Vatican News
Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Tanzania, tarehe 30 Mei 2019 limeadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Askofu Alfred Lanctot alipofariki dunia! Huyu ni muasisi wa Jimbo Katoliki Rulenge! Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Tanzania, tarehe 30 Mei 2019 limeadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Askofu Alfred Lanctot alipofariki dunia! Huyu ni muasisi wa Jimbo Katoliki Rulenge!  (AFP or licensors) Historia

Miaka 50 tangu alipofariki dunia Askofu Alfred Lanctot, Rulenge!

Hayati Askofu Alfred Lanctot alizaliwa kunako mwaka 1921 huko Canada. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa daraja ya Upadre kunako mwaka 1936. Papa Pius XI akamteuwa kuwa Askofu tarehe 13 Desemba 1951 na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 6 Machi 1952. Tarehe 30 Mei 1969 akafariki dunia ghafla kutokana na ugonjwa wa shambulio la moyo! Anakumbukwa!

Na Padre Talemwa Gaudence Nkobelerwa –Rulenge-Ngara.

Hayati Askofu Alfred Lanctot alizaliwa huko Canada katika eneo linalojulikana kama Sherbrooke mnamo tarehe 14 mwezi Aprili mwaka 1912.Baada ya masomo yake ya awali alisoma masomo yake ya shule ya upili katika katika Seminari ya mtakatifu Karoli. Mwaka 1932 alijiunga na shirika la white Fathers ( kwa sasa Wamisionari wa Afrika) huko Carthage na kuanza masomo yake ya kitaalimungu tokea mwaka 1933 hadi 1936.Alipewa daraja takatifu la upadre mwaka 1936 akiwa kijana mbichi kabisa wa miaka 24 ya kuzaliwa.Mara tu baada ya upadrisho wake alitumwa kufanya utume katika Afrika ya mashariki, kwenye vikariati ya Bukoba. Akiwa huko Bukoba alisifika sana kwa uwezo wake wakuongea lugha ya kihaya kwa ufasaha,lakini zaidi alisifika kwa kipaji chake cha musiki wa kanisa,na moyo wa usikivu  kwa waamini.

Kutokana na uhitaji wa Kanisa katika kuhudumia watu wake, Padre Lanctot pamoja na padre Daniel walitumwa katika maeneo ya Bushubi kuanzisha misioni ya Rulenge. Katika utume huu padre Lanctot alikuwa ni mweka hazina hivyo alisimamia ujenzi wa Kanisa na vigango vyake. Hii kazi aliifanya kwa ufanisi sana. Alisifika sana kwa kuongea lugha ya Kishubi kwa ufasaha. Akiwa katika utume wake huko Rulenge, mwaka 1942 aliteuliwa kuwa Paroko na mwanzilishi wa Parokia ya Ngote. Kwa sasa Parokia hii ni sehemu ya Jimbo la Bukoba( kwa wakati huu alikuwa ni paroko kijana pekee katika vikarieti nzima).Tunaambiwa kuwa misioni ya Ngote aliijenga kwa msaada mkubwa alioupata kutoka kwa dada yake aliyeitwa Magdalena na ndiyo maana ikapewa jina la Mtakatifu Magdalena kwa heshima yake hadi leo.

Kama kawaida ya umisionari na utume, mnamo mwaka 1946 Padre Lanctot aliamishiwa katika misioni ya Bukoba. Mwaka 1948 Askofu mteule Laurent Tetraut alimteua Padre Lanctot kuambatana naye huko Canada kwa lengo la kuinadi vikarieti ya Bukoba na mahitaji yake (Padre Lanctot alikuwa na “mdomo wa dhahabu”). Akiwa huko Canada, mkuu wa shirika alimteua asaidie kuhamasisha kukusanya fedha kwa ajili ya jumuia.  Kumbe, matarajio ya kurudi Bukoba kwa haraka yakashindika, badala yake akateuliwa kuwa kiongozi wa Jumuiya ya Mtakatifu Bonifasi huko Manitoba. Kwa kutambulika kwake huko Canada na katika Shirika lake Vikarieti ya Bukoba ilipata kutambulika pia na kuheshimiwa. Pamoja na kwamba, alitamani kufanya utume tena Barani Afrika, wajibu huu aliokuwa nao huko Canada haukumfanya afikiri kama angeweza kurudi tena katika Bara hilo alilolipenda.

Mipango ya Mungu haichunguliziki! Baada ya ya kifo cha ghafla cha Askofu Tetraut, Baba mtakatifu Pius XI, alimteua mheshimiwa Padre Lanctot kuwa mrithi, tarehe 13, Desemba, 1951. Katika uteuzi huo Vikarieti ya Bukoba waliigawa katika sehemu mbili. Sehemu ya Kaskazini iliwekwa chini ya uongozi wa Askofu Laurian Rugambwa, na sehemu ya Kusini, yaani Bukoba ikawa chini ya askofu Lanctot. Katika kuonesha upendo wake kwa Mama Bikira Maria, Shirika la Wamisionari wa Afrika  White Fathers na Afrika, Askofu Lanctot, aliipamba nembo yake ya kiasikofu, kwa alama ya Mama Bikira Maria , pelikani na tawi la mtende. Tarehe 6 Machi, 1952 aliwekwa wakfu kuwa Askofu huko Canada. Na baadaye mwezi Juni, 1952 kwa shangwe kubwa alipokelewa Bukoba. Aliunganisha Canada na Bukoba hivi kwamba ndugu wa Canada walisaidia sana maendeleo ya shughuli za kichungaji kwa ufanisi mkubwa katika vikarieti ya Bukoba.

Kutoka na mpango mkakati wa kuimarisha na kulitegemeza Kanisa. Mwaka 1960 ,Askofu Lanctot alitangazwa kuwa askofu wa jimbo jipya la Rulenge. Hii ilikuwa habari njema kwa misioni ya Rulenge aliyokuwa ameianzisha mwaka 1940. Alifanya utume wake kwa moyo wote na roho yake yote na kwa upendo wa dhati. Kutokana na uchovu wa kiafya uliotokana kujitoa kwake katika utumishi, aliomba apatiwe msaada wa askofu msaidizi.  Ndiposa, tarehe 6 Machi 1969, Mtakatifu Yohane XXIII akamteua Padre Christopher Mwoleka (sasa marehemu) kuwa askofu msaidizi wa jimbo la Rulenge. Katika maandalizi ya daraja ya uaskofu wa askofu msaidizi mteule, Mwoleka (tunaambiwa aliandika barua 480 kwa mkono wake kwa wafadhili ilikumtambulisha askofu mteule. Pia aliandika kadi za mialiko 190 kwa mkono wake). Katika hali isiyokuwa ya kawaida mpendwa Askofu Alfred Lanctot, kipenzi cha wana Rulenge aliaga dunia ghafla kwa ugonjwa wa shambulio la moyo (heart attack), mnamo tarehe 30 Mei, 1969. Na kaburi lake lipo hapa kwetu Kanisani Rulenge hadi leo.

Baba askofu Lanctot atakumbukwa sana kwa moyo wake wa upendo katika utume wake kwa Bukoba, na zaidi kwa wana Rulenge. Alijenga makao makuu ya kwanza ya Jimbo la Rulenge, aliimarisha imani katika Parokia za jimbo lake, alianzisha vituo vya elimu, Seminari ya Katoke, vituo vya afya, huko: Rulenge, Buhororo na Biharamulo.  Kwa msaada wa Shirika la Masista wa Malkia wa Malaika kutoka Canada alianzisha Shirika la Wabernadeta wa Mtakatifu Francisko wa Assisi (FSSB). Alisistizia zaidi juu ya Sala ya Rosari katika familia na uanzishwaji wa Legio Mariae hata SACCOs kwa lengo la kuwawezasha waamini kujitegemea kiuchumi pia. Uongozi wake wa moyo wa ubaba umeonekana wazi katika jitihada za Maaskofu ambao wamefuata nyanyo zake ndani ya Jimbo letu hadi sasa.

Tunapoadhimisha miaka 50 ya kifo cha Baba Lanctot, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai aliomjalia alipokuwa hapa duniani, tunashukuru pia kwa moyo wa umisionari katika Afrika na jimbo la Rulenge (sasa Rulenge-Ngara). Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujalie kutimiza ndoto za Hayati Askofu Lanctot za kuelendelea kusimika mizizi ya Kanisa linalo amini na kuwajibika. Mwenyezi Mungu atujalie pia moyo wa umisionari katika maisha ya ukristo wetu. Shukrani pia kwa Shirika la Wamisionari wa Afrika la White Fathers kwa utumishi uliotukuka wa Baba Lanctot. Raha ya Milele Umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie. ASTAREHE KWA AMANI.

31 May 2019, 08:54