Vatican News
Askofu mkuu Philip Arnold Subira wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya wakati akisimikwa rasmi. Askofu mkuu Philip Arnold Subira wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya wakati akisimikwa rasmi. 

Askofu mkuu Philip Anyolo, Jimbo kuu la Kisumu! Yaliyojiri!

Askofu mkuu Anyolo nasema, yuko kati yao kama mtoto wa Mungu na katika Kristo Yesu wanatimilika katika yote; kwa kujengwa katika yeye, ili waweze kuimarishwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake kama kielelezo cha shukrani! Changamoto kubwa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu ni kuhakikisha kwamba, inajenga familia inayokita mizizi yake kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya, Jumamosi, tarehe 12 Januari 2019 alisimikwa rasmi kuwa Askofu mpya wa Jimbo kuu la Kisumu baada ya Askofu mkuu Zacchaeus Okoth kung’atuka kutoka madarakani, baada ya kuliongoza Jimbo hilo kwa muda wa miaka 40. Katika kipindi chote hiki, kipaumbele chake cha kwanza anasema, Askofu mkuu Mstaafu Okoth: shughuli za kichungaji na uinjilishaji wa kina uliogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Alipenda kujikita zaidi katika suala zima la elimu, ili kuwajengea wananchi wa Kenya: stadi, ujuzi na maarifa ya kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili Kenya iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi na mahubiri kutolewa na Askofu John Oballa Owaa wa Jimbo Katoliki la Ngong. Katika wosia wake kwa Askofu mkuu Philip Anyolo, amemtaka kusimama kidete kupambana na changamoto pamoja na matatizo mbali mbali yanayowaathiri watu wa Mungu, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Awe ni dira na mwanga katika kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Askofu mkuu Anyolo awe ni kiongozi anayetumia zaidi hekima, busara na upendo wa kichungaji, daima akijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kupambana na umaskini wa hali na kipato. Kanisa liendelee kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kuragibisha haki jamii, kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Ikumbukwe kwamba, Askofu ni kiongozi na mchungaji wa Kanisa, anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, ili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake barabara! Familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu imempata mchungaji: mnyenyekevu, mvumilivu, mchapa kazi na kwamba, kwa hakika ni mtu wa sala anayetegemea pia mchango kutoka kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu!

Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo kwa upande wake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Kisumu pamoja na kuwashukuru Maaskofu wenzake, kwa umoja, upendo na mshikamano katika kuwahudumia watu wa Mungu nchini Kenya. Anasema, yuko kati yao kama mtoto wa Mungu na katika Kristo Yesu wanatimilika katika yote; kwa kujengwa katika yeye, ili waweze kuimarishwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake kama kielelezo cha shukrani! Changamoto kubwa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu ni kuhakikisha kwamba, inajenga familia inayokita mizizi yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Askofu mkuu Anyolo anawataka watawa na wakleri kuhakikisha kwamba maisha, wito na utume wao unapata asili na hitimisho lake kwa kumwambata Kristo Yesu, hasa zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Kisumu. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, daima Kristo Yesu, awe ni mwambata wa hija ya maisha yao hapa duniani na kamwe wasimwekee kizingiti. Waamini wakumbuke kwamba, ulimwengu mamboleo unataka kumezwa na mmong’onyoko wa maadili na utu wema; watu wanataka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha yao; watu wanataka kugeuza maisha kuwa kama bidhaa inayoweza kununuliwa dukani.

Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Tofauti kubwa zitaendelea kujitokeza kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, kwa sababu ya rushwa, ufisadi, uchoyo na ubinafsi. Yote haya ni mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani, tayari kuchuchumilia neema ya utakaso, ili kuambata utakatifu wa maisha. Ikiwa kama familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu, itakuwa imeungana na kushibana na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake; watu wote wataweza kuonja neema ya wokovu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watu wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau; kwa kukuza na kudumisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Wawe na ari na moyo mkuu wa kuweza kupambana na dhambi, udhaifu na mapungufu yao kama binadamu; sanjari na kuendelea kuchukuliana kama ndugu.

Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo anakaza kusema, kwa hakika anataka kuwatumikia watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Kisumu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu; daima akijiweka katika ulinzi, tunza na maongozi ya Mwenyezi Mungu. Anasema, yuko kati yao kama Mchungaji ambaye yuko tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ataendelea kuchota utajiri wa Neno la Mungu katika kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Kisumu. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Kisumu ijielekeze kwa Kristo Yesu na wala si kwa Askofu mkuu, ili waweze kukaa na kudumu pamoja naye!

Sherehe ya kumsimika Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo wa Jimbo kuu la Kisumu zimehudhuriwa pia na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Serikalini na vyama vya upinzani nchini Kenya, bila kusahau umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema, uliofika kushuhudia tukio hili la aina yake! Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Philip Arnold Subira Anyolo alizaliwa tarehe 18 Mei 1956 huko Tongareni. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, hapo tarehe 15 Oktoba 1983 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 6 Desemba 1995 akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kericho na kuwekwa wakfu tarehe 3 Februari 1996. Papa Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Machi 2003 akamteuwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Homa Bay na kusimikwa rasmi tarehe 23 Mei 2003. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Novemba 2018 akamteuwa kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Katoliki la Kisumu, Kenya.

Jimbo kuu la Kisumu
17 January 2019, 14:58