Tarehe 27 Aprili 2024, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka Kumi, tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu. Tarehe 27 Aprili 2024, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka Kumi, tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu.  

Miaka 10 Tangu Papa Yohane Paulo II Atangazwe Kuwa Mtakatifu: 2014-2024

Papa Francisko amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 27 Aprili 2024, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka Kumi, tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu. Kwa kuyaangalia maisha na utume wake, waamini wanaweza kugundua ndani mwake yale ambayo Mungu anayoweza kutenda ndani ya mja wake, aliporuhusu karama na fadhila mbalimbali kama vile: imani, matumaini na upendo kumwilishwa katika maisha na vipaumbele vyake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Akatekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ndiyo maana Kanisa linamkumbuka na kumwadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005 na kuzikwa tarehe 8 Aprili 2005. Ilikuwa ni Mei Mosi, 2011, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipomtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu waliofurika kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Aprili 2024 amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 27 Aprili 2024, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka Kumi, tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu.

Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Papa Yohane Paulo II atangazwe Mtakatifu
Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Papa Yohane Paulo II atangazwe Mtakatifu

Kwa kuyaangalia maisha na utume wake, waamini wanaweza kugundua ndani mwake yale ambayo Mwenyezi Mungu anayoweza kutenda ndani ya mja wake, anaporuhusu karama na fadhila mbalimbali kama vile: imani, matumaini na upendo kumwilishwa katika maisha na vipaumbele vyake. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuendelea kuwa waaminifu kwa amana na urithi kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa sala na maombezi yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Yohane Paulo II ili aweze kuwaombea amani, ambayo katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliipatia kipaumbele cha pekee. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbukumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari. Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo!

Mkesha wa kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo II
Mkesha wa kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo II

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake. Neema hii ikamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Binadamu na mahitaji yake msingi, alipewa kipaumbele cha pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kufanya hija za kitume 104 nje ya Italia. Akabarikiwa kufanya hija za kichungaji 142 nchini Italia, daima maneno yake yaliambatana na vitendo; akagusa na kufariji mamilioni ya watu duniani, huku akitangaza na kushuhudia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama kiini cha haki msingi za binadamu! Matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989. Kanisa likatoka kidedea na kusimama kifua mbele ili kupinga sera za kibaguzi zilizoigawa dunia, kati ya Kaskazini na Kusini: likaimarisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kujikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kama kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II: Utuombee
Mtakatifu Yohane Paulo II: Utuombee

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata dira na mwongozo wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akaimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kiasi hata cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini sana mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake, mambo yanayojionesha hata katika Nyaraka zake za kichungaji “MULIERIS DIGNITATEM” yaani “Utu na wito wa mwanamke”. Alikazia sana umuhimu wa utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuthubutu kuwatangaza watakatifu wapya 482 na wenyeheri 1319, mwaliko na changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu kama chemchemi ya utakatifu na utimilifu wa maisha ya Kikristo. Mtakatifu Yohane Pualo II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata nyakati hizi. Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mt. Yohane Paulo II

 

26 April 2024, 15:57