Tafuta

Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu la mbingu, anaomba daima kwa ajili yetu. Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu la mbingu, anaomba daima kwa ajili yetu. 

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Chanzo cha Imani, Matumaini na Mapendo: Ushuhuda

Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni alama dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mungu, ambako toka huko atarudi (Mdo 1:11, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu (Kol 3:3.) Kristo Yesu kichwa cha Kanisa, anatutangulia katika Ufalme mtukufu wa Baba ili nasi, viungo vya huo mwili, tuishi katika tumaini la kuwa siku moja pamoja naye milele. Hii pia ni Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Akili Mnemba!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji, leo Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Zimepita siku arobaini tangu tulipoadhimisha sherehe ya Ufufuko wake Bwana. Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni alama dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya mungu, ambako toka huko atarudi (Mdo 1:11, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu (Kol 3:3.) Kristo Yesu kichwa cha Kanisa, anatutangulia katika Ufalme mtukufu wa Baba ili nasi, viungo vya huo mwili, tuishi katika tumaini la kuwa siku moja pamoja naye milele. Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu la mbingu, anaomba daima kwa ajili yetu kama mshenga anayetuhakikishia kumiminwa kwa daima Roho Mtakatifu. Rej. KKK 666-667. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2024 unanogeshwa kwa kauli mbiu Baba Mtakatifu anatoa ujumbe unaobeba kauli mbiu: “Akili Mnemba (AI) na Hekima ya Moyo: Kuelekea katika Mawasiliano Imara ya Mwanadamu.” Kauli mbiu hii ni mwendelezo wa ujumbe ambao Baba Mtakatifu aliutoa katika maadhimisho ya Siku ya Amani Ulimwenguni ambapo alikazia kuhusu maendeleo ya mifumo ya akili mnemba, yanavyoathiri ulimwengu wa mawasiliano. Hivyo, hupelekea katika maswali ya kina kuhusu asili ya mwanadamu, utofauti wetu na hatima ya viumbe “homo sapiens” katika kipindi hiki cha akili mnemba. Leo Yesu anapopaa mbinguni anawaachia Mitume wake na Kanisa lote wajibu mkubwa wa kwenda duniani kote kuhubiri Neno lake kwa kila kiumbe, Lengo ni kwenda kutuandalia makao ya milele kwa Baba, na kuketi kuumeni kwa Baba katika utukufu.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu
Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu

Tendo hili linakamilisha kazi yake ya kutukomboa sisi wanadamu hapa duniani. Hamu hii imo ndani ya wote, hata wasioamini… Mungu ameiweka nafsini mwetu nayo imekuwa sehemu yetu… hivi hata katika kutenda dhambi mwanadamu huyu huwa anatafuta furaha, ukamilifu na hali njema ila kwa namna isiyo sawa… ni hali hii ya kutafuta kupanda mbinguni juu humpelekea mwanadamu kuwa na mahangaiko mengi, akijaribu kushika hili na kuliacha anapogundua kumbe hilo sio ukamilifu wenyewe, roho ya mtu huyu hutulia tu ifikapo katika Mungu aliyeiumba kwa ajili yake (Mtakatifu Augustino) hivi ni dhahiri tupo duniani tumjue Mungu, tumpende, tumtumikie ili kufika kwake mbinguni. baada ya kujionyesha kwa siku arobaini kwa Mitume na wanafunzi wake katika mwili wake wa utukufu, alipaa mbinguni na kuketi kuume kwa Mungu Baba kama tunavyokiri katika kanuni ya imani. Ndiye Bwana anayetawala katika utukufu wa milele wa Mwana wa Mungu na kutuombea daima kwa Baba. Anaahidi kututumia Roho wake Mtakatifu na kutupatia tumaini la kufika siku moja mbinguni, kwa kuwa amekwenda kutuandalia mahali (KKK ufupisho makini No. 132). Lakini pamoja na ahadi hizo, Yesu leo anatupatia sisi sote wajibu mkubwa wa kumshuhudia na kumtangaza kwa kila kiumbe. Lakila mmoja wetu aazimie neno hili moyoni mwake ya kuwa iwe iwavyo, katika hali yoyote, sala yetu iwe “Mbinguni nitapanda na moyo wangu utatlia…” Na hili ndio linakuwa fundisho letu litakaloongoza tafakari yetu ya leo yaani kutangaza injili kwa kila kiumbe.

Sherehe ya Kupapa Bwana Mbinguni: Tamko la Jubilei 2025
Sherehe ya Kupapa Bwana Mbinguni: Tamko la Jubilei 2025

UFAFANUZI: Katika somo la kwanza na somo la Injili tumesikia juu ya agizo ambalo Bwana wetu Yesu Kristo aliwaachia Mitume wake, siku ile kabla ya kupaa la kuwa mashahidi wake na watangazaji wa Neno lake kwa kila kiumbe. Waandishi wa vitabu vya Matendo ya Mitume na Injili ya Marko, waliwaandikia Wakristo wa nyakati zao ili kuwakumbusha juu ya agizo ambalo Bwana aliwaachia Mitume wake. Ili nao waendelee kumshuhudia na kumtangaza Bwana na wala wasibaki wamesimama na kusubiria ujio wa pili wa Bwana kama walivyokuwa wakidhani kuwa upo karibu (kadiri ya Matendo ya Mitume), au wasisite kumshuhudia na kumtangaza Bwana licha ya madhulumu wanayoyapata (Injili ya Marko). Mtume Paulo katika somo la pili anawafundisha Wakristo wa Efeso juu ya uweza na utajiri wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo. Mungu alimfufua Yesu kutoka wafu, akamketisha mkono wake wa kuume na akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa. Kwa hiyo, Kristo akiwa ndiyo kichwa cha kanisa, nasi tukiwa viungo vya mwili wake yaani kanisa, yupo nasi daima katika utume wetu. Ukweli ni kwamba Yesu Kristo alipaa mbinguni siku ileile ya ufufuko wake, kama Injili ya leo inavyoshuhudia. Lakini mwandishi wa Kitabu cha Matendo ya mitume, yaani Mt. Luka, anazungumzia siku arobaini, akitaka kueleza kuwa Yesu akiwa na mwili wa utukufu, baada ya kufufuka kwake aliwatokea mitume na wafuasi wake mara kwa mara kwa kipindi cha siku arobaini, akiwaimarisha katika imani; akiwathibitishia kuwa kweli amefufuka na ni mzima. Hivyo, Kupaa kwa Bwana ni tendo la kihistoria si la kubuni. Kristo amepaa mbinguni, ni adhimisho la matumaini yetu kwamba kama Yeye alivyoshinda kifo na mauti ushindi huo si wake peke yake bali ni wetu pia. Kwamba tukiyashiriki vema mafumbo tuliyoachiwa kwa moyo mnyofu na utii kamili basi wakati utakapofika nasi ‘tutapaa mbinguni’ na kujipatia furaha isiyo na mwisho…

Maadhimisho ya Siku 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni
Maadhimisho ya Siku 58 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni

Yesu amepaa mbinguni, Bwana kwa sauti ya baragumu, alleluia… amepaa ili apokee tuzo baada ya utume wake duniani kufanikiwa kwa 100%, amepaa ili ashike kiti cha utawala kama Mkuu wa Kanisa na Bwana wa viumbe vyote, na huko mbinguni amefanyika Mfalme kuume kwa Mungu Baba yake, amepaa ili kutuletea Roho Mtakatifu atuimarishie imani yetu na kutuongoza vema… kadhalika Kristo amepaa mbinguni kwenda kutuandalia makao kwenye nyumba ya Baba [Yoh14:2-3] na nyakati zitakapotimia atarudi kutuchukua ili alipo Yeye nasi tuwepo kwa milele (Yn 14:4). Bwana wetu Yesu Kristo leo anapopaa kwenda kwa Baba yake si kwamba anawaacha mitume hapa duniani waendeleze utume huo aliowaachia pekee yao. Lakini, Kristo anapopaa anawaahidi Mitume wake kuwa atakuwa pamoja nao katika utume huu kama alivyodhihirisha hilo katika somo la injili kuwa mara baada ya mitume kupewa agizo, “wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na akilithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.” Vilevile anawaahidi nguvu ya Roho Mtakatifu ambaye atakuwa akitenda kazi pamoja nao katika utume wao wa kuwa mashahidi wake kwa kila kiumbe. Sisi nasi tumepokea wajibu huo huo kama walivyokuwa wamepokea Mitume na anatuhahidi kuwa pamoja nasi katika utekelezaji wa agizo lake hilo. Imani ya kikristo ni zawadi ya Mungu kwetu ambayo tumeipokea bure katika kanisa kwa njia ya Sakramenti ya ubatizo, lakini baada ya kuipokea tunawajibika katika kuiishi Imani hiyo na kuieneza kwa watu wengine ambao bado hawajamtambua Kristo, kwa njia ya kuwahubiria Neno la Mungu, kuwafundisha mafundisho mbalimbali ya Kanisa na kuwaongoza kwa njia ya mifano yetu mizuri tunayowaonyesha, ili nao waweze kumsogelea na kumpokea Kristo. Kuhubiri Neno la Mungu si jambo la hiari na wala haliwahusu watu wachache kama vile makatekista, watawa na makleri tu; bali ni agizo la lazima kwa kila mbatizwa. Kwani, Bwana mwenyewe ametupatia agizo hili kwa kusema “Enendeni ulimwenguni kote, mkahubiri Injili kwa kila kiumbe.” Tunaweza tukajiuliza swali nini hasa natakiwa nikishuhudie na kukitangaza kwa wengine? Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Furaha ya Injili anatupatiajibu la swali hili anaposema kuwa: “…kila mmoja wetu anapaswa kutafuta njia za kumwasilisha Yesu mahali popote tunapokuwa. Sisi sote tunapaswa kuwapa ushuhuda wa wazi wa upendo wenye kuokoa wa Bwana…kile ulichokuja kutambua, kile kilichokusaidia kuishi na kukupa matumaini, ndicho unachotakiwa kukiwasilisha kwa wengine…” yaani ndiyo hiyo imani yetu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza Kristo Yesu katika maisha yao
Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza Kristo Yesu katika maisha yao

Katika Ulimwengu mamboleo bado wapo watu wengi ambao bado hawajafikiwa na Neno la Mungu na kumfahamu Kristo; na wapo wengine wengi ambao hapo awali walilipokea Neno hilo lakini sasa wamepoa katika Imani – wote hao wanatuhitaji sisi twende tukawahubirie Neno hilo na kuihuisha tena Imani yao na kuwapata matumaini nachelea kusema daima maneno ya Krsto tazama nipo pamoja anyi hata mwisho wa nyakati, leo maendeleo ya technolojia ya mawasiliano injili inaendelea kutangazwa na kupitia radio, TV, mitandao ya kijamii, na ushuhuda wazi ni huu tunaofanya sisi hapa Radio Vatican na kurasa zetu nyingine za mawasiliano, tunawafikia sasa upokeaji na utendaji ubabaki kwako wewe msikilizaji ana msomaji wetu Mungu azidi kukufunulia siri zake, kwa wale waliorudi nyuma katika imani. Swali la kujiuliza kila mmoja wetu liwe hili je, tunatekeleza kweli agizo hilo la Bwana katika mazingira yetu tunayoishi? Familia zetu za Kikristo zinamhubiri na kumshuhudia Kristo katika maisha yao ya kifamilia kwa kuishi maisha safi ya kikristo, kulea watoto wao katika misingi bora na maadili ya kikristo na kuwa mfano bora kwa familia nyingine na majirani wanaoishi nao? Wafanyakazi wa sekta binafsi na umma, nanyi mnamhubiri na kumshuhudia Kristo kupitia huduma zenu mnazozitoa kwa watu – je, huduma zenu hizo mnazozitoa zinawafanya watu wengine wamwone Kristo katika ninyi? Wapendwa Wakristo wenzangu nanyi je, mnamhubiri kweli Kristo katika mazingira yenu na kuwafanya ndugu zenu waweze kumtambua na kumwongokea Kristo kutokana na mienendo yenu mizuri? Tumshuhudie na kumtangaza Bwana pia kwa njia ya maneno na matendo yetu kwa kuuishi vema ukristo wetu. Tumshuhudie na kumtangaza Kristo tunapokuwa katika pilikapilika za kujitafutia riziki zetu, katika kumbi za starehe na burudani, katika vyombo vya usafiri, viwanjani, tunapotumia vyombo vya mawasiliano- mfano simu na mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Facebook, WhatsApp, Twitter n.k kote huko tusisite kumtangaza na kumshuhudia Kristo, kwa kuishi maadili mema ya Kikristo na kutenda matendo mema. Na mazungumzo yetu yawafanye wengine wanaotusikia, wamtambue, wamjue na  kisha wamwongokee Kristo kupitia sisi.

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo

Ikiwa tu nitaishi uhalisia wa maisha yangu na kuzingatia lengo la Mungu katika kuniumba “…enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni?” (Mdo 1:11)… hii ni dalili ya uzubaifu, tamaa ya yasiyowezekana… Tuache kutazama mawingu na turudi kwenye uhalisia wa maisha, tusishangae jua, mwezi na nyota, maisha halisi yapo nyumbani na katika jumuiya… tusiishi maisha bandia, tuchuchumie wito tulioitiwa wa kufanana na kumfuasa Kristo… tusilumbane, tupendane, tusameheane, tujijengee ujasiri na uhodari, kuona tunapita katika katika majira gani na alama za nyakati zinatufunulia nini, kukumbatiana kwa busu takatifu, kuheshimiana, kuwa wakweli, kujitambua sisi ni akina nani na lipi hasa lengo la uwepo wetu duniani… kuzijua karama tulizojaliwa, mapungufu tuliyonayo, uimara na udhaifu wetu, kusali bila kuchoka na kujiunda upya kila wakati… safari ya kiroho inatuelekeza kudumu katika nuru ya Kristo mfufuka… huyo tu tumtafute, huyo tu tumpende, huyo tu tumtumikie na huko alikopaa Bwana nami nitafika nikifuata yale aliyo niagiza kutenda na kusema kazi ya kumhubiri na kumshuhudia Kristo kwa kila kiumbe inatudai tuwe watu wenye Imani thabiti, wenye upendo, wajasiri, wavumilivu na wenye moyo wa majitoleo ili tusiweze kukata tamaa kirahisi hasa pale tunapokutana na magumu au vikwazo katika utume wetu kama vile: ujumbe wetu unaposhindwa kupokeleka, tunapodhihakiwa na kutukanwa, tunaponyanyaswa na kuteswa na hata pengine kuuawa. Hizo zote ni changamoto ambazo tunaweza kukutana nazo wakati tukitekeleza utume wetu, lakini tusikate tamaa, bali tubaki waaminifu katika kuikiri Imani yetu, kwani Kristo yupo pamoja nasi katika utume wetu kamwe hatatuacha pekee yetu. Tuombe neema yake itusindikize katika kutimiza vema wajibu huu aliotuachia wa kumshuhudia na kumtangaza Yeye kwa kila kiumbe, ili kama Yeye alivyoshinda na akapokea taji la ushindi, atujalie nasi kushinda katika utume wetu ili baada ya kumaliza vema maisha haya, tupate kulipokea lile taji alilotuwekea tayari katika ufalme wa Baba yake.

Kupaa Bwana
11 May 2024, 09:59