Liturujia Neno la Mungu Dominika 5 ya Mwaka B: Nguvu ya Sala Katika Huduma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tano ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tarehe 4 Februari 2024 inamwonesha Kristo Yesu akidhihirisha uweza wake wa kuponya katika Sinagogi, anamponya pia mkwewe Petro aliyekuwa kitandani hawezi homa na aliwaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Kristo Yesu akatoka Kapernaumu akaenda akihubiri katika Masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya. Hii ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kristo Yesu kwani inazungumzia juu ya umuhimu wa Mungu pamoja na kutoa maswali juu ya imani ya Kanisa. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya tano ya Mwaka B wa Kanisa wakati wa tafakari kwenye Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Kristo Yesu alitoka ili kuwaendea binadamu waliojeruhiwa, ili kuwafunulia Uso wa Baba wa milele. Pengine katika sakafu ya nyoyo za waamini bado wanayo dhana ya Mungu ambaye yuko mbali sana na waja wake; Mungu ambaye ni mgumu wala hajiangaishi na matatizo yanayomkumba binadamu. Lakini, Injili inawafunulia waamini kwamba, Kristo Yesu baada ya kuwa amewafundisha watu kule kwenye Sinagogi, anatoka ili Neno alilolitangaza na kulishuhudia liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, na hatimaye, watu waweze kuona na kumshuhudia, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anayejishusha ili kuwaendelea waja wake, kuwatembelea katika makazi yao, kwani anapenda kuwaganga na kuwaponya na magonjwa pamoja na udhaifu wao wa kiroho na kimwili. Baada ya kushughuli zote hizi, Kristo Yesu, aliondoka na kwenda kusali, ili kuwabeba wote katika moyo wa Baba yake wa mbinguni. Sala inamkirimia tena nguvu ya kurejea tena ili kuwahudumia ndugu zake.
Baba Mtakatifu anawauliza waamini Je, katika safari yao ya imani, wamewahi kugundua kwamba, Kristo Yesu ni ndiye ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba, au bado wamebaki na mawazo mgando kuhusu Mwenyezi Mungu kwamba, yuko mbali na waja wake. Je, imani inawafanya waamini kuwa na wasi wasi au inawaachia faraja na utulivu wa ndani? Je, wanaposali wanahisi imani, au Neno la Mungu linawasukuma kutoka ili kwendaa kukutana na wengine, tayari kueneza faraja ya Mungu? Changamoto kubwa ya maisha ya kiroho ni kuachana na Mungu wanaye fikiri kwamba, wanamjua na hivyo kumgeukia kila siku, Mungu ambaye kila siku Kristo Yesu anawaletea katika Injili kama ufunuo wa Baba wa huruma na upendo, ili kukomaza imani na kamwe wasibaki kuwa ni Wakristo wa Sebuleni” bali wawe ni vyombo na mashuhuda wa tumaini la Mungu na uponyaji wake. Bikira Maria Mtakatifu sana, Mwanamke anayesafiri, awasaidie waamini kutoka katika ubinafsi wao ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu.