Askofu Martin Banga Ayanyaki, OSA., Askofu Jimbo Katoliki Buta, Nchini DRC
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Aprili 2024 amemteua Mheshimiwa sana Padre Martin Banga Ayanyaki, O.S.A, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Buta, nchini DRC. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Martin Banga Ayanyaki, O.S.A., alikuwa ni Msimamizi wa Shirika la Mtakatifu Augustino Kanda ya Haut-Uélé, nchini DRC. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Martin Banga Ayanyaki, O.S.A., alizaliwa tarehe Mosi, Desemba 1972 huko Dungu, Kanda ya Haut-Uélé, nchini DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 30 Novemba 2002 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Agosti 2003 huko Poko, Jimbo Katoliki la Dungu-Doruma.
Tangu wakati huo kama Padre aliweza kutekeleza utume wake kama Paroko-usu, Mshauri wa Shirika la Mtakatifu Augustino na Paroko hadi mwaka 2010. Baadaye akachaguliwa kuwa Mkuu wa Vikarieti ya Shirika la Mtakatifu Augustino kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2014. Baadaye akatumwa na Shirika kwenda Roma kujiendeleza zaidi, wakati wa masomo alisaidia pia shughuli za kichungaji kwenye Konventi ya “Santa Maria del Popolo” kati yam waka 2014 hadi mwaka 2020 na kunako mwaka 2020 akajipatia Shahada ya Uzamivu katika somo la masuala ya jamii “Sociology. Na tangu mwaka 2022 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Buta amekuwa ni Msimamizi wa Shirika la Mtakatifu Augustino Kanda ya Haut-Uélé, nchini DRC na Jaalimu wa Sayansi Jamii na “Atholopologia” Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino, nchini DRC.