Tafuta

Katekesi Kuhusu Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Ulafi wa Chakula!

Kristo Yesu anakazia usafi wa moyoni na mahusiano kati ya mtu na chakula, changamoto na mwaliko wa kugundua tena umuhimu wa mahusiano haya hasa katika jamii zinazojiweza ambazo zimedhihirisha ukosefu wa uwiano wa matumizi ya chakula pamoja na hivyo kusababisha magonjwa ambayo kwa sasa yanaanza kuenea kwa kasi kubwa. Magonjwa haya ni pamoja na: Kutokuwa na hamu ya chakula “Anorexia”, “Bulimia nervosa” pamoja na uzito wa kupindukia "Obesity."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.  “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Katekesi ya Kuhusu: Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Ulafi
Katekesi ya Kuhusu: Fadhila na Mizizi ya Dhambi: Ulafi

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Katika katekesi yake amekazia kuhusu dhambi na vishawishi vya dhambi, usithubutu kamwe kufanya majadiliano na Shetani, Ibilisi na kwamba, kila mwamini anapaswa kuulinda moyo wake, lakini Waswahili wanachakarika kuumwagilia moyo! Papa amekwisha kugusia kuhusu mizizi ya dhambi na fadhila mintarafu mapambano ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Januari 2024 amejielekeza zaidi katika uroho/Ulafi kama mzizi wa dhambi. Tafakari hii imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu kuhusu maonyo ya kibaba yanayosimikwa katika hekima: “Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi, utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa… Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa, kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.” Mit 23:15. 20-21. Katika Injili, ishara ya kwanza kutendwa na Kristo Yesu ni kugeuza maji kuwa divai kwenye harusi ya Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake na kuwarejeshea furaha wale wanandoa waliokuwa wametindikiwa na divai. Mtindo wa maisha ya Kristo Yesu ulikuwa ni tofauti sana na wa Yohane Mbatizaji ambaye maisha yake yalikuwa kwa kiasi kikubwa jangwani. Kristo Yesu alikaa na watu mezani, akala na kunywa pamoja nao, hali ambayo kwa Mafarisayo ilionekana kama kikwazo, lakini hii ilikuwa ni namna yake ya kujenga ushirika na wale waliokuwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Ulafi kama mzizi wa dhambi!
Ulafi kama mzizi wa dhambi!

Katika maisha na utume wake, Kristo Yesu alijiweka chini ya sheria, lakini wakati mwingine aliwadhihirishia kwamba, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Mk 2: 23-28. Na kwamba uwepo wa Kristo Yesu kati ya waja wake ni ishara ya furaha. Huu ni mwaliko pia wa kushiriki katika mateso yake, yanayojidhihirisha miongoni mwa maskini na watoto wadogo. Kuhusu majadiliano kati ya Kristo Yesu na Mafarisayo alionesha msimamo wake kuhusu chakula akisema kwamba, “kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.” Mk 7:19. Kristo Yesu anakazia usafi moyoni na mahusiano kati ya mtu na chakula, changamoto na mwaliko wa kugundua tena umuhimu wa mahusiano haya hasa katika jamii zinazojiweza ambazo zimedhihirisha ukosefu wa uwiano wa matumizi ya chakula na hivyo kusababisha magonjwa ambayo kwa sasa yanaanza kuenea kwa kasi kubwa. Magonjwa haya ni pamoja na: Kutokuwa na hamu ya chakula “Anorexia”, “Bulimia nervosa” ni ugonjwa wa kula ambao kwa kawaida unahusisha kula kupita kiasi na kufuatiwa na kusafisha. Kusafisha kunamaanisha kuondoa mwili wako kutoka kwa chakula ulichomeza kupitia kutapika au kuhara. Mtu anayefanya bulimia hasafishi. Badala yake hufanya mazoezi kupita kiasi ili kuchoma mafuta na kalori; Unene wa kupindukia, “Obesity.” Yote haya ni magonjwa yenye uhusiano tenge na chakula na kwamba, wanasaikolojia wanajaribu kutafuta suluhu ya magonjwa haya yenye athari zake kiroho na kimwili. Kumbe, uhusiano kati ya chakula na binadamu ndicho kitu ambacho kinapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa; kwa kujenga uwezo wa kushukuru kwa chakula unachopata, au kujenga kiburi; au ubinafsi kwa kujikusanyia chakula. Chakula anachokula mtu kinaweza kuonesha hali yake ya moyo! “Gastrimargia” kama Mababa wa Kanisa walivyouita ugonjwa huu ni hali ya kutafuta raha ya chakula ambayo ni hamu ya kula kwa raha kupita kiasi, hali ambayo inaendelea kusababisha madhara makubwa katika ulimwengu mamboleo, kwa kumfanya mwanadamu kuwa kama mmliki wa ulimwengu na kusahau kwamba, binadamu alikabidhiwa na Mwenyezi Mungu kulinda na kutunza kazi ya Uumbaji.

Mwanadamu amekabidhiwa kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji
Mwanadamu amekabidhiwa kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji

Kumbe, dhambi kubwa kwa sasa ni ulafi wa kupindukia na kusahau kwamba, waamini wanapaswa kuwa ni watu wa Ekaristi, Mkate unaomegwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao; kuwa ni watu wa shukrani na watumiaji bora wa ardhi. Lakini kwa bahati mbaya mwanadamu amegeuka na kuwa ni “mlafi” na mtumiaji mbaya wa kazi ya uumbaji na matokeo yake ni madhara makubwa kwa binadamu na mazingira wanamoishi. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoa nafasi kwa Injili ili iweze kuwaponya kama mtu binafsi na jamii katika ujumla wake.   Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na mahujaji kwa lugha mbalimbali amewakumbusha kwamba, Kristo Yesu amejifanya kuwa chakula chao kilichoshuka kutoka mbinguni, kumbe anawakirimia nguvu na ujasiri wa kusonga mbele katika fadhila ili kuweza kufanana naye! Bikira Maria awe ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa waamini wote. Amewataka wakristo kuwa waaminifu kwa wito wao kwa maana wote waliobatizwa katika Kristo, wamemvaa Kristo Yesu, kumbe wanapaswa kuishi katika upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. Gal 3: 27; 5:222. Amewataka vijana wa kizazi kipya, wagonjwa, wazee na wanandoa wapya kuenenda katika upya wa maisha yanayooneshwa na Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya waja wake, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu anawaalika pia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuwaombea watu wa Mungu sehemu mbalimbali za duniawanaoteseka kwa vita ili Mwenyezi Mungu aweze kupandikiza katika nyoyo za viongozi wao mbegu ya amani.

Katekesi Ulafi
10 January 2024, 14:25

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >