Vatican News
Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, amewataka watanzania kusimama kidete dhidi ya: Ushoga, Utoaji mimba na ukoloni wa kiitikadi! Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, amewataka watanzania kusimama kidete dhidi ya: Ushoga, Utoaji mimba na ukoloni wa kiitikadi!  (Musei Vaticani)

Askofu mkuu Renatus Nkwande: Ushoga, Utoaji mimba & Ukoloni!

Askofu mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza amewataka watanzania kusimama kidete kupinga: Ushoga unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu; kupambana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa katika sera za utaoji mimba pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kupambana na ukoloni wa kiitikadi, ili kulinda: utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 12 Mei 2019, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, Kanisa limeadhimisha ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu”. Katika maadhimisho haya Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania amesimikwa rasmi, kuwa ni Askofu mkuu wa tatu wa Jimbo kuu la Mwanza. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.

Mahubiri yametolewa na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ambaye, hapo awali alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Ibada hii imehudhuriwa na Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania pamoja na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Mwanza. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Viwanja vya Kawekamo, Jimbo kuu la Mwanza.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika salam za pongezi kutoka kwa Maaskofu Katoliki Tanzania, amesema, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bunda. Hii inaonesha kwamba,  ana uwezo na nguvu katika mchakato mzima wa kutekeleza dhamana na majukumu yake kama Askofu.

Askofu mkuu Nyaisonga, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumteuwa na hatimaye, kusimikwa kwa Askofu mkuu Nkwande, kuwa Mchungaji mkuu wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza. Amemwomba ajitahidi kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema. Uongozi ni dhamana nzito inayohitaji fadhila ya: upendo, ukarimu na sadaka ili kuwatangazia watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza, Injili ya matumaini. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza kujikita katika Amri ya Upendo kama dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa. Waamini wapendane kama Kristo Yesu alivyowapenda na upendo huo, uwe ndicho kipimo chao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limechukua nafasi hii kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inazozitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote, kwa kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha umoja, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, amana na utajiri mkubwa kutoka kwa waasisi wa nchi ya Tanzania! Askofu mkuu Nyaisonga amesema, Jimbo kuu la Mwanza lina umaarufu wake katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii ya Tanzania katika ujumla wake. Hapa ni kitovu cha huduma ya afya inayotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) kwa kushirikiana kwa karibu sana na Serikali. Jimbo kuu la Mwanza ni Makao makuu ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Tanzania, SAUT, kilichoanzishwa kunako mwaka 2002, kimepata mafanikio makubwa pamoja na changamoto zake.

Mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika sekta ya elimu na afya ni matunda ya ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kuwahudumia watanzania wote: kiroho na kimwili. Amesema, Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma makini kwa watoto na vijana, ili siku moja waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza! Kanisa linaishukuru Serikali kwa kujenga mazingira bora katika utekelezaji wa huduma hizi na kwamba, bado kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha umoja na mshikamano kati ya Serikali na Kanisa, kwa kuboresha miundo mbinu ya huduma ya afya na elimu kutoka katika ngazi za chini kabisa, ili kupata mafanikio makubwa zaidi.

Daima, macho na fikira za Serikali na Kanisa, ziwe ni kwa ajili ya huduma bora kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga, amehitimisha salam za Maaskofu kwa kumwombea Askofu mkuu Nkwande kuendeleza mema yote yaliyotekelezwa na watangulizi wake na kwamba, ni jukumu la waamini kuhakikisha kwamba, wanampatia ushirikiano na mshikamano, ili aendelee kusoma alama za nyakati na kufanya maboresho makubwa kadiri ya mahitaji ya watu wa Mungu, Jimbo kuu la Mwanza.

Naye Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, katika salam zake kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Mwanza, kwanza kabisa, amemshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, anayemwezesha hata katika udhaifu wake, matendo makuu ya Mungu kuweza kuonekana. Amewashukuru watu wote wa Mungu waliofika kusali pamoja naye na hivyo kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kubariki nia zao njema, ili ziwe ni sababu ya kuwapeleka mbinguni, changamoto kubwa ni kujikita na kuambata mchakato wa utakatifu wa maisha, kwa kukazia Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani; Umoja na mshikamano wa watanzania wote.

Kanisa ni Mama na Mwalimu! Askofu amekabidhiwa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwafundisha wafuasi wake: Heri za Mlimani kama muhtasari wa mafundisho yake makuu na Sala ya Baba Yetu inayowaunganisha wote kuwa ni watoto wa Mwenyezi Mungu licha ya tofauti zao msingi. Yesu kwa ukarimu na upendo wake, amewaachia wafuasi wake, Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho.

Kanisa litaendelea kufundisha: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Sala. Kanisa linapania kuelimisha jamii, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Imani za kishirikina na hofu za pepo wachafu ni “ushamba wa elimu” ni dalili za kukosa imani. Askofu mkuu Nkwande, amelitaka Kanisa kusaidia kuwaokoa watu wanaoelemewa na hofu katika maisha ili kuondokana na imani za kishirikina zinazosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kanisa liwasaidie watu kujikomboa kimwili na kwamba, wokovu wa Mungu unapatikana kwa njia ya Kristo Yesu!

Askofu mkuu Nkwande amesema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa ni tabibu na mganga wa maisha ya kiroho! Aliwaondolea watu magonjwa, akawapatia mahitaji yao msingi pamoja na kuwaondolea dhambi zao, ili kujenga na kudumisha uhusiano mwema kati ya Mungu na mwanadamu. Shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa katika sekta ya elimu na afya zinalenga kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Familia zinapaswa kuwa ni mahali pa kwanza kabisa pa kuwaelimishia watoto tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, watoto wanaiga mila na desturi njema za Kiafrika na kamwe wasiwe ni watu wanaoiga hata mambo yasiyofaa katika jamii!

Askofu mkuu Nkwande kwa uchungu anasema, atasimama kidete kupinga ushoga unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu kadiri mpango wa Mungu. Kanisa litaendelea kupinga utamaduni wa kifo, unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba pamoja na ukoloni wa kiitikadi. Anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo, kwa kumkataa Shetani, Ibilisi na mambo yake yote!

Kwa hakika, watu wakimtumainia na kumkimbilia Mwenyezi Mungu, atawalinda na kuwakirimia kila jema katika maisha. Hii ni hotuba iliyogusa changamoto mamboleo, ambazo wakati mwingine, zinatumiwa na nchi wahisani, kama masharti ya kupatiwa misaada, hali ambayo ni hatari kwa uhuru wa nchi. Umefika wakati kwa watanzania kujikomboa na kuondokana na ukoloni wa kiitikadi! Huu ni uamuzi mzito, lakini ni kwa ajili ya utu, heshima, ustawi na maendeleo ya watanzania katika ujumla wao!

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa katika salam zake, amechangia mifuko 400 ya sementi pamoja na shilingi milioni 2 kusaidia ujenzi wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Paulo II, Kawekamo, Jimbo kuu la Mwanza. Amempongeza Askofu mkuu Nkwande kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika maisha na utume wake, hasa kutokana na moyo wake wa upendo na huduma makini kwa watu wa Mungu. Anamwombea: Imani, hekima na busara; uaminifu na udumifu katika kuwaongoza watu wa Mungu, Jimbo kuu la Mwanza. Anayaweza yote haya katika Yeye anayemtia nguvu na kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana naye kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Waziri mkuu amekazia umuhimu wa ushirikiano na mshikamano kati ya Serikali na Kanisa, ili kuendeleza mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika sekta ya elimu, afya na huduma ya maji na kwamba, Serikali inalitambua Kanisa Katoliki kuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini Tanzania bila kusahau mchango unaotolewa pia na sekta binafsi. Viongozi wa dini wasaidie kuhimiza umuhimu wa kukuza upendo, huruma na msamaha, kwa kuzingatia kanuni ya dhahabu, ili kuponya madonda ya: chuki na uhasama, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii na kisiasa inayopelekea misimamo mikali ya kidini na kiimani, hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Amani ya kweli, utulivu na mshikamano ni kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu. Watanzania waendelee kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa ili kuondokana na umaskini na hatimaye, Tanzania iendelee kuwa ni kisiwa cha amani na kivutio cha watu kutoka nje!  Amani, utulivu, upendo na mshikamano ni nguzo imara na utambulisho wa watanzania!

Askofu Mkuu Nkwande
13 May 2019, 10:55