Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu: Ujasiri wa kuthubutu kujikita katika: historia, karama na utume kwa kusoma alama za nyakati! Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu: Ujasiri wa kuthubutu kujikita katika: historia, karama na utume kwa kusoma alama za nyakati! 

Ujasiri wa Masista Wakarmeli wa Mt. Theresia wa Mtoto Yesu!

Baba Mtakatifu Francisko katika siku ya kuombea miito duniani, anawaalika vijana na taifa lote la Mungu kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu. Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, waanzilishi wanatufundisha kuwa na ujasiri wa kuthubutu kwa kujikita katika historia, karama na utume wetu, daima tukijitahidi kusoma alama za nyakati!

Na Sr. Veronica Silvester Buganga, CMTBG - Roma.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2019 anawaalika vijana na taifa lote la Mungu kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu. Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, waanzilishi wanatufundisha kuwa na ujasiri wa kuthubutu kwa kujikita katika historia, karama na utume wetu, daima tukijitahidi kusoma alama za nyakati!

Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu limeanzishwa na Mwenye heri Maria Crocifissa Curcio na Padre Lorenzo Van Den Eerenbeemt. Maria Crocifissa alizaliwa tarehe 30 Januari 1877 huko kwenye Kisiwa cha Ispica, Sicilia nchini Italia. Watawa hawa walikuwa wanasukumwa na hamu ya kushiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu kwa kuwaonjesha watu wa Mataifa upendo na huruma ya Mungu inayookoa. Katika maisha na utume wao wamepitia dhoruba na misusuko mingi.

Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha kwamba, hii ni sehemu ya maisha ya mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Mitume waliokesha usiku kucha lakini, hawakupata kitu!  Bali kwa njia ya nguvu ya upendo na matumaini thabiti, waanzilishi hawa waliendelea kuamini uwezo wa Mungu katika kutimiza mapenzi yake. Hata katika adha wamekuwa na ujasiri wa kuthubutu kuendelea kupambana wakiamini kuwa wao ni mabalozi wa Kristo, “Mbegu ndogo ya haradari” itakayokua mti mkubwa na kuzaa matawi yake na kuyaelekeza sehemu mbali mbali za dunia (Rej. Mt.13: 31).

Baada ya Kashfa ya Msalaba, Mitume wa Yesu walijikatia tamaa, wakasutwa na dhamiri zao na kuanza kurejea tena katika kazi yao ya awali. Wakavua usiku kucha, lakini hawakupata kitu. Yesu alipowatokea na kuwaamuru kutupa jarife lao upande wa kulia, wakatii na hatimaye, wakafanikiwa kupata samaki wengi ajabu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Katika shida na mahangaiko ya maisha, waamini na watawa kwa namna ya pekee kabisa, wanapaswa kuvaa ujasiri wa kuthubutu kupambana na hali yao, ili hatimaye, kuwa na dira na mwongozo kamili wa maisha!

Baba Mtakatifu anakaza kusema kama ilivyo katika historia ya kila wito, kuna “kukutana” na Yesu ambaye alikuwa anatembea, akawaona wavuvi na akawakaribia, ni hivi kwa aliekutana na mwenza katika maisha ya wito wa ndoa hata kwa yule alipata mvuto wa kuishi maisha ya wakfu. Yesu anawaahidia hawa Mitume kuwa hawatakuwa wavuvi wa samaki bali atawafanya kuwa wavuvi wa watu. Hii ndio asili na tabia ya Yesu anapokuita anataka akutoe katika uduni wa maisha na kukuboresha ili aweze kukushirikisha mpango wake mkubwa.

Padre Lorenzo na Maria Crocifissa mipango yao midogo ilianza kupata mwelekeo mpya kunako mwaka 1925. Hii ni siku ambayo Kanisa lilimtangaza Theresia wa mtoto Yesu kuwa Mtakatifu. Ni katika tukio hili “walikutana” kwa mara ya kwanza na kukamilisha maongezi yao yaliyokuwa yakifanyika kwa njia ya barua.  Wakaonekana kunia mamoja yaani kuanzisha Shirika la Kikarmeli la kike kwa ajili ya shughuli za kimissionari ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Huo ukawa ni mwanzo wa Shirika la Wakarmeli Wamissionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu baada ya kupata ruhusa ya mdomo kutoka kwa Kardinali Antonio Vico.

Tarehe 3 Julai 1925 wasichana wa kwanza wakaonesha ujasiri wa kuthubu kutekeleza ahadi za Mungu katika maisha yao. Tarehe 16 Julai, Shirika likatambuliwa rasmi na familia ya Kikarmeli. Ile mbegu ya matumaini ikaanza kuchipua, kukua na hatimaye kueneza matawi yake ndani na nje ya Italia. Watawa hawa wakakita utume wao katika ukarimu wa Kiinjili kwa ajili ya huduma kwa watoto yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wakajenga shule ili kupambana na umaskini pamoja na kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa, wazee na wasiojiweza.

Mnamo tarehe 3 Aprili 1930 Kardinali Tommaso Pio Boggiani, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Porto Santa Lufina kwa kuafikiana na Baba Mtakatifu Pio X1 wakawatambua watawa hawa wapya kwa jina la “Masista Wakarmeli Wamissionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Tarehe 3 Oktoba 1963, Shirika letu likapewa hadhi ya Kipapa na kuendelea kuchanua sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka 1984, wakarmeli wakafungua nyumba ya kwanza Barani Afrika, huko Tanzania, baadaye, tumekwenda nchini Ufilippini, Romania, India na Indonesia.

Kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu tunathubutu kutunza asili yetu ya ubatizo ikikamilishwa na ile tuliyorithi kwa waanzilishi wetu yaani kukuza upendo na muungano wa kina kwa Mungu na kwa jirani. Hii ni changamoto ya kuishi kama mabinti wa Kiekaristi tayari kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Haya ni maisha sala na tafakari ya Neno la Mungu, ambamo tunachota ujasiri wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kuwaita wasichana, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!  

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka huu 2019 anawaalika wanakanisa: kuwasindikiza vijana katika maisha yao, kuwasaidia kufanya mang’amuzi ya miito yao na hatimaye, kufanya maamuzi magumu! Baba Mtakatifu anawaambia “vijana msiwe viziwi kwa wito wa Mungu… msijiruhusu kutawaliwa na woga”.

Miito 2019 Carmeli
18 May 2019, 16:47