Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu ni jibu makini ya kilio cha damu! Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu ni jibu makini ya kilio cha damu!  

Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo ni kiini cha mshikamano na jibu la kilio cha damu!

Fadhila kuu tatu zitokanazo na tafakari ya mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote: Huruma, upendo usiobagua na mshikamano wa upendo kama njia muafaka wa kujibu kilio cha damu! Tunu hizi ni muhimu kwa Mkristo anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu kama njia ya kumuiga Kristo na kufanana naye.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu msikilizaji napenda kukaribisha katika tafakari ya tasaufi ya Damu Takatifu. Tuko katika mwezi wa saba, mwezi ambao Mama Kanisa ameutenga maalumu kwa ajili ya kutafakari na kuitukuza kwa namna ya pekee Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Damu ya ukombozi na upatanisho.Katika tafakari iliyopita tulisema kuwa tasaufi ni ujumla wa mambo yanayohuisha na kuongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu; ni mambo yahusuyo imani, mitazamo na matendo maalumu. Katika mazingira ya Kikristu tunaweza kusema kwamba tasaufi ni mtindo wa maisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Katika Kanisa kuna tasaufi mbalimbali ambazo ni zawadi zitokazo kwa Roho Mtakatifu. Ikumbukwe daima kuwa kiini cha tasaufi yeyote ya Kikristo ni Yesu mwenyewe: yaani mafundisho na mfano halisi wa maisha yake. Kila tasaufi hujaribu kuyaishi mafundisho ya Yesu katika matendo na maisha ya kila siku. Tasaufi huongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu katika mahusiano na Mungu, mahusiano na watu wengine, na ulimwengu kwa jumla. Tasaufi yeyote haiwezi kuwa tasaufi ya kweli kama haina uhusiano na maisha halisi.

Ikijengwa katika misingi ya Neno la Mungu, Mapokeo ya Kanisa, Mang’amuzi na mafundisho ya watakatifu mbalimbali katika historia ya Kanisa, Liturjia na hasa Ekaristi Takatifu, tasaufi ya Damu Takatifu inatusaidia kuishi katika imani thabiti ya Kikristu na inatujenga katika mitazamo sahihi ya Kikristu kadiri ya mafundisho ya Yesu mwenyewe. Leo hii tutaongelea tunu au fadhila tatu zitokanazo na tafakari ya mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote: Huruma, upendo usiobagua na mshikamano wa upendo kama njia muafaka wa kujibu kilio cha damu! Tunu hizi ni muhimu kwa Mkristo anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu kama njia ya kumuiga Kristu na kufanana naye

Mshikamano na wale wenye taabu na shida mbalimbali: Hii ni tumu muhimu sana katika tasaufi ya Damu Takatifu. Tasaufi ya Damu Takatifu ni tasaufi ya mshikamano ambayo chimbuko lake ni Mungu mwenyewe aliyekubali kuingia katika mshikamano nasi kupitia Mwanae wa pekee. Ili kuukamilisha mpango wa Mungu wa ukombozi Yesu ambaye kwa asili ni Mungu, alikubali kuacha yote, akajishusha, akachukua damu yetu ya kibinadamu, akawa mwanadamu. Hilo ndilo fumbo la umwilisho kama jinsi Mtume Yohana anatuthibitishia katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote Sura ya nne, aya ya pili hadi ya tatu. Nao Waraka kwa Waebrania unatudhihirishia kwamba kwa fumbo la umwilisho Yesu aliishi kama sisi isipokuwa hakuwa na dhambi. Alikubali kuwa ndugu yetu na hakuona aibu kutuita sisi “ndugu zake”. (Rejea Ebr 2:11). Alionja shida na mahangaiko yetu tena alikubali kujitwisha mzigo wa dhambi zetu mabegani mwake. (Rejea 1 Pet 2:24).

Mtakatifu Gaspari, mwanzilishi wa shirika la wamisionari wa Damu Takatifu, aliwaasa daima wamisionari wake kuwa na moyo wa kutoka na kwenda kujifunza mahangaiko ya watu na kuingia katika mshikamano nao. Anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu ni mtu wa mshikamano, ni mtu ambaye haogopi kwenda kuonja shida na mahangaiko ya watu hasa wanyonge na wale walioko pembezoni mwa jamii. Wale wote wanaoongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu hawachoki kuchukuliana mizigo na hawaogopi kuingia katika mshikamano na masikini na wanyonge. Ndiyo maana Mtakatifu Yohane II alipokutana na wamisionari wa Damu Takatifu mwaka 2001 aliwakumbusha wamisionari juu ya tunu hii, kuwa tayari kwenda kule ambako wengine hawapendi, yaani kwa masikini na wenye shida.

Basi ninakualika ndugu yangu tuchukue nafasi ili kuitafiti mioyo yetu na kuona kama kweli tasaufi hii ya Damu Takatifu inaongoza maisha yetu, mahusiano yetu, mitazamo yetu na katika mambo tunayoyachagua. Tasaufi ya Damu Takatifu ni tasaufi inayopaswa kuongoza maisha ya kila Mkristo, awe mtawa, padre, au mlei maana tasaufi hii imejengwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuishi fadhila zitokanazo na tasaufi hii ili iwe njia kwetu ya kushuhudia imani yetu kwa maneno na matendo.

 

 

 

26 July 2018, 09:45