Tafuta

Mfuko wa Blanquerna wa Chuo Kikuu cha Ramon Llull cha Barcellona nchini Hispania, kilichoanzishwa kunako mwaka 1948 ili kutoa mafunzo makini kwa walimu Mfuko wa Blanquerna wa Chuo Kikuu cha Ramon Llull cha Barcellona nchini Hispania, kilichoanzishwa kunako mwaka 1948 ili kutoa mafunzo makini kwa walimu  (Vatican Media)

Wito wa Familia Katika Malezi na Makuzi ya Watoto Wao

Mwenyeheri Raymond Lull “Daktari wa Mwanga” alijibidiisha kuhakikisha kwamba, anarejesha wito wa familia katika malezi na makuzi ya watoto wao, kwa kuwapatia vijana wa kizazi kipya miongozo mbalimbali ya maisha, ili kukabiliana na changamoto kwa kuwafunda vijana ili siku moja waweze kuwa ni mashuhuda, na raia wema mambo msingi katika malezi na majiundo ya elimu makini, ili baada ya kumaliza safari ya maisha wakutane na Kristo Yesu huko mbinguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubora na umakini wa elimu, maadili mema na tafiti za kisayansi ni kati ya mambo msingi yanayozitambulisha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Lengo ni kumwandaa mwanafunzi kiutu na kimaadili, ili aweze kuwa: mwaminifu, mwadilifu na mzalendo kwa nchi yake na balozi mwema kwa Kanisa. Wasomi wanaohitimu kutoka katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa wanapaswa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Kanisa Katoliki linapenda kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika mwono chanya na utambulisho wake katika sekta ya elimu, kwa kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaojikita katika elimu makini inayopania kumpatia mwanadamu ukombozi kamili: kiroho na kimwili. Kanisa linataka kuondokana na mwelekeo wa kujitafuta na kujilinda, ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Wito wa familia katika malezi na makuzi ya watoto wao
Wito wa familia katika malezi na makuzi ya watoto wao

Mchakato wa elimu makini pamoja na mambo mengine unakazia umuhimu wa: majiundo awali na endelevu; imani, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ushuhuda kutoka katika maeneo ambayo hayana uhuru kamili kuhusiana na masuala ya uhuru wa kidini; wajibu wa kuzungumza ukweli katika uwazi pasi na woga; umuhimu wa elimu katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ili elimu iweze kuwapatia ukombozi wa kweli. Kanisa linatambua kwamba elimu kimsingi, ni ufunguo wa maisha na ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu inayotekelezwa katika upendo kwa Mungu na jirani. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kikamilifu ili hatimaye, waweze kujikita katika elimu inayowajengea utamaduni wa watu kukutana na kushirikiana kwa dhati katika mchakato wa maendeleo fungamani. Kanisa linataka kukuza majadiliano ya kina na wadau mbalimbali katika sekta ya elimu pasi na kupoteza utambulisho wake na badala yake kuwa kweli ni kielelezo cha ushuhuda wa huduma ya upendo inayovunjilia mbali kuta zinazowatenganisha watu kwa sababu mbalimbali. Mfuko wa Blanquerna wa Chuo Kikuu cha Ramon Llull cha Barcellona nchini Hispania, kilichoanzishwa kunako mwaka 1948 ili kutoa mafunzo makini kwa walimu, kwa kukazia: Ubora wa elimu na ubunifu ili kuweza kuunga mkono mabadiliko ya kijamii. Blanquerna-URL inaendelea kujikita katika nyanja za elimu, michezo, afya, mawasiliano na mahusiano ya kimataifa. Hii ni Jumuiya ya Chuo Kikuu kinachoendeshwa kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; mafundisho jamii ya Kanisa, ili kusaidia kuleta mabadiliko ndani ya jamii kwa kukazia maarifa katika huduma ya haki na utu wema.

Malezi makini ya watoto na vijana katika malezi na makuzi ya watoto
Malezi makini ya watoto na vijana katika malezi na makuzi ya watoto

Hiki ni Chuo Kikuu kinachotambulikana Kitaifa na Kimataifa kwa mtindo wake wa ubunifu wa elimu, kwa ubora katika mafunzo ya wataalamu wenye kiwango cha juu cha kuajiriwa na kujitolea kwa kijamii, na pia kwa athari za utafiti wake kwa jamii. Ni katika muktadha huu wajumbe wa Mfuko wa Blanquerna wa Chuo Kikuu cha Ramon Llull cha Barcellona nchini Hispania wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican tarehe 3 Mei 2024 Mwenyeheri Raymond Lull, 'Doctor Illuminatus' maarufu kama “Daktari wa Mwanga” alikuwa ni mwanafalsafa na taalimungu mahiri, ambae ameacha mfano bora wa kuigwa katika kumfuasa Kristo Yesu, popote pale mtu anapoitwa. Alikuwa anatumia lugha iliyoeleweka na wengi, katika mchakato wa kumfuasa Kristo Yesu ili kupata furaha ya kweli changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujibidiisha kugundua mpango wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa familia kujikita katika mchakato wa elimu, umuhimu wa malezi na majiundo kwa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, wajitahidi kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anafahamika na kupendwa.

Ubora na umakini wa elimu, maadili na utu wema utambulisho wa vyuo vya Kanisa
Ubora na umakini wa elimu, maadili na utu wema utambulisho wa vyuo vya Kanisa

Mwenyeheri Raymond Lull 'Doctor Illuminatus” yaani “Daktari wa Mwanga” katika maisha na utume wake, alijibidiisha kuhakikisha kwamba, anarejesha wito wa familia katika malezi na makuzi ya watoto wao, kwa kuwapatia vijana wa kizazi kipya miongozo mbalimbali ya maisha, ili kukabiliana na changamoto za maisha, kwa kuwafunda vijana ili siku moja waweze kuwa ni mashuhuda wa imani; raia wema na wawajibikaji, mambo msingi katika malezi na majiundo ya elimu makini, ili baada ya kumaliza safari ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi waweze kukutana na Kristo Yesu.Ni katika muktadha huu wa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu anawahimiza wadau wa elimu kutoa malezi makini yatakayowezesha vijana kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao, kwa kutambua kwamba, huko duniani, bondeni kwenye machozi, ni wapita njia na wala hawana makazi ya kudumu, kumbe, jitihada zote ziwawezeshe kukutana na Kristo Yesu, ili kuonja upendo wake wa daima, upendo ambao ameumimina katika nyoyo zao; huu ndio upendo unaowapatia nguvu ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Wasimame kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wajitahidi kuboresha maisha ya wanafunzi wao kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu, tayari kuondoa giza linalowaandama waja wake na hivyo kuwaweka mbali na uwepo wake angavu!

Barcellona elimu
03 May 2024, 14:44