Tafuta

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Kutukuka Kwa Mwili wa Mwanadamu

Baba Mtakatifu anasema, kupanda juu mlimani kunahitaji nguvu za ziada na kama Kanisa Kristo Yesu anapenda kuwavuta waja wake kwake. Kristo Yesu anaendelea kujifunua na kuzungumza na wafuasi wake kwa: Neno, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na uzuri wa mbinguni ambapo waamini wanaalikwa kuukumbatia, ili kwa furaha na shangwe waweze kuwa mahali alipo Yeye ambaye ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Tokeo la mwisho la Yesu linakamilika na kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu uliojionesha katika sura ya wingu na mbingu (Lk 24:51) ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Kwa namna moja tofauti kabisa na ya pekee atajionesha kwa Paulo “kama mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” katika tokeo la mwisho lililomfanya kuwa Mtume. Hali iliyofunikwa ya utukufu wa Kristo Mfufuka kipindi hiki inaonekana katika maneno yake ya fumbo kwa Mariamu Magdalena: “Sijapata kwenda kwa Baba.Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu.” Hii inaonesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Tukio ambalo kwa upande mmoja ni la kihistoria na bora sana linaloonesha kupita toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Lakini yote yanabaki yakiwa yameungana kabisa na lile la kwanza yaani kushuka kutoka mbinguni kulikotekelezwa katika Fumbo la Umwilisho. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba. Kristo peke yake ameweza kumfungulia mtu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shila letu na kwamba, akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake!

Sherehe ya Kupalizwa Bwana Mbinguni, Tumaini la uzima wa milele
Sherehe ya Kupalizwa Bwana Mbinguni, Tumaini la uzima wa milele

Huku ni kuinuliwa juu ya Msalaba ambako huonesha na kutangaza kuinuliwa kwa kupaa mbinguni. Huo ndio mwanzo wake. Mbinguni Kristo Yesu anatekeleza Ukuhani wake daima, Yeye ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu Baba wa mbinguni. Kristo Yesu ameketi kuume kwa Baba, maana yake: ameketi katika utukufu na heshima ya Kimungu, ambaye Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Kuanzia hapo Mitume wamekuwa ni mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mwisho. Rej. KKK 659-664. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbingu, Dominika tarehe 12 Mei 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu amesema, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ambako ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Mk 16:19. Baba Mtakatifu anasema, kupanda juu mlimani kunahitaji nguvu za ziada na kama Kanisa Kristo Yesu anapenda kuwavuta waja wake kwake. Kristo Yesu anaendelea kujifunua na kuzungumza na wafuasi wake kwa: Neno, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na uzuri wa mbinguni ambapo waamini wanaalikwa kuukumbatia, ili kwa furaha na shangwe waweze kuwa mahali alipo Yeye ambaye ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa. Rej. Kol1:18; 1Kor 12:12-27. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, wabatize na kutoa pepo wachafu, wakabiliane na nyoka pamoja na kuwaponya wagonjwa. Rej. Mk 16:16-18.

Mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mipaka
Mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mipaka

Kwa maneno machache anasema Baba Mtakatifu Francisko huu ni mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu: kwa kutoa zawadi ya maisha, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na hivyo kuendelea kujitenga na maovu, kwa kujibu ubaya kwa wema; kwa kuwahudumia wanaoteseka. Yote haya kwa njia ya Roho Mtakatifu yataweza kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kwa sababu ya ujirani mwema, maneno na matendo mema na kwamba, kwa njia hii hata moyo hupata furaha ya daima. Jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kujiuliza ikiwa kama ndani mwao wanayo hamu ya Mungu na upendo wake usiokuwa na kifani pamoja na maisha yake ya uzima wa milele. Au pengine waamini wanaelemewa zaidi ili kutafuta mafanikio katika maisha, fedha pamoja na raha za dunia hii? Je, ile hamu yake ya kutaka kwenda mbinguni, inamfanya ajitenge na wengine? Inamfanya ajifungie katika upweke na ubinafsi wake? Au hii inakuwa ni hamasa ya kuwapenda wengine kwa moyo wote na hivyo kujisikia kuwa ni wandani wa safari kuelekea mbinguni. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni awasaidie waamini ambao bado wanasuasua huku bondeni kwenye machozi, ili waweze kutembea kwa pamoja katika mshikamano, unaosimikwa katika furaha kuelekea katika utukufu wa Mungu mbinguni.

Kupaa Bwana
12 May 2024, 14:35

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >