Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Mjini Venezia: Ibada ya Misa Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika Agano la kale ufunuo wa ufalme wa Mungu umetolewa mara nyingi kwa njia ya mifano. Vivyo hivyo sasa maumbile ya ndani ya Kanisa hujidhihirisha kwetu kwa ishara mbalimbali, zitokanazo na maisha ya wachungaji na wakulima, kama vile na kazi ya kujenga, au na maisha ya familia na arusi. Na ishara hizo zimewahi kutayarishwa katika vitabu vya Manabii. Hivyo Kanisa ni zizi, ambalo mlango wake mmoja tu na wa lazima ndiye Kristo (taz. Yn 10:1-10). Nalo ni pia kundi la kondoo, ambalo Mungu mwenyewe alihubiri tangu zamani ya kwamba atakuwa mchungaji wake (taz. Isa 40:11; Eze 34:11nk). Kondoo wake, ijapokuwa wanachungwa na wanadamu, huongozwa na kulishwa na Kristo mwenyewe aliye Mchungaji mwema na Mkuu wa wachungaji (taz. Yn 10:11; 1Pet 5:4), ambaye aliutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo (taz. Yn 10:11-15). Kanisa ni ardhi iliyolimwa, ni shamba la Mungu (taz. 1Kor 3:9). Katika shamba hilo mzeituni ule wa zamani hukua, ambao shina lake takatifu ni Mababu, na ndani yake upatanisho wa Wayahudi na wa Mataifa umeletwa na utaendelea kuletwa (taz. Rum 11:13-26). Mzeituni huu ulipandwa na Mkulima wa mbinguni kama shamba la mizabibu lililoteuliwa (taz. Mt 21:33-43//; Isa 5:1nk). Kristo ndiye mzabibu wa kweli anayeyajalia matawi, yaani sisi, uhai na uwezo wa kuzaa; nasi, kwa njia ya Kanisa, twakaa ndani yake, na pasipo yeye hatuwezi kufanya neno lolote (taz. Yn 15:1-5). Rej Lumen gentium, 6.
Kristo Yesu ndiye mzabibu wa kweli na waamini ni matawi yake na Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma ndiye mkulima anayeifanya kazi hii kwa uvumilivu mkubwa, changamoto na mwaliko kwa waamini kukaa ndani mwake ili wapate kuzaa matunda. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Marko wakati wa hija yake ya kichungaji mjini Venezia, Dominika tarehe 28 Aprili 2024. Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia inanogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Kristo Yesu wakati wa karamu ya mwisho alikazia sana umuhimu wa wafuasi wake kubaki wakiwa wameungana naye, maneno yanayopata chimbuko lake katika Sala na Zaburi, kwa kutambua kwamba, shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe aliona dhuluma, alitamani kuona haki, na kumbe alisikia kilio. Is 5:7. Kristo Yesu katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 21: 33-44 anazungumzia kuhusu vibarua waovu, kwa kuonesha kazi na uvumilivu mkubwa ulioneshwa na Mwenyezi Mungu na jinsi ambayo watu wake walivyomkataa. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa huduma ya upendo wa Mungu kwa binadamu, muungano wa dhati na waamini ili wapate kuzaa matunda, vinginevyo watanyauka na hatimaye kukatwa na kutupwa nje.
Mji wa Venezia anasema Baba Mtakatifu Francisko una historia ndefu ya kilimo cha mizabibu, uzalishaji wa divai, utunzaji bora wa mashamba ya mizabibu bila kusahau mchango wa Wamonaki katika mchakato wa uzalishaji wa divai kwa ajili ya jumuiya zao. Ujumbe muhimu katika simulizi hili ni imani kwa Kristo Yesu ni mwaliko kwa waamini kuupokea upendo wa Mungu unaozalisha furaha, kwani Mwenyezi Mungu anawahudumia waja wake na kuwawezesha kuzaa matunda hata kama udongo wa maisha ya waamini tayari ulikwisha choka na kwamba, Mungu anathamini sana uhuru wa watoto wake. Venezia ni mji uliojengwa juu ya bahari na hivyo unahitaji sana utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Na waamini, daima wakiwa wamezamishwa kwenye Maji ya Ubatizo, wanazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kufanywa kuwa ni sehemu ya Kristo Yesu, Mzabibu wa kweli, ili kupata maisha na uzima wa milele. Kwa hakika, waamini wakibaki wameungana na Kristo Yesu watakuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wake na hivyo wataweza kuzaa zabibu bora inayozalisha divai ya upendo wa Mungu inayoujaza moyo wa mwanadamu furaha na matumaini. Matunda ya muungano huu na Kristo Yesu yanapaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya waamini.
Uzuri wa mji wa Venezia unatishiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kuongezeka kwa kina cha maji, hali inayohatarisha miundombinu, amana na urithi wa kitamaduni, maisha ya watu, shughuli za kitalii na matokeo yake kunaweza kuibuka mahusiano tenge ya kijamii, uchoyo, ubinafsi na upweke hasi. Waamini wanapaswa kuwa ni matawi yaliyoungana na Mzabibu wa kweli ambao ni Kristo Yesu katika Shamba la Mzazibu ambalo Mwenyezi Mungu ndiye mkulima ili kuzaa matunda ya: haki na amani, mshikamano na upendo; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, urafiki na mafungamano ya kijamii katika medani mbalimbali za maisha, ili kweli familia, jumuiya na miji iweze kuwa ni mahali pa ukarimu na ushirika. Mji wa Venezia unasifika kuwa ni mji unaowakutanisha watu na mahali pa kubadilishana tamaduni. Huu ni mwaliko kwa mji wa Venezia kuwa ni alama ya uzuri unaofikiwa na wengi, kwa kuanzia maskini na wanyonge katika jamii; alama ya udugu wa kibinadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maonesho ya kisanii ya “Biennale” mkusanyiko wa Sanaa mbalimbali, ni sawa na Injili ya Kkristo Yesu, chimbuko la furaha ya kweli, chachu ya mabadiliko katika maisha, iwakirimie matunda ya upendo na furaha ya kweli.
Naye Patriaki Francesco Moraglia wa Venezia, mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Marko, mjini Venezia, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu, kwa kuwakirimia siku iliyosheheni matumaini na mapendo, kiasi cha kujisikia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kweli ni Baba na Kiongozi, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu Venezia chini ya ulinzi na maombezi ya Mtakatifu Marko, wanapenda kuendelea wakiwa wameungana na Kristo Yesu, Mzabibu wa kweli. Wenyeji wa Venezia licha ya kuwa ni: wachapakazi, waaminifu na wakarimu, lakini kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi wanalazimika kuukimbia mji wao, na kuanza kuonja ile adha ya kuishi ughaibuni; wanakabiliana na utamaduni wa kifo, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai inayopaswa kupendwa, kulindwa na kupokelewa. Ni katika muktadha huu Jimbo kuu la Venezia limeanzisha nyumba ya upendo ya Mtakatifu Yosefu. Wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuhamasisha amani ulimwenguni kote.