Vatican News
Viongozi wa kidini wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na mardhiano kati ya watu! Viongozi wa kidini wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na mardhiano kati ya watu!  (Vatican Media)

Mkutano wa Majadiliano ya Kidini Kimataifa, Abu Dhabi, 2019

Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa na sauti moja dhidi ya misimamo mikali ya kidini inayohatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano, kiasi cha kuwatumbukiza watu katika majanga na maafa makubwa: kiroho na kimwili. Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini huko Abu Dhambi, Umoja wa Falme za Kiarabu umeongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu"

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni nguzo ya majadiliano ya kidini, ili kudumisha amani duniani na kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hii ni hati ambayo imeandaliwa kwa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kudhibiti: vita, uharibifu unaosababishwa na vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama kati ya watu! Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana ya ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani duniani.

Hii ni hati inayopata chimbuko katika misingi ya imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Imefanyiwa kazi kwa muda wa mwaka mzima na baada ya sala na tafakari ya kina, viongozi wakuu wameridhia na sasa ni dira na mwongozo wa majadiliano ya kidini. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake Jumatano, tarehe 6 Februari 2019 amesema, wakati wote wa hija yake huko Umoja wa Falme za Kiarabu amemfikiria sana Mtakatifu Francisko wa Assisi; moyoni mwake uliwaka moto wa Injili na Upendo kwa Kristo Yesu! Katika matukio mbali mbali, Sala ya Baba Yetu kwa ajili ya watoto wake wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii iliendelea kusikika moyoni mwake.

Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa na sauti moja dhidi ya misimamo mikali ya kidini inayohatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano, kiasi cha kuwatumbukiza watu katika majanga na maafa makubwa: kiroho na kimwili. Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini huko Abu Dhambi, Umoja wa Falme za Kiarabu umeongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima katika ujumbe wake kwenye mkutano huu, amekazia umuhimu wa waamini kujenga na kudumisha dhamiri nyofu na kamwe wasikubali dini kutumika kama chanzo cha vita, kinzani na migogoro ndani ya jamii.

Patriaki Cyril, amewaomba viongozi wa dini kimataifa kushikamana kwa dhati ili kuwasaidia wananchi wanaoteseka kwa vita sehemu mbali mbali za dunia, lakini hasa zaidi huko Mashariki ya Kati: Siria, Iraq bila kuisahau Libia. Viongozi wa dini wawe ni mashuhuda na vyombo vya kanuni maadili na utu wema, unaosimikwa katika: umoja, upendo, huruma na mshikamano wa dhati. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa na hata wakati mwingine viongozi wa kidini wakitumia dini kusababisha vita, ghasia na mauaji yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vitendo vya kigaidi.

Vita, nyanyaso na madhulumu huko Mashariki ya Kati ni matokeo ya misimamo mikali ya kidini na kiimani, kiasi cha watu kushindwa kudumisha haki, amani na maridhiano. Makanisa mengi huko Mashariki ya Kati yamebomolewa kiasi kwamba, idadi ya Wakristo inaendelea kupungua kila mwaka. Kuna watu wanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao na matokeo yake ni kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora ughaibuni! Lakini hata huko mambo si shwari sana kwani wanaendelea kupambana na hali ngumu ya maisha! Kumbe, majadiliano ya kidini, amani na maridhiano ni nyenzo msingi katika kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu!

Kwa upande wake, Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema udugu wa kibinadamu ni wito maalum kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hiki ni kiini cha imani ya Kikristo, changamoto na mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali kufanya hija katika haki na amani, ili kubomoa kuta za utengano na ubaguzi wa aina mbali mbali katika mwanga wa udugu wa kibinadamu! Ubaguzi wa rangi ni tishio kwa umoja na mafungamano ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wanaotaka haki na amani katika maisha yao, wanapaswa hata wao kuwatendea jirani zao kadiri ya kanuni ya dhahabu.

Ubaguzi wa rangi ni sumu kali inayotishia ustawi na maendeleo ya watu. Changamoto kwa wakati huu ni kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Dr. Olav Fykse Tveit anasema, Karne ya XX itakumbukwa kwa kuwa na kurasa chafu za mauaji ya kimbari yaliyopelekea Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kumbe, udugu wa kibinadamu ni wito na dhamana kutoka mwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutekelezwa na waamini wa dini mbali mbali kama chachu ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Tofauti msingi kati ya watu wa Mataifa ni utajiri na amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Tofauti za: imani, dini, taalimungu na kisiasa, kuna wakati zimetumiwa kwa malengo binafsi na hivyo kuwa ni chanzo cha vita, kinzani na misigano mbali mbali, hali inayoweza hata kwa siku za mbeleni kuhatarisha udugu wa kibinadamu. Viongozi wa dini wajitahidi kuwekeza katika elimu makini na fungamani, ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kutafuta na kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kuendelea kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Tofauti msingi za kidini na kiimani; kitamaduni na mahali anapotoka mtu, iwe ni chachu ya ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano; kwa kuthamini utu, heshima na haki msingi za  binadamu. Iwe ni fursa ya kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini, mambo msingi katika umoja na mafungamano ya kijamii!

Majadiliano ya kidini: Viongozi
07 February 2019, 15:50