Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Fadhila ya Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua. “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia pia fadhila ya subira katika maisha na utume wa Kristo Yesu.
Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Baba Mtakatifu kuhusu fadhila ya haki, amekazia zaidi fadhila mbadala zinazowawezesha watu kuishi kwa amani, mtu wa haki daima yuko tayari kuomba msamaha, ni shuhuda wa kanuni maadili na utu wema, kwa hakika watu wa haki ni wachache sana ndani ya jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa haki. Katika maisha ya jamii, kila mtu anapaswa kutendewa kwa haki sanjari na kuheshimu utu wake wake. Fadhila ya haki inadai fadhila nyingine kama: ukarimu, heshima, shukrani, urafiki, uaminifu na kwamba hizi fadhila zinazochangia kuishi pamoja kwa watu vizuri. Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu na uthabiti katika kufuata mema. Yaimarisha uamuzi wa kushindana na vishawishi, kushinda vikwazo vya maisha adili. Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu, hata hofu ya kifo; na kukabiliana na majaribu, na madhulumu. Yamwandaa mtu kuwa tayari hata kujikatalia na kutoa sadaka ya uzima wake kwa ajili ya kutetea haki. Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu. Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu. Rej. KKK 1808.
Kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Ni fadhila inayopatikana pia katika nyanja za falsafa za akina Aristotle inayofundisha sanaa ya maisha, ili hatimaye, watu waweze kupata furaha ya kweli katika maisha. Fadhila ya kiasi “enktateia” inabeba uzito wa juu katika fadhila mbalimbali. Yahifadhi nguvu ya utashi wa kutawala silika na huziweka tamaa katika mipaka ya kile kilicho kinyofu. Mtu wa kiasi huongoza vionjo vya silika kuelekea kilicho chema, na hushikilia busara safi: “Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako.” Kiasi husifiwa mara nyingi katika Agano la Kale. Usizifuate tamaa za roho yako, bali ujizuili uchu wake.” Katika Agano Jipya huitwa: “Kiasi” au “utulivu.” Tunapaswa kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa katika ulimwengu huu. Kuishi vyema si kitu kingine zaidi ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na roho yote na kwa nguvu zote. Toka hapo yatokea kwamba upendo unashikwa wote bila uharibifu (kwa njia ya kiasi.) Hakuna bahati mbaya inayoweza kuusumbua (na hii ndiyo nguvu.) Humtii Mungu peke yake (na hii ni haki), na una makini katika kupambanua vitu, ili usije ukashangazwa na uwongo au udanganyifu (na hii ni busara.) Rej. KKK 1809. Kiasi ni fadhila inayoratibu kile anachofikiri mtu na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa. Hata divai, mtu anapaswa kuitumia kwa kiasi. Mtu wa kiasi huchagua na kupanga maneno yake na kamwe hapendi hasira ivuruge mahusiano na urafiki, kwani kurejesha tena hali hii yataka moyo! Kiasi ni fadhila muhimu sana katika maisha ya kifamilia ili kuratibu kinzani, migogoro na hasira. Kila jambo anasema Baba Mtakatifu lina wakati; kuna wakati wa kuzungumza na wakati wa kukaa kimya. Kuna wakati wa kukaa pweke na wakati wa kushirikiana na wengine. Mtu wa kiasi daima anaonesha furaha, amani na utulivu wa ndani. Kuna wakati mtu anapaswa kuzungumza, lakini afanye yote kwa kiasi. Wakati mwingine karipio linasaidia kuliko ukimya unaosimikwa katika hasira na chuki. Mtu mwenye kiasi anajua kuwa hakuna kinachomsumbua zaidi kuliko kuwarekebisha wengine, kwani kwake hili ni jambo muhimu sana, vinginevyo uovu unaweza kutawala. Mtu wenye kiasi anathibitisha matumizi ya kanuni kamili, anadai maadili yasiyoweza kujadiliwa, lakini pia ni mtu mwenye huruma kwa jirani zake. Kwa hiyo zawadi ya mtu mwenye kiasi ni usawa, sifa yenye thamani kama ilivyo nadra.
Kwa kweli, kila kitu katika ulimwengu wetu kinatusukuma kuelekea ziada. Badala yake, kiasi huenda vizuri na mitazamo ya Kiinjili kama vile: Udogo, busara, kujificha na upole. Wale walio na kiasi wanathamini heshima ya wengine, lakini hawaifanyi kuwa kigezo pekee cha kila tendo na kila neno. Mtu mwenye kiasi anafahamu mambo nyeti, anajua kulia na wala haoini aibu. Akichechemea na kuanguka, anainuka na kusimama tena; ni mshindi katika maisha yake ya kawaida; maisha ambayo kwa kiasi fulani yamefichika, lakini pia anatambua kwamba, anawahitaji wengine, ili kukamilisha furaha yake. Kiasi kinamfanya mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha, na kuweza kushirikiana na wengine katika: upole wa urafiki, imani kwa watu wenye hekima, na kuweza kushangaa kwa uzuri wa kazi ya uumbaji. Furaha pamoja na kiasi ni furaha inayositawi katika mioyo ya wale wanaotambua na kuthamini kile ambacho ni muhimu zaidi maishani. Tuombe kwa Mwenyezi Mungu atujalie karama hii: karama ya ukomavu, ukomavu wa umri, ukomavu wa kihisia, ukomavu wa kijamii na zawadi ya kiasi. Kristo Yesu anamponya mzaliwa kipofu na ushuhuda wake wa imani baada ya malumbano makali. Wakati wa malumbano haya yote, kipofu yule alikuwa na roho ya Kristo, ingawaje Yesu mwenyewe hakuonekana kwa macho. Mtu aliyeangazwa hahitaji uwepo wa moja kwa moja wa Yesu. Kwani Yesu alimwacha ili kipofu ajiongeze mwenyewe na nguvu ya Roho aliyempata. Baada ya mizengwe yote na kufukuzwa nje. "Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alienda kumtafuta." Kisha alimwuliza: "Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?" Naye akajibu akasema, "Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? Yesu akamwambia, “Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.” Akasema “Naamini, Bwana.” Rej.Yn 9: 35-38. Kuamini maana yake ni kumpokea Kristo Yesu katika maisha. Kusadiki ni chaguo la upendo. Huu ni ushuhuda wa imani ya mtu huyu katika neno analoliona, ufunuo wa mwana wa Mungu, anayemwalika kumpokea katika maisha yake.
Hii ndiyo sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano Mei Mosi, 2024 kuhusu fadhila za Kimungu ambazo zinaweka msingi, zinahuisha, kuaminisha utendaji adili wa Mkristo. Zinapasha habari na kuzihuisha fadhila zote za maadili. Zinamiminwa na Mwenyezi Mungu katika roho za waamini ili kuwawezesha kutenda kama watoto wake na hivyo kustahili uzima wa milele. Nazo ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu ya binadamu. Kuna fadhila tatu za Kimungu nazo ni: Imani, matumaini na mapendo. Rej. KKK 1813. Mababa wa Kanisa wanasema, imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunamsadiki Mungu na kila kitu alichokisema na alichotufunulia, na ambacho Kanisa takatifu latutaka tukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye Ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu. Ni kwa sababu hiyo mwamini hutafuta kujua na kuyafanya mapenzi ya Mungu. Mwenye haki ataishi kwa imani. Imani hai hutenda kazi kwa mapendo. Paji la imani ladumu ndani yake ambaye hakutenda dhambi dhidi yake. Lakini imani bila matendo imekufa; imani ikinyimwa matumaini na mapendo haiwezi kumwunganisha mwamini kikamilifu na Kristo Yesu, na hawezi kuwa kiungo hai cha mwili wake.
Mfuasi wa Kristo anatakiwa kuishika, kuiishi, kuiungama, kuishuhudia na hatimaye, kuineza na kuwa tayari kuikiri mbele ya watu, tayari kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, kati ya madhulumu ambayo hayakosekani katika Kanisa. Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu na kwamba, waamini wanahimizwa na Kristo Yesu kumkiri mbele ya watu, naye atamkiri mbele ya Baba yake wa mbinguni. Lakini, atakayemkana mbele ya watu, Kristo naye atamkana mbele ya Baba yake aliye mbinguni. Rej. K.K.K. 1814. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Maandiko Matakatifu, Ibrahimu anatajwa kuwa ni Baba wa imani, aliyepokea wito wa Mungu na kutenda kwa haraka kiasi hata cha kuiacha nchi yake, kwa kufuata maongozi ya Mungu, kiasi hata cha kuwa tayari kumtoa sadaka, Mwanaye mpendwa Isaka, lakini akaokolewa na Malaika wa Bwana na kwa imani hii, Ibrahimu anapokea ahadi kwa Bwana kwamba katika uzao wake Mataifa yote ya dunia watajibarikia kwa sababu ya kutii sauti ya Mungu. Maandiko Matakatifu yanamtaja Mtumishi wa Mungu Musa kuwa ni mtu wa imani, aliyesimama kidete kulinda na kutetea imani yake; akawa na imani thabiti kiasi cha kuwa ni mtetezi wa watu wake, ambao daima walikuwa wanatindikiwa imani. Bikira Maria ni kielelezo makini cha mwanamke wa imani, tangu siku ile alipopashwa habari na Malaika kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, akakubali dhamana na wajibu huu kwa kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Lk 1:38.
Baba Mtakatifu anasema, Moyo Safi wa Bikira Maria ulisheheni imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, aliamua kushika njia ambayo hakutambua matatizo, changamoto na fursa zilizokuwa mbele yake. Imani ni fadhila inayomjenga Mkristo, kwa kuambata tunu msingi za imani, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko, wanafunzi wa Kristo Yesu walipokumbana na dhoruba kali na chombo kikaanza kujaa maji na Yesu mwenyewe alikuwa katika shetri, amelala juu ya mto, wanafunzi wake wakamwendea na kusema, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii? Rej. Mk 4:35-41. Baba Mtakatifu Francisko anasema, adui mkubwa wa fadhila ya imani ni woga na wasiwasi. Imani ni zawadi inayopaswa kupokelewa na kuendelea kupyaishwa siku kwa siku. Hii ndiyo imani wanayorithishwa watoto wakati wakipokea Sakramenti ya Ubatizo, hii ndiyo imani katika Ubatizo. Imani ni zawadi ambayo ni dhaifu sana na kwamba, upendo wa Mungu ndio unaoweza kuvunjilia mbali hofu ya kifo. Imani ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anaitoa kwa mtu binafsi na kwamba, kama waamini wangekuwa na imani kubwa kiasi cha chembe ya haradali, wangeweza kutenda maajabu: wangeweza kuuambia mkuyu huu: “Ng’oka, ukapandwe baharini,” nao ungewatii.” Lk 17:6. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo, hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Kristo Yesu ili awaongezee imani. Rej. Lk 17:5.