Tafuta

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.   (AFP or licensors)

Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani: Mtakatifu Yosefu Waombee Wafanyakazi Wote

Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa vile Sikukuu hii iligubikwa sana na kilio cha wafanyakazi, machafuko, kinzani na misigano, hasa kwenye Karne ya XIX, Mama Kanisa akataka Mtakatifu Yosefu kuwa ni kielelezo makini cha mapambano ya kudai haki msingi za wafanyakazi, utu na heshima yao pamoja na kutoa hadhi kwa kazi kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kazi ya uumbaji na ukombozi ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliishiriki kiasi hata cha watu kumsema: “Huyu si yule seremala…” Mk. 6:3. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; kwa kutambua na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Kazi, Ushiriki na Demokrasia
Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Kazi, Ushiriki na Demokrasia

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Mei Mosi, 2024 amewakumbusha waamini na mahujaji waliohudhuria Katekesi yake kwamba, Mei Mosi, Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi na mwanzo wa mwezi Mei, uliotengwa kwa ajili ya heshima na ibada kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano bora wa Familia Takatifu ya Nazareti ya Mtoto Yesu, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, ili familia zao, Kanisa dogo la nyumbani, liweze kuwa ni Jumuiya ya maisha, kazi na upendo. Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika usiku na mchana kutafuta fursa za kazi! Kanisa ni Mama na Mwalimu, daima anapenda kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu hazina budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu, ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu, anathamini sana kazi ya uumbaji aliyoitekeleza kwa muda wa siku sita na siku ya saba akapumzika. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa wafanyakazi, aendelee kuwakumbuka na kuwaombea watu wote, ili asiyewepo kijana, familia au mtu awaye yote asiyekuwa na fursa ya ajira. Hii iwe ni dhamana inayowawajibisha watu wote. Mei Mosi ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na kuwaua wafanyakazi wanne.

Kazi kwa ajili ya ushiriki na demokrasia
Kazi kwa ajili ya ushiriki na demokrasia

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, 2024 Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika ujumbe wake linasema, ni lazima kuziba mapengo ya kiuchumi kati ya vizazi na jinsia, bila kusahau masuala mazito ya ajira hatarishi na unyonyaji wa wafanyakazi wahamiaji. Hadi haki za wafanyakazi wote zitakapotambuliwa, wananchi wa Italia hawezi kamwe kuzungumzia demokrasia kamili nchini Italia. Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu: “Kazi kwa ajili ya ushiriki na demokrasia.” Mwenyeheri Professa Giuseppe Toniolo, Baba wa Familia, Jaalimu wa siasa za kiuchumi toka Chuo kikuu cha Pisa, mwamini makini aliyeacha harufu ya utakatifu katika maisha ya kijamii nchini Italia ndiye Muasisi wa Maadhimisho ya Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii, ambalo kwa Mwaka 2024 linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yatafanyikia mjini Trieste kuanzia tarehe 3 – 7 Julai 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Katika moyo wa demokrasia. Kushiriki kati ya historia na siku zijazo." Hii ni haki inayopaswa kutekelezwa na kila mtu ili demokrasia ya kweli iweze kutimia. Maaskofu wanakazia zaidi kazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kushiriki katika kufanya kazi ni kitendo cha upendo katika siasa sanjari na ukuzaji wa demokrasia.

Mtakatifu Yosefu
02 May 2024, 11:54