uamuzi huo. Iliamuliwa kuwa kipaumbele cha kanisa Tanzania tangu hapo itakuwa ni kujenga JNNK. “Uundwaji wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu uwe ndio mpango kabambe katika majimbo yote Tanzania Bara na Visiwani. Juhudi zote za kichungaji zilenge kwenye utume huo. Vyombo vya upashanaji habari kwa mfano:- radio, magazeti nk. vitumiwe kwa kuunda na kustawisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu. Mapadre, Watawa na walei watunmie mikutano yao kuwezesha utume huo ufanikiwe. Utume wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu uzungumziwe katika vituo vyote inapofundishwa dini hasa katika nyumba za malezi ya watawa na katika seminari kubwa na ndogo.”[6]

Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu ni kanisa dogo mahalia ya familia zinazopakana na  ambalo kazi yake hasa ni kusali pamoja, kusikiliza na kutafakari pamoja Neno la Mungu na kulieneza. Wanajumuiya wanahamasishana kuishi maisha ya Kikristu na kuwa mashuhuda wa imani yao. JNNK msingi wake ni Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ambavyo huwaimarisha katika Imani, Upendo na Matumaini katika umoja (Koinonia - Umoja), wakishuhudia Kristo aliyefufuka na kumtangaza kama Mungu na Mwokozi ndiyo imani yetu (kerygma - Imani); na kuonyesha imani hiyo kwa huduma wanayotoa miongoni mwao wenyewe na kwa maskini (Diakonia - Utumishi). Mfumo huu uliingizwa katika mikakati yote ya uinjilishaji katika maparokia, majimbo na maelekezo ya kitaifa.[7] Tangu hapo barua za kichungaji hasa barua za Kwaresma zilikumbushia juu ya umuhimu wa JNNK. Halmashauri za Walei nchi nzima zilijikita kwa hilo.

Mwaka 1997 kikao cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, kiliamuru tume ya sheria za kanisa kurekebisha katiba ya Baraza la Walei. Katika katiba mpya waliagiza kwamba viongozi wote wa Halmashauri za Walei kuanzia chini hadi taifani kwanza wawe wamechaguliwa kama viongozi katika JNNK. Hivyo mtu asingeliweza kuwa kiongozi katika ngazi ya kigango, parokia, jimbo au taifa kama hakuwa kiongozi katika Jumuiya Ndogo Ndogo ya Kikristo. Hili lilihamasisha JNNK. Mwaka 2006 Jimbo Kuu la Dar es Salaam lilitangaza mwaka wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na kufatia mafanikio hayo, mwaka 2007 - 2008 ulitangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kama mwaka wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu.[8] Mwaka huo ulizinduliwa majimboni siku ya Pentekoste tarehe 27 Mei 2007 na katika ngazi ya kitaifa ulizinduliwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza tarehe 1 Julai, 2007. Mwaka huo ulitumika kufanya semina katika ngazi mbali mbali kuelimisha na kuhamasisha JNNK. Hivyo si tu katika ngazi ya kitaifa lakini katika ngazi zote, JNNK zimepewa kipaumbele katika mpango wa kichungaji. Hili linathibitishwa na Sinodi mbali mbali za majimbo kama Mwanza, Musoma, Rulenge - Ngara ambazo zilipendekeza kama kipaumbele uimarishaji wa JNNK.

UMUHIMU WA JUMUIYA NDOGO NDOGO: Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni chombo cha ujenzi wa ujirani mwema

JNNK zimeunda ujiani wa watu wanaofahamiana na wanaelewana. Zamani hasa katika miji majirani walikuwa wanapishana bila kufahamiana hasa wale matajiri ambao nyumba zao zimezungushiwa na ugo. Lakini katika JNNK waamini wanakwenda kwa zamu nyumba moja baada ya nyingine. Hivyo hata maskini anaingia katika nyumba ya tajiri bila kuwa na wasi wasi; mama ntilie anaingia nyumba ya waziri na kinyume chake. Pole pole wanakuwa marafiki na kusadiana katika heri na katika majonzi; katika shibe na katika mahitaji.  Katika JNNK wanaunda vikundi vya akina mama, vijana na watoto. Mara nyingine hata vikundi vya wanaume kwa sababu wanaume ingawa huwa wazembe katika mikutano ya kila wiki wanakuwa msitari wa mbele katika matukio muhimu ya JNNK.

Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu kama chombo cha uinjilishaji

Parokia mpya hasa katika miji huanzishwa na Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu. Katika makazi mapya waamini wachache walio imara katika imani yao huanza JNNK wakisali nyumba hadi nyumba. Waamini wakiongezeka JNNK zinagawanyika na mwumini mmoja hutoa sehemu ya ardhi kwa ajili ya matukio ya pamoja. Wakiwa wengi hununua ardhi na kujenga kigango ambacho baadaye huwa parokia. JNNK hujenga mshikamano mkubwa. Msingi wa JNNK ni Neno la Mungu ambalo husomwa kwa pamoja, hutafakari na kumegeana jinsi wanavyoliewa na jinsi linavyogusa maisha yao na maisha ya jumuiya. Wanajumuiya hukutana mara moja kwa wiki. Wanategemezana katika kuelewa na kuishi maisha ya Kikristu.[9] Jumuiya Ndogo Ndogo ya Kikristu ya kweli ni ya kimisionari katika nyanja zake tatu, kwanza ni kuimarishana kudumu katika imani; pili kuwatafuta kondoo waliopotea na kwa sababu mbali mbali ukristo wao umepoa na tatu kuwaendea wale ambao hawamjui Kristu Mungu na Mkombozi. Hii huanza kwa kuwaalika katika sherehe za jumuiya.

Imani bila matendo imekufa. Na sisi ile imani tunayoipata katika neno la Mungu hufuatiwa na matendo. Ili jumuiya iwe hai lazima iwajibike kwa pamoja. Maamuzi yafanywe na wanaoweza, wengi iwezekanavyo wahusishwe katika utekelezaji kila mmoja akiwa amepangiwa kazi. Kama kuna mgonjwa basi wakumtembelea wanapangwa hata kama kuna ulazima wa kumpa usafiri nk. Kama kuna mwanajumuiya hafiki wa kumtafuta anapangwa. Kuna mtafaruku katika familia basi wa kwenda huko anatumwa. Jumuiya zisiwe tu sehemu ya kupanga namna ya kukusanya michango ya kanisa ingawa nalo ni muhimu. Jumuiya pasiwe mahali pa kuhukumu wadhambi bali mahali pa kurudisha waliopotea, sio mahali pa kutoa adhabu na kulipiza kwa wavivu bali mahali pa kufanya kila mmoja apende kwenda kukutana na wenzake.

Jumuiya Ndogo Ndogo na Maisha ya Kikristo

Jumuiya Ndogo ndogo huboresha maisha ya kiroho ya Wakristo. Hasa mjini mtu akiingia katika JNNK hujulikana kwa wengine na huwa na heshima. Mara nyingi mtu ambaye hana heshima ya kutunza hufanya anavyotaka bila kuwa na aibu. Lakini katika JNNK mtu hutaka kulinda heshima yake na heshima ya jumuiya. Anajisikia kwa sababu anakubalika katika nyumba za watu nao wanampa heshima ya kuingia nyumbani kwake hata wale ambao asingetegemea. Katika makazi mapya na mjini JNNK huunganisha watu kutoka katika makabila mbali mbali na aina mbali mbali za maisha. Katika lugha ya kiafrika ni kama amepata ukoo mpya ambako anaweza akapata marafiki na jirani wa kukimbilia akiwa na hitaji la kiroho na kimwili. Wanahimizana na kupeana nguvu katika wema.

Hata matajiri wengi wanakuwa wanaishi katika upweke, kama wana matatizo nyumbani hawana mtu wa kuwatuliza na kuwashauri. Wanaishi maisha ya kuingiza ili waonekane mambo yako sawa. Katika jumuiya wanapata kitulizo.[10] Katika JNNK watoto hufahamiana na bila ubaguzi hucheza pamoja na kujifunza pamoja. Hili hurahishisha malezi kwa sababu wanapata makuzi yanayofanana yenye moyo wa Bwana.  Inakuwa rahisi kwa wazazi kupanga pamoja namna ya kuwafundisha hasa wale wadogo sana. Vijana wanapata fursa ya kupanga pamoja maendeleo yao hasa shughuli za mapumziko na michezo. Wanawake hupanga mambo yao pamoja hasa yale ya malezi na familia.  JNNK inapashwa kuwa familia moja kubwa, familia ya Mungu na kanisa dogo mahalia.

Katika mikutano yetu ya kila wiki tuna sehemu ya kujuliana hali. Tunajuliana hali katika neno la Bwana na siyo tu “habari” ‘Nzuri’ hata kama unaumwa. Hapo tunashirikishana machungu, furaha, mafanikio, mategemeo na shida zetu. Kama mbele yetu kuna tukio maalumu au shida maalum siku hiyo tunaweza kupanga tafakari yetu ya somo kuendana na tukio hilo. Kwa mfano kuna ndoa nasi tunachagua simulizi la harusi ya Kana. Ni kwa sababu hiyo JNNK  inapashwa kuwa ndogo isiyozidi watu familia – Kaya 15 ili wote waweze kufahamiana vizuri kwa majina na uhusiano.

Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na Miundombinu ya Kanisa

Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu zinaimarisha mawasiliano ya kichungaji katika maparokia. Kimsingi shughuli zote za kichungaji huanzia katika JNNK. Huduma za sakramenti huratibishwa na JNNK. Hata na ukusanyaji wa fedha kusaidiwa na JNNK. Kama mambo yanaenda vizuri mawazo hutoka JNNK na kwenda katika ngazi za juu hadi taifani na vile vile huteremka kutoka taifani hadi kwa waamini katika JNNK.[11] Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu huboresha mahusiano na madhehebu na dini nyingine. JNNK hasa kwenye matukio maalum kama siku ya somo wao au tukio lingine muhimu huwaalika waamini wa madhehebu mengine kwenye maadhinisho yao. JNNK zinafanya vizuri hivyo kiasi kwamba siku moja askofu mmoja wa kiluteri aliniomba tumweleze jinsi tunavyoendesha jumuiya ili nao waanze.

Dhamana na wajibu wa Kushirikishana majukumu

Uongozi katika JNNK ni huduma ambayo kila mmoja anapashwa kushiriki. JNNK iweze kufanikiwa majukumu yanapashwa kushirikishwa na kugawanywa ili kila mmoja ajisikie anawajibika katika jumuiya. JNNK isiwe ni ukiritimba wa watu wawili au watatu hata kama wana vipaji na wanajitoa. Ni kweli jumuiya itafanikiwa ikiwa na watu ambao wanajitoa na kuhamasisha wengine lakini siyo kuhodhi utumishi na madaraka. Kila mmoja katika jumuiya apewe jukumu alilo na uwezo nalo na hiyo itamfanya ajisikie yuko hai. Hii ndiyo sababu inasisitizwa kila inapowezekana mkutano wa jumuiya ufanyike nyumba hadi nyumba kama ilivyofanya jumuiya kwanza ya Kikristo. Askofu Mwoleka alikuwa akiimarisha Jumuiya Ndogo Ndogo kwa kuwafanya wajumbe wengi katika jumuiya viongozi na wawajibikaji. Hakutaka kuwa na watazamamaji katika jumuiya. Hivyo waligawana kazi; na mifano ya kazi ndani ya jumuiya ni hizi:

1.     Mwenyekiti na makamu wake ambao ndio waratibu wakuu wa shughuli zote za jumuiya. Vile vile anashikriki kwa karibu kama mlezi wa jumuiya ili jumuiya iwe na maisha ya Kikristo.

2.     Katibu wa Jumuiya pamoja na makamu wake hutunza kumbukumbu za jumuiya na kuratibu matukio mbali mbali

3.     Mtunza hazina husaidia makusanyo ya mfuko wa Jumuiya na vile vile kuratibisha michango ya parokia, jimbo na taifa.

4.     Msalishaji au kiongozi wa ibada na nyimbo huyu akiwa na kikundi chake huongoza ibada, kuchagua wasomaji wa masomo, kufundisha na kuimbisha nyimbo kwa kuwashirikisha wanajumuiya wote

5.     Mnyumba au Mtunza Familia huyu husaidia kufuatilia uchumba ili watayarishwe kwa ajili ya ndoa takatifu, kuhimiza wanaoishi bila ndoa kubarikiwa wafanye hivyo, kuwa na wazee wa kusuluhisha matatizo ya ndoa, kutayarisha mafundisho endelevu ya ndoa na kutembelea familia mbali mbali hasa zenye shida.

6.     Mlezi: huyu na wenzake husaidia ili kila mtoto katika jumuiya abatizwe na kupata sakramenti stahiki. Kusimamia mafundisho msingi ya watoto kama sala. Kuratibu malezi ya kikristu jumuiyani hasa kwa watoto. Kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kusaidiwa kushinda. Vile vile huratibu semina za kiroho za watu wazima na malezi endelevu.

7.     Mhudumu ni wa kuratibu matendo ya huruma kama kuwatembelea wagonjwa na kuhakikisha wanapata huduma za kiroho na kufarijiwa. Hata kushauri wagonjwa wapelekwe hospitali inapohitajika. Vile vile ni mhuishi wa maisha ya sakramenti katika jumuiya. Huratibu hata matendo ya Huruma nje ya jumuiya.

8.     Mchumi huyu kazi yake ni kuratibu hali ya kimwili ya jumuiya. Huyu ni bwana Mipango. Kwa namna ya pekee kutafuta namna ya kuwasaidia vijana kupata ajira. Vile vile kutunisha mfuko wa jumuiya na hata jumuiya kuwekeza. Kusaidia wasiojiweza na hata kuunda VICOBA.

9.     Mlinzi wa haki na amani ni mtu wa mahusiano na watu wa nje akiwajibika kulinda na kutetea haki za wanajumuiya. Husaidia kutazama upepo wa kisiasa, kiuchumi na kudumisha uhusiano mzuri na madhehebu na dini nyingine nk.

10.  Mtamadunishaji: huyu husherekesha katika sikukuu mbali mbali za jumuiya, kupanga michezo, ngoma na kuongoza jumuiya katika furaha. Famila licha ya kusali na kusaidiana katika matatizo inabidi vile vile wafurahi pamoja.

FAIDA ZA JUMUIYA NDOGO NDOGO[12]

 

a)     Zinawaungamisha waamini wenye elimu, itikadi na kipato tofauti.

b)    Zimesaidia na kuboresha uinjilishaji. Taarifa za kikanisa zinafika moja kwa moja na kwa muda mfupi kwa waamini wote.  Wachungaji wanapata mrejesho kwa haraka ya maamuzi na matekelezo mbalimbali. Kwa namna hiyo zimepunguza ombwe kati ya mapadri na waamini

c)     Zinasaidia kutatua matatizo mengi ya kijamii. 

d)    Zimetoa utambulisho kwa wakristo. Wakristo wanakutana siku moja kwa wiki kusali na kusaidana kukabili changamoto za maisha.

e)     Zimewawezesha waamini kuuishi ukristo wao kwa vitendo.  Zimeongeza uwajibikaji wa mkristo mmoja mmoja. Zimerahishisha utambuzi wa karama na vipaji vya waamini.

f)      Zinatoa msaada kwa familia pale zinapopungukiwa hasa kuwafundisha watoto sala na mafundisho mengine ya dini.

g)    Zinaandaa sakramenti, zinawakutanisha vijana wana ndoa watarajiwa na kusaidia kutatua matatizo ya ndoa/familia

h)    Zimerahisisha ukusanyaji wa michango ya waamini.

MAPENDEKEZO JUU YA JNNK: Jumuiya Ndogo Ndogo huundwa na familia kati ya  12 na 15 zinazoishi karibu. Wanajumuiya wanamchagua Kristo kama Bwana na Mungu wao; wanakubali kuongozwa na Roho Mtakatifu wakipendana, wakisali pamoja na kuhudumiana katika mahitaji yao ya kiroho na mwili. Yaani “Wana Moyo Mmoja; Roho Moja na Nia Moja katika Kristu.[13]. Jumuiya yenyewe ichague viongozi wake. Jumuiya ijaribu inavyoweza kumhusisha kila mkristu katika eneo hilo. Isimbakize mtu nje hata yule mwenye matatizo ya kidini. JNNK zisiwe mzigo bali furaha, zisiundwe kwa kuadabisha bali kwa kuhamasisha, mtu asiende kwenye jumuiya ili watoto wake wasiachwe sakramenti au kusudi azikwe kikristu la hasha. Wanajumuiya wajikite kuwa watu wa Kristo. Msingi wa JNNK ni neno la Mungu hivyo kulisoma na kutafakari Neno la Mungu ni muhimu.

Kazi kubwa ni kujengana katika maisha ya Kikristo, kama kuimarisha familia na ndoa za Kikristo. Kuwajenga vijana kiroho na kimwili. Kazi nyingine ya JNNK ni kujengana kiutu, kujuana, kushirikiana na kusaidiana; kujuliana hali na kukuza kazi ya maendeleo. Kuwaendea wakristo waliolegea na kutowaacha peke yao wapotee. Kuonyesha mfano wa upendo kwa majirani wasiokuwa Wakatoliki. Kujenga ujirani mwema pamoja na madhehebu na dini nyingine. Kushirikana nao panapowezekana lakini tukiwa tumeimarika la sivyo tutapotea sisi

JE, TUFANYE NINI KUIMARISHA JUMUIYA NDOGO NDOGO ZA KIKRISTO?

Kuhamasisha mapadre wote waone umuhimu wa JNNK na kuzipa kipaumbele katika uchungaji wao. Wanapashwa kusaidia kuziunda, kuzilea, kuzitembelea, kusali pamoja nao, kuadhimisha sakramenti katika jumuiya. Kama ilivyofanyika mwaka 1998 kuhamasisha juu ya kusoma, kutafakari na kuelezea Neno la Mungu. Hii iambatane na usambazaji wa Maandiko Matakatifu. Kuhamasisha jeshi kubwa la watawa hasa wanawake kujisikia pamoja na JNNK. Kama waamini wengine watoe muda wao baada ya kazi kushiriki na kusaidia JNNK. Baraza la Maaskofu kupitia Idara ya Kichungaji na idara amabatanishi wahuishe mwongozo wa JNNK. Kuonyesha namna ya kuunda, kuongoza, kusali pamoja, kusaidiana na mengine mengi ya jumuiya. Kuwa na semina mbali mbali kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya parokia na vigango juu ya namna ya kuunda, kuendesha na kudumisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo.

HITIMISHO: Mafaniko ya kazi ya uchungaji Tanzania yanategemea ufanisi wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikrstu. Kwa sehemu kubwa ufanisi wa Halmashauri za walei katik ngazi zote umetegemea uimara wa jumuiya Ndodo Ndogo za Kikristu. Waamini wengi nje ya AMECEA n ahata Afrika wanasifu sana mfumo wetu wa JNNK na hata wanajaribu kuiga mara nyingi bila mafanikio kwa mfano India na Ugerumani. Sisi Tanzania ambao tumefanikiwa kuwa na mfumo huu mzuri wa uinjilishaji tujitoe kwa moyo na nguvu zetu zote kuuimarisha.

“Jumuiya Ndogo Ndogo:  Moyo Mmoja na Roho Moja katika Kristo”

[1] Mtaguso II wa vaticani, Dikrii juu ya utume wa walei , no 26.

[2] Comunidas de Base

[3] Jumuiya ndodo Ndogo aliziita ‘Miphakati’

[4] RWECHUNGURA John Joseph, Mjue Askofu Christopher Mwoleka, Bukoba 2012

[5] AMECEA 14th Plenary Assembly, Deeper Evangelization in the New Millennium: A challenge for AMECEA; TEC Dar es Salaam, 2002

[6] Tanzania Episcopal Conference, Plenary meeting minutes 1977.

[7] MRINGI Augustine, Small Christian Communities in Eastern Africa: Canonical Implications with particular reference t Tanzania, Catholic University of America, 1985

[8] ISHENGOMA Rita STH, Small Christian Communities in Tanzania, http://www.smallchristiancommunities.org/africa/tanzania/109--small-christian-communities-sccs-in-tanzania-.html

[9]Post-Synodal Apostolic Exhortation Africae Munus, no. 131.

[10]Post-SynodalApostolic ExhortationEcclesia in Africa. No.43

[11]Post-SynodalApostolic Exhortation “Ecclesia In Africano. 23

[12] Utafiti wa Pd. Stefano Kaombe Jimbo Kuu la Dar es Salaam

[13] JIMBO KUU LA ARUSHA, Mwongozo katika Mkutano wa Sala katika Jumuiya, http://parokiaolosipa.blogspot.com/2015/08/mwongozo-katika-mkutano-wa-sala-kwenye.html

20 June 2019, 13:21