Jangwani Ni Mahali pa Mapambano ya Maisha ya Kiroho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru: Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” Kut 20:2. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia zaidi wito wa ukombozi kutoka utumwani, ili kukutana na Mungu, huku wakiacha nyuma yao kongwa la utumwa, mwaliko kwa Kipindi hiki cha Kwaresima kufungua macho yao ili kujionea hali halisi. Katika safari ya kutoka utumwani, ni Mwenyezi Mungu anayeona, ongoza na kuwakirimia waja wake uhuru kamili. Kwaresima ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Mungu, toba, wongofu wa ndani sanjari na kuambata uhuru na kwamba, haya ni mapambano ya jangwa la maisha ya kiroho. Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa inamwonesha Kristo Yesu akishawishiwa jangwani. “Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na Malaika walikuwa wakimhudumia.” Mk 1:12-13. Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha. Kule jangwani, Kristo Yesu alikuwa pamoja na wanyama, na malaika walikuwa wakimhudumia. Wanyama na Malaika ni lugha ya picha na kwamba, wanyama na malaika ni wandani wa safari ya maisha ya kiroho na kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa mwamini kukutana na wanyama pamoja na Malaika.
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 18 Februari 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika kufafanua maana ya “wanyama pori katika maisha ya kiroho pamoja na Malaika ambao kimsingi ni wajumbe wa Mungu wanaowasaidia waamini kutenda mema na kwamba, dhamana na wajibu wao msingi ni huduma! Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Wanyama wa porini katika maisha ya kiroho” wanaweza kufikiriwa kuwa ni tamaa mbaya ambayo hugawanya nyoyo za watu na kujaribu kutaka kuimiliki. Hawa ni washawishi wakuu na kwamba, waamini wasipokuwa makini kuna hatari ya kuweza kuraruriwa vipande vipande! Wanyama hawa wa maisha ya kiroho ni maovu mbalimbali yanayotendeka; uchu wa mali na madaraka; hali ya kutoridhika, raha na starehe kupita kiasi; ukosefu wa amani na utulivu wa ndani; upweke hasi; ubinafsi, uchoyo na umaarufu ambao huleta ukosefu wa usalama. Hawa ni wanyama mwitu kumbe wanahitaji kufugwa na kupigwa vita, vinginevyo watakula uhuru wa waamini. Jangwa ni mahali pa kuona uwepo wao, ili kuweza kukabiliana nao kikamilifu. Kwaresima ni kipindi muafaka cha kwenda jangwani, ili kukoleza mapambano ya maisha ya kiroho.
Baba Mtakatifu anasema Malaika ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu wanaowasaidia wamini kutenda mema na kimsingi, kulingana na Injili wao ni wahudumu, kinyume kabisa cha milki kama ilivyo kwa “Wanyama porini”. Roho za Malaika hukumbuka mawazo na hisia nzuri na zinazopendekezwa na Roho Mtakatifu. Wakati wa majaribu, wanawasaidia waamini kuwatenga na maovu na kuwaelekeza katika maongozi mema ya Kimungu katika muktadha wa upatanisho. Maongozi yao mema ni kitulizo cha roho za waamini na hivyo kutia “ladha ya mbinguni.” Husaidia sana kurejesha amani na utulivu wa nafsi bila kujali hali ya maisha ya mwamini, iwe ni nzuri au hata kinyume chake. Jambo la msingi ni kutambua hisia za Mungu, kumbe, waamini wanahitaji kukaa kimya na kujikita katika maisha ya sala. Kwaresima ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika maisha ya sala! Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanzoni kabisa mwa Kipindi cha Kwaresima, waamini wanapaswa kujiuliza maswali msingi, Je, ni hisia za wanyama wa porini wanaochochea hisia zao? Ni vyema kuwatambua wanyama wa porini kwa kutambua na kuwapatia majina halisi sanjari na kujitahidi kuelewa mbinu zao. Jambo la pili ni kuhusu sauti ya Mungu, yaani dhamiri nyofu. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuulinda na kuutunza moyo wake kwa kujikita katika wema, kwa kukuza maisha ya sala, katika kuabudu, kutukuza na kushukuru sanjari na tafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha. Bikira Maria Mama wa Mungu alilishika Neno la Mungu, wala hakujiruhusu kuguswa na majaribu ya Shetani, Ibilisi na Mwovu, awasaidie katika safari hii ya maisha ya kiroho kuelekea jangwani.