Tafuta

Katekesi Kuhusu Fadhila Na Mizizi ya Dhambi: Fadhila ya Upendo

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi amegusia fadhila ya upendo. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa...

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.  “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Upendo ni chachu ya utakatifu wa maisha
Upendo ni chachu ya utakatifu wa maisha

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia pia fadhila ya subira katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

Waamini wakihudhuria Katekesi ya Papa kuhusu Upendo
Waamini wakihudhuria Katekesi ya Papa kuhusu Upendo

Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Baba Mtakatifu kuhusu fadhila ya haki, amekazia zaidi fadhila mbadala zinazowawezesha watu kuishi kwa amani, mtu wa haki daima yuko tayari kuomba msamaha, ni shuhuda wa kanuni maadili na utu wema, kwa hakika watu wa haki ni wachache sana ndani ya jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa haki. Katika maisha ya jamii, kila mtu anapaswa kutendewa kwa haki sanjari na kuheshimu utu wake wake. Fadhila ya haki inadai fadhila nyingine kama: ukarimu, heshima, shukrani, urafiki, uaminifu na kwamba hizi fadhila zinazochangia kuishi pamoja kwa watu vizuri. Nguvu ni fadhila adili inayothibitisha ushupavu katika magumu na uthabiti katika kufuata mema. Yaimarisha uamuzi wa kushindana na vishawishi, kushinda vikwazo vya maisha adili. Fadhila ya nguvu huwezesha kushinda hofu, hata hofu ya kifo; na kukabiliana na majaribu, na madhulumu. Yamwandaa mtu kuwa tayari hata kujikatalia na kutoa sadaka ya uzima wake kwa ajili ya kutetea haki. Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu. Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu. Rej. KKK 1808.

Upendo ni fadhila ya Kimungu
Upendo ni fadhila ya Kimungu

Kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Ni fadhila inayopatikana pia katika nyanja za falsafa za akina Aristotle inayofundisha sanaa ya maisha, ili hatimaye, watu waweze kupata furaha ya kweli katika maisha. Fadhila ya kiasi “enktateia” inabeba uzito wa juu katika fadhila mbalimbali. Yahifadhi nguvu ya utashi wa kutawala silika na huziweka tamaa katika mipaka ya kile kilicho kinyofu. Mtu wa kiasi huongoza vionjo vya silika kuelekea kilicho chema, na hushikilia busara safi: “Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako.” Kiasi husifiwa mara nyingi katika Agano la Kale. Usizifuate tamaa za roho yako, bali ujizuili uchu wake.” Katika Agano Jipya huitwa: “Kiasi” au “utulivu.” Tunapaswa kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa katika ulimwengu huu. Kuishi vyema si kitu kingine zaidi ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na roho yote na kwa nguvu zote. Toka hapo yatokea kwamba upendo unashikwa wote bila uharibifu (kwa njia ya kiasi.) Hakuna bahati mbaya inayoweza kuusumbua (na hii ndiyo nguvu.) Humtii Mungu peke yake (na hii ni haki), na una makini katika kupambanua vitu, ili usije ukashangazwa na uwongo au udanganyifu (na hii ni busara.) Rej. KKK 1809. Kiasi ni fadhila inayoratibu kile anachofikiri mtu na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa. Hata divai, mtu anapaswa kuitumia kwa kiasi. Mtu wa kiasi huchagua na kupanga maneno yake na kamwe hapendi hasira ivuruge mahusiano na urafiki, kwani kurejesha tena hali hii yataka moyo! Kiasi ni fadhila muhimu sana katika maisha ya kifamilia ili kuratibu kinzani, migogoro na hasira. Kila jambo anasema Baba Mtakatifu lina wakati; kuna wakati wa kuzungumza na wakati wa kukaa kimya. Kuna wakati wa kukaa pweke na wakati wa kushirikiana na wengine. Mtu wa kiasi daima anaonesha furaha, amani na utulivu wa ndani. Kuna wakati mtu anapaswa kuzungumza, lakini afanye yote kwa kiasi. Wakati mwingine karipio linasaidia kuliko ukimya unaosimikwa katika hasira na chuki. Mtu mwenye kiasi anajua kuwa hakuna kinachomsumbua zaidi kuliko kuwarekebisha wengine, kwani kwake hili ni jambo muhimu sana, vinginevyo uovu unaweza kutawala. Mtu wenye kiasi anathibitisha matumizi ya kanuni kamili, anadai maadili yasiyoweza kujadiliwa, lakini pia ni mtu mwenye huruma kwa jirani zake. Kwa hiyo zawadi ya mtu mwenye kiasi ni usawa, sifa yenye thamani kama ilivyo nadra.

Matunda ya upendo ni wema, furaha, amani na huruma
Matunda ya upendo ni wema, furaha, amani na huruma

Kwa kweli, kila kitu katika ulimwengu wetu kinatusukuma kuelekea ziada. Badala yake, kiasi huenda vizuri na mitazamo ya Kiinjili kama vile: Udogo, busara, kujificha na upole. Wale walio na kiasi wanathamini heshima ya wengine, lakini hawaifanyi kuwa kigezo pekee cha kila tendo na kila neno. Mtu mwenye kiasi anafahamu mambo nyeti, anajua kulia na wala haoini aibu. Akichechemea na kuanguka, anainuka na kusimama tena; ni mshindi katika maisha yake ya kawaida; maisha ambayo kwa kiasi fulani yamefichika, lakini pia anatambua kwamba, anawahitaji wengine, ili kukamilisha furaha yake. Kiasi kinamfanya mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha, na kuweza kushirikiana na wengine katika: upole wa urafiki, imani kwa watu wenye hekima, na kuweza kushangaa kwa uzuri wa kazi ya uumbaji. Furaha pamoja na kiasi ni furaha inayositawi katika mioyo ya wale wanaotambua na kuthamini kile ambacho ni muhimu zaidi maishani. Tuombe kwa Mwenyezi Mungu atujalie karama hii: karama ya ukomavu, ukomavu wa umri, ukomavu wa kihisia, ukomavu wa kijamii na zawadi ya kiasi. Kristo Yesu anamponya mzaliwa kipofu na ushuhuda wake wa imani baada ya malumbano makali. Wakati wa malumbano haya yote, kipofu yule alikuwa na roho ya Kristo, ingawaje Yesu mwenyewe hakuonekana kwa macho. Mtu aliyeangazwa hahitaji uwepo wa moja kwa moja wa Yesu. Kwani Yesu alimwacha ili kipofu ajiongeze mwenyewe na nguvu ya Roho aliyempata. Baada ya mizengwe yote na kufukuzwa nje. "Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alienda kumtafuta." Kisha alimwuliza: "Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?" Naye akajibu akasema, "Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? Yesu akamwambia, “Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.” Akasema “Naamini, Bwana.” Rej.Yn 9: 35-38. Kuamini maana yake ni kumpokea Kristo Yesu katika maisha. Kusadiki ni chaguo la upendo. Huu ni ushuhuda wa imani ya mtu huyu katika neno analoliona, ufunuo wa mwana wa Mungu, anayemwalika kumpokea katika maisha yake.

Upendo humpa Mkristo uhuru wa watoto wa Mungu
Upendo humpa Mkristo uhuru wa watoto wa Mungu

Hii ndiyo sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano Mei Mosi, 2024 kuhusu fadhila za Kimungu ambazo zinaweka msingi, zinahuisha, kuaminisha utendaji adili wa Mkristo. Zinapasha habari na kuzihuisha fadhila zote za maadili. Zinamiminwa na Mwenyezi Mungu katika roho za waamini ili kuwawezesha kutenda kama watoto wake na hivyo kustahili uzima wa milele. Nazo ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu ya binadamu. Kuna fadhila tatu za Kimungu nazo ni: Imani, matumaini na mapendo. Rej. KKK 1813. Mababa wa Kanisa wanasema, imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunamsadiki Mungu na kila kitu alichokisema na alichotufunulia, na ambacho Kanisa takatifu latutaka tukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye Ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu. Ni kwa sababu hiyo mwamini hutafuta kujua na kuyafanya mapenzi ya Mungu. Mwenye haki ataishi kwa imani. Imani hai hutenda kazi kwa mapendo. Paji la imani ladumu ndani yake ambaye hakutenda dhambi dhidi yake. Lakini imani bila matendo imekufa; imani ikinyimwa matumaini na mapendo haiwezi kumwunganisha mwamini kikamilifu na Kristo Yesu, na hawezi kuwa kiungo hai cha mwili wake. Mfuasi wa Kristo anatakiwa kuishika, kuiishi, kuiungama, kuishuhudia na hatimaye, kuineza na kuwa tayari kuikiri mbele ya watu, tayari kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, kati ya madhulumu ambayo hayakosekani katika Kanisa. Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu na kwamba, waamini wanahimizwa na Kristo Yesu kumkiri mbele ya watu, naye atamkiri mbele ya Baba yake wa mbinguni. Lakini, atakayemkana mbele ya watu, Kristo naye atamkana mbele ya Baba yake aliye mbinguni. Rej. K.K.K. 1814.

Ujuzi huleta mavivuno lakini upendo hujenga
Ujuzi huleta mavivuno lakini upendo hujenga

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Maandiko Matakatifu, Ibrahimu anatajwa kuwa ni Baba wa imani, aliyepokea wito wa Mungu na kutenda kwa haraka kiasi hata cha kuiacha nchi yake, kwa kufuata maongozi ya Mungu, kiasi hata cha kuwa tayari kumtoa sadaka, Mwanaye mpendwa Isaka, lakini akaokolewa na Malaika wa Bwana na kwa imani hii, Ibrahimu anapokea ahadi kwa Bwana kwamba katika uzao wake Mataifa yote ya dunia watajibarikia kwa sababu ya kutii sauti ya Mungu. Maandiko Matakatifu yanamtaja Mtumishi wa Mungu Musa kuwa ni mtu wa imani, aliyesimama kidete kulinda na kutetea imani yake; akawa na imani thabiti kiasi cha kuwa ni mtetezi wa watu wake, ambao daima walikuwa wanatindikiwa imani. Bikira Maria ni kielelezo makini cha mwanamke wa imani, tangu siku ile alipopashwa habari na Malaika kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, akakubali dhamana na wajibu huu kwa kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Lk 1:38. Baba Mtakatifu anasema, Moyo Safi wa Bikira Maria ulisheheni imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, aliamua kushika njia ambayo hakutambua matatizo, changamoto na fursa zilizokuwa mbele yake. Imani ni fadhila inayomjenga Mkristo, kwa kuambata tunu msingi za imani, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu.

Upendo ni sura ya fadhila
Upendo ni sura ya fadhila

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Marko, wanafunzi wa Kristo Yesu walipokumbana na dhoruba kali na chombo kikaanza kujaa maji na Yesu mwenyewe alikuwa katika shetri, amelala juu ya mto, wanafunzi wake wakamwendea na kusema, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii? Rej. Mk 4:35-41. Baba Mtakatifu Francisko anasema, adui mkubwa wa fadhila ya imani ni woga na wasiwasi. Imani ni zawadi inayopaswa kupokelewa na kuendelea kupyaishwa siku kwa siku. Hii ndiyo imani wanayorithishwa watoto wakati wakipokea Sakramenti ya Ubatizo, hii ndiyo imani katika Ubatizo. Imani ni zawadi ambayo ni dhaifu sana na kwamba, upendo wa Mungu ndio unaoweza kuvunjilia mbali hofu ya kifo. Imani ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anaitoa kwa mtu binafsi na kwamba, kama waamini wangekuwa na imani kubwa kiasi cha chembe ya haradali, wangeweza kutenda maajabu: wangeweza kuuambia mkuyu huu: “Ng’oka, ukapandwe baharini,” nao ungewatii.” Lk 17:6. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo, hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Kristo Yesu ili awaongezee imani. Rej. Lk 17:5.

Utimilifu wa kazi zote ni upendo
Utimilifu wa kazi zote ni upendo

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake yake, Jumatano tarehe 8 Mei 2024 amejikita katika kuchambua fadhila ya matumaini. Mababa wa Kanisa wanasema, matumaini ni fadhila ya kimungu inayotuwezesha kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo na kutegemea, siyo nguvu zetu, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kulishika kikamilifu ungamo la matumaini yao kwa sababu Kristo Yesu ni mwaminifu daima. Ni Roho ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Kristo Yesu Mwokozi wetu, ili tukihesababiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Fadhila ya matumaini yajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na upendo. Matumaini ya Kikristo huchukua na kukamilisha matumaini ya Taifa Teule lililo na chanzo na mfano katika matumaini ya Ibrahimu, aliyebarikiwa kwa wingi wa ahadi za Mungu zilizotimilizwa katika Isaka na aliyetakaswa kwa majaribu ya sadaka. Alitumaini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa ni Baba wa Mataifa mengi. Heri za Mlimani ni muhtasari wa matumaini ya Kikristo, kwa kuonesha majaribu wanayoweza kukutana nayo katika hija ya maisha yao. Lakini kwa mastahili ya Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anawalinda katika tumaini lisilotahayarisha. Matumaini ni nanga ya roho hakika na thabiti, ni pia silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini huleta furaha hata katika majaribu na ni muhtasari wa Sala ya Baba yetu. Kila mtu anaweza kutumaini kwa msaada wa neema ya Mungu. Katika tumaini Kanisa linasali ili watu wote waokolewe. Latamani kuungana na Kristo Yesu, Mchumba wake katika utukufu wa mbinguni. Rej. KKK 1817-1821.

Mapendo ni tunda la Roho na utimilifu wa sheria
Mapendo ni tunda la Roho na utimilifu wa sheria

Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama katika hija ya maisha yao wamejitahidi kuwa ni watu wafadhila, watu wenye busara, wenye haki, wenye nguvu na kiasi; watu wa imani na matumaini? Fadhila ya matumaini ni muhimu sana kwa sababu ni kwa njia ya matumaini, waamini wanasimika matumaini yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chimbuko la matumaini ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ulimwengu mamboleo unahitaji sana fadhila ya matumaini, uvumilivu na amani, kwani mtu wa matumaini anaweza kutembea na hatimaye kuvuka nyakati za giza katika maisha. Matumaini ni fadhila inayopokelewa na watu wenye nyoyo za ujana hata kama kiumri wanaonekana kuwa ni wazee kama ilivyokuwa kwa Mzee Simeoni na Ana waliokuwa wanasubiri kumwona Masiha wa Bwana. “Mzee Simeoni na Ana wakiwa wameongozwa na Roho Mtakatifu wanamtambua Kristo Yesu kuwa ni Masiha wa Bwana. Mzee Simeoni akamshukuru Mwenyezi Mungu kwa utenzi wa sifa kwani amewawezesha kuuona wokovu, nuru na utukufu kwa watu wake Israeli. Huu ndio utenzi wa Mzee Simeoni maarufu kama: “Nunc dimittis servum tuum, Domine, secundum verbum tuum in pace: Quia viderunt oculi mei salutare tuum. Quod parasti ante faciem omnium populorum: Lumen ad revelationem gentium, et gloriam plebis tuae Israel.” Yaani: “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” Lk 2:29-32. Mzee Simeoni katika ufukara wa Mtoto Yesu anauona wokovu wa watu wa Mungu. Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa.

Upendo ni fadhila kuu
Upendo ni fadhila kuu

Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Mei 2024 kuhusu fadhila ya upendo, imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho 13: 1-10: Upendo kati ya Ndugu: “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.

Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho
Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho

Mababa wa Kanisa wanasema mapendo ni fadhila ya Kimungu inayotuwezesha kumpenda Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake mwenyewe; na jirani kama sisi wenyewe, kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Kristo Yesu aliyafanya mapendo kuwa ni Amri kuu na mpya kwa kuwapenda walio wake upeo, kielelezo cha upendo kati ya Mitume ni kuiga ule upendo wa Kristo Yesu kati yao na hivyo kukaa katika pendo lake na Kristo Yesu ndiye kielelezo cha upendo wenyewe. Mapendo ni tunda la Roho na utimilifu wa sheria. Kristo Yesu anawaamuru wafuasi wake kuwapenda hata adui zao. Bila upendo mwamini si kitu kabisa. Upendo ni sura ya fadhila. Ni chemchemi la lengo la utendaji wao wa Kikristo. Upendo wathibitisha na kutakasa uwezo wetu wa kibinadamu wa kupenda, na huuinua katika ukamilifu wa kiroho wa mapendo ya Kimungu. Upendo humpa Mkristo uhuru wa watoto wa Mungu, huku akijibu mapendo ya yule aliyetupenda kwanza. Matunda ya upendo ni furaha, amani na huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kidugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana, hubaki huru bila kujitafutia faida; ni urafiki na umoja. Utimilifu wa kazi zetu zote ni upendo. Hapo ndipo lilipo lengo. Na kwa ajili ya kulipata nasi twakimbia, twalikimbilia hilo, na mara tufikapo tutapata pumziko letu ndani yake. Rej. KKK 1822 – 1829. Mtakatifu Paulo, Mtume anakaza kusema “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.” 1Kor13:3. Kwa kuiangalia Jumuiya ya Wakorintho, Paulo Mtume akagundua kwamba, kulikuwa na mipasuko ya ndani, na baadhi ya watu walijisikia kuwa ni wanyonge na kwamba, ujuzi huleta majivuno lakini upendo hujenga. Kulikuwepo na kashfa iliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya Karamu ya Bwana, yaani Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiasi kwamba, wakutanikapo haiwezekani kula chakula cha Bwana, kwani huu ni mlo wa kipagani!

Upendo na msamaha ni chemchemi ya thawabu
Upendo na msamaha ni chemchemi ya thawabu

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo, mahusiano na mafungamano ya kirafiki, kifamilia na kijamii ni muhimu sana katika kukoleza upendo. Huu ni upendo unaojisadaka, unaofichika na kwamba, huu ni upendo unaojishusha chini na kwamba, huu ni upendo ambao kimsingi ni fadhila ya Kimungu. Huu ni upendo wa hali ya juu kabisa unaoitwa “Agape.” Huu ni upendo kwa ajili ya Mungu na jirani; upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni upendo unaowasukuma hata kuwapenda adui zao. Fadhila ya upendo inabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni kazi ya Roho Mtakatifu. “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.” Lk 6: 32-33. Upendo wa Kikristo unapenda kile kisichopendeka na kutoa msamaha wa kweli; ni upendo unaobariki na kwamba, hii ni njia nyembamba inayowapeleka waamini mbinguni kwa Baba wa milele. Upendo ndicho kipimo kitakachotumika: “Amini, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Mt 25: 40. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na ujasiri wa kukuza na kudumisha upendo.

Fadhila ya Upendo
15 May 2024, 14:32

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >