Vatican News
Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: ILO izingatia uchumi unaokita mizizi yake katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu! Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC: ILO izingatia uchumi unaokita mizizi yake katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu!  (ANSA)

Mtazamo wa WCC: Miaka 100 ya Shirika la Kazi Duniani, ILO: Utu!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: WCC: Mwaka 2019, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ukuaji hafifu wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na upatikanaji wa kazi zenye staha na zinazoheshimu utu, heshima ya binadamu na haki msingi ni kati ya changamoto endelevu kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Kazi Duniani, ILO lilianzishwa rasmi kunako mwaka 1919 mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kumbe kwa mwaka 2019, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ukuaji hafifu wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na upatikanaji wa kazi zenye staha na zinazoheshimu utu, heshima ya binadamu na haki msingi ni kati ya changamoto endelevu kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, linalounganisha Makanisa 350, yenye waamini zaidi ya milioni 560, hivi karibuni amepata nafasi kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani. Katika hotuba yake, amelipongeza Shirika la Kazi kwa Taarifa Kuhusu Mwelekeo wa Kazi kwa Siku za Usoni Duniani, chini ya uongozi wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika ya Kusini pamoja na Bwana Stefan Lofven, Waziri mkuu wa Sweden. Taarifa hii inaonesha changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa mintarafu fursa za ajira.

Jambo la msingi inalopewa kipaumbele na ILO ni mchakato wa uchumi unaosimikwa katika utu, heshima na mahitaji msingi za binadamu. Huu ni mwelekeo unaopaswa kuzingatiwa na watunga sera, wanasiasa na viongozi wa Serikali katika ujumla wao! Baraza la Makanisa linasema, huu ni mchakato ambao unapaswa kutekelezwa ili kudumisha misingi ya haki na amani duniani; mambo ambayo hayana budi kufumbatwa katika unyenyekevu pamoja na utashi wa kisiasa, ili kuona kwamba, hayo yaliyoamriwa yanatekelezwa kweli kweli! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakaza kusema, utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kamwe mwanadamu asigeuzwe kuwa “kichokoo” katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kuheshimiwa. Nguvu kazi ni kielelezo na ukamilifu wa utu na heshima ya binadamu. Ni katika muktadha huu, wafanyakazi wanaweza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii kwa kuendeleza zawadi ya maisha hapa duniani! Dr. Olav Fykse Tveit anakiri kwamba, ulimwengu wa kidigitali na akili bandia ni mambo ambayo hayamo kwenye Maandiko Matakatifu, lakini hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu; haki, amani, ustawi na maendeleo ya wote pamoja na uwiano sawa katika soko la kimataifa! Katika mkutano huu, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican alikazia kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa kama dira na mwongozo wa tafakari kuhusu nguvu kazi.

Mada hii inakwenda sanjari na nafasi ya familia,  mfumo wa maisha; changamoto ya usawa wa binadamu na pengo kubwa kati ya maskini, yaani “akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi” na matajiri wanaokula na kusaza. Mchango wa nguvu kazi katika mchakato mzima wa ukuaji wa uchumi ni muhimu kuzingatiwa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa mstari wa mbele kukuza na kudumisha majadiliano kati yake na Shirika la Kazi Duniani pamoja na kusaidia harakati za maboresho ya nguvu kazi kwa kuwapatia vijana ujuzi, stadi na maarifa, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Juhudi hizi pia zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

ILO iendelee kuwasaidia wafanyakazi katika kipindi hiki cha mpito kuelekea katika ulimwengu wa kidigitali; kuibu sera na mbinu mkakati wa kupambana na ukosefu wa fursa za ajira kwa muda mrefu zaidi. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na ukuzaji wa haki ya kifedha kati ya kazi na mtaji pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na taratibu za soko la fedha zinazingatiwa na kuheshimiwa na wote! Shirika la Kazi Duniani linapania pamoja na mambo mengine kudumisha haki msingi za binadamu maeneo ya kazi, maboresho ya mazingira ya kazi na vitendea kazi; kuendeleza na kudumisha hifadhi ya jamii sanjari na kukuza majadiliano katika masuala ya kazi!

Utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi na haki jamii inayopatikana kwa njia ya utu na heshima katika mchakato mzima wa kazi ya mwanadamu. Hizi ni tunu msingi ambazo zimekuwa ni mihimili mikuu katika Mapokeo na mafundisho ya dini mbali mbali duniani. Katika kipindi hiki cha kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa na athari zake kuendelea kuonesha makucha yake sehemu mbali mbali za dunia, kuna haja ya kuwa na mwongozo makini kuhusu masuala ya kazi.

Dr. Tveit, ILO
02 May 2019, 15:09