Tafuta

2023.08.05 Viaggio Apostolico in Portogallo in occasione della XXXVII Giornata Mondiale della Gioventu' - Preghiera del Santo Rosario con i giovani ammalati presso la Cappellina delle Apparizioni

Mfungulieni Bikira Maria Malango ya Maisha Yenu Apate Kuingia

Hii ni fursa kwa Bikira Maria kuingia ndani ya Jimbo, Parokia na kwenye familia zao, huku akibisha hodi katika nyoyo zao, dhamiri zao nyofu na katika nyumba zao, katika hali na mazingira haya, jambo la msingi kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, na kumkaribisha, tayari kumshirikisha furaha, majonzi na changamoto za maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na ujasiri wa kuweza kumkaribisha B. Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano Mei, Mosi 2024 amesema, Mama Kanisa anauanza Mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada kwa Bikira Maria na Ibada ya huruma ya Mungu ni nyenzo muhimu sana katika hija ya kuutafuta na kuukumbatia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kuwa wafuasi aminifu wa Kristo sanjari na mashuhuda wa huruma ya Mungu hapa duniani. Anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutambua na kuthamini dhamana na nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika ufuasi wao. Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu, Mtumishi mwaminifu na mwalimu mkuu katika shule ya huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni nyota angavu inayowasindikiza waamini katika hija ya kumwendea Baba wa milele!

Mwezi Mei ni kwa ajili ya Ibada na Heshima kwa Bikira Maria
Mwezi Mei ni kwa ajili ya Ibada na Heshima kwa Bikira Maria

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Termoli nchini Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima, sanjari na kutembeza Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima, anawaalika watu wa Mungu Jimboni humo kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao. Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima, imeanza kutembezwa Jimboni humo kuanzia tarehe 27 Aprili 2024 hadi Dominika tarehe 5 Mei 2024. Hii ni fursa kwa Bikira Maria kuingia ndani ya Jimbo, Parokia na kwenye familia zao, huku akibisha hodi katika nyoyo zao, dhamiri zao nyofu na katika nyumba zao, katika hali na mazingira haya, jambo la msingi kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, na kumkaribisha, tayari kumshirikisha furaha, majonzi na changamoto za maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na ujasiri wa kuweza kumkaribisha Bikira Maria.

Watu wa Mungu wamfungulie Bikira Maria malango ya maisha yao
Watu wa Mungu wamfungulie Bikira Maria malango ya maisha yao

Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano ya maisha ya kiroho, kwani ni kielelezo cha Eva mpya, Sanduku la Agano, Mlango wa huruma ya Mungu na mbingu, Nyota angavu ya asubuhi na Mama wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo makini cha upendeleo wa Mungu katika maisha yake, akamkinga na dhambi pamoja na mauti, ili aweze kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kumfuasa Kristo kwa ujasiri na moyo mkuu. Huu ni mwaliko wa kuingia katika shule ya upendo inayoongozwa na kusimamiwa na Bikira Maria.

Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele
Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele

Hapa waamini wanapaswa kukubali kuona kwa jicho la imani: mateso na mahangaiko ya Bikira Maria tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu hadi aliposimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa akiinamisha kichwa na kukata roho! Waamini wajitahidi kumchukua Bikira Maria katika maisha yao kwa kujiweka wakfu kwa Bikira Maria; kwa kusali na kutafakari Rozari ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili, yaani: maisha, utume na historia ya kazi nzima ya ukombozi na kwamba, hii ni Biblia ya waamini wa kawaida! Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria pamoja na kufanya mapilizi kwa ajili ya dhambi za walimwengu. Ili kukuza na kudumisha moyo na ari ya Ibada kwa Bikira Maria kuna haja ya kujikita katika fadhila ya: imani, utii, unyenyekevu, huruma, uwajibikaji pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu!

Ibada kwa Bikira Maria
03 May 2024, 15:29