Dominika ya V ya Neno la Mungu: Wito wa Kutangaza na Kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Dominika ya Tano ya Neno la Mungu, tarehe 21 Januari 2024 ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika maisha halisi. Itakumbukwa kwamba Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27. Na Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Dominika ya V ya Neno la Mungu, amezama zaidi katika wito wa Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu, mwaliko kwa wafuasi wake, kushiriki kikamilifu katika kutangaza Injili ya matumaini na wokovu wa mwanadamu, inayowakirimia watu wa Mungu furaha ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa! Injili kama ilivyoandikwa na Marko 1: 14-20 ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuitikia wito, kuacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu, tayari kushiriki katika maisha na utume wake. Huu ni wito shirikishi katika kazi ya ukombozi na anawataka wafuasi wake kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwa kuwajibika na kuwa ni wadau wakuu!
Kristo Yesu anafahamu fika uwezo na udhaifu wa wafuasi wake, lakini bado anatumia muda wake kuwaonesha upendo na uvumilivu na hata wakati mwingine, walishindwa kuyafahamu na kuyaelewa maneno yake, kwa mfano pale Wasamaria walipokataa kumpokea, wanafunzi wake Yakobo na Yohane wakataka aagize moto ushuke kutoka mbinguni ili uwaangamize, lakini Kristo Yesu akawajibu kwamba, Mwana wa Adamu hakuja kuziangamisha roho za watu, bali kuziokoa! Rej. Lk 9:51-56. Lakini hata wakati mwingine, Mitume walipishana wao kwa wao na hata wakati mwingine, iliwawia vigumu kung’amua mambo msingi katika mahubiri yake, kama huduma kwa watu wa Mungu. Pamoja na mambo yote haya, Kristo Yesu aliwachagua kuwa Mitume wake, na akaendelea kuwaamini, ili washiriki kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, ili mwisho wa siku wote waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote ni kati ya mambo yaliyoonesha furaha kubwa ya Kristo Yesu, kielelezo cha uwepo kati pamoja na waja wake na jibu lake makini la upendo wa Mungu kati ya wanadamu na kwamba, kila neno na tendo la Kristo Yesu linawaunganisha na Kristo Yesu mwenyewe, tayari kushirikisha upendo, mwanga na furaha, kwa wale wanaowazunguka, lakini furaha inayokita mizizi yake katika maisha na utume wao pia! Kwa jinsi hii, wafuasi wa Kristo Yesu, wanakuwa wakamilifu kwa kile ambacho wameumbwa kwa ajili yake yaani: watu wenye mioyo iliyo wazi, wenye mwelekeo chanya, wenye hekima na utulivu wa ndani; watu wenye shauku ya kupenda kama Mwenyezi Mungu apendavyo na hivyo kuleta tumaini la wokovu kwa watu wote.
Kwa hiyo, kutangaza na kushuhudia Injili si kupoteza wakati: ni kuwa na furaha zaidi kwa kuwasaidia wengine wawe na furaha; ni kujiweka huru na hivyo kuwasaidia wengine wawe huru zaidi; wito na mwaliko wa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kila mwamini amepokea wito wa uinjilishaji unaopaswa kutekelezwa na kila mtu katika: uwezo na hali ya maisha yake; uinjilishaji ufanywe kati ya marafiki, maeneo ya kazi, kwa makundi ya watu pamoja na majirani wanaoishi nao! Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake kwa kuwataka waamini kuchunguza ndani mwao, kama kweli wanatulia na kukumbuka furaha ya kumtambua na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao! Je, wanao moyo wa shukrani kwa kukubali wito wa kumfahamu na kumshuhudia Kristo Yesu, ili kuwafurahisha wengine? Je, wanajibidiisha kuwafanya watu wengine kwa njia ya ushuhuda wake wa maisha, waonje furaha na jinsi inavyopendeza kumpenda Kristo Yesu. Bikira Maria awasaidie Wakristo kuonja tena ile furaha ya Injili.