Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa Novemba 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 8 Novemba 2023 linaadhimisha Mkutano Mkuu unaojadili pamoja na mambo mengine: Tathmini ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39 mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam; Vijana na Mabadiliko ya Tabianchi Kijamii; Nyanyaso za Kijinsia ndani ya Kanisa Katoliki nchini Ufaransa na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa ni mahali pa salama kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto na vijana sanjari na Kanisa kujenga mazingira ya kuwapokea na kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu Katoliki Ufaransa wanajadili pia kuhusu: Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyonogeshwa kwa kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa katika awamu kuu mbili.
Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Hii ni fursa pia kwa Kanisa nchini Ufaransa kufanya marekebisho makubwa katika miundo mbinu yake sanjari na Katiba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa. Maaskofu Katoliki Ufaransa wanatambua kwamba, michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu Francisko anasema michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa iliuchagua mji mkuu wa Ufaransa, Paris, kuwa mwenyeji wa michuano ya Olimpiki mwaka 2024, na kuutunuku mji wa Los Angeles nchini Marekani kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa mwaka 2028.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu nchini Ufaransa, kuonesha moyo wa ukarimu, upendo na wajibu mkuu kwa kuwakaribisha wanamichezo kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Ufaransa kutumia fursa hii kuwa ni tukio la kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni na dini mbalimbali. Hii ni changamoto ya kujenga moyo wazi na wakujitolea, tayari kutumia: Makanisa, Shule na Nyumba zao kama kielelezo cha upendo, ukarimu na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo, chemchemi ya furaha ya kweli. Iwe ni fursa ya kujenga mshikamano na maskini, walemavu na wale wote wanaobaguliwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Michezo ya Olimpiki iwe ni fursa ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaohitajiwa sana katika nyakati hizi. Tangu wakati huu, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za Kitume kwa waandaaji na watu wote wa kujitolea bila kuwasahau wote watakaoshiriki katika mashindano haya kwa mwaka 2024. Ikumbukwe kwamba, michezo ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Katika vita inayoendelea kati ya Israel na Palestina kumezuka pia chuki dhidi ya Wayahudi, jambo ambalo si la “kupigia debe” hata kidogo. Chuki dhidi ya Wayahudi ilipamba moto wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kiasi cha Wayahudi millioni 6 waliuwawa kikatili, lakini hata leo hii bado watu wanaendekeza vita tu! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mateka na wafungwa wa vita wanaachiliwa bila masharti.
Mashambulizi Ukanda wa Gaza yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kumbe kuna haja ya kusitisha vita na kuanza kujielekeza kwenye majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu wa maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Éric Marie de Moulins d’Amieu de Beaufort, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo na ushirika wake, kwa sala na katika mchakato wa kuendelea kukuza na kudumisha huduma ya kimisionari kwa watu watakatifu wa Mungu nchini Ufaransa. Watambue kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko wa kutembea katika umoja pamoja na kuheshimu tofauti zao msingi. Baada ya kumsikiliza Roho Mtakatifu waache chumba cha juu kikiwaka moto wa Roho Mtakatifu, kwa kuwatangazia na kuwashuhudi watu waMungu ile furaha ya Injili, huku wakiendelea kumkazia macho Kristo Yesu. Baba Mtakatifu bado anakumbuka kwa furaha kabisa hija yake ya kitume huko Marseille ambako aliweza kuonja nguvu ya Kanisa nchini Ufaransa, changamoto na mwaliko kwa Maaskofu kuendelea kujifunza kutoka katika Mediterania masomo yenye kuvutia, lakini sehemu kubwa sana ni masomo yanayokatisha tamaa na kuvunja mioyo ya watu. Watu wa Mungu nchini Ufaransa waendelee kujikita katika Amri ya upendo na mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kusaidia kulinda na kutetea maisha ya binadamu na chachu ya amani ulimwenguni mwote. Kanisa la Ufaransa limebahatika kupata Makardinali wawili waliosimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu katika waraka wake wa “Njia ndogo ya tumaini na upendo” anawahimiza Wakristo kuamini katika upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo sanjari na kujipatia uzoefu wa kukutana na Kristo Yesu kwa uwazi kwa njia ya mbalimbali. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki Ufaransa kujenga na kudumisha ujasiri na kamwe wasikatishwe tamaa kutokana na matatizo na changamoto mbalimbali wanaokabiliana nazo katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa nchini Ufaransa liendelee kubaki kuwa ni Kanisa la kinabii. Maaskofu waendelee kupyaisha nyoyo za Mapadre waliojaribiwa, kuteseka na hatimaye kuvunjika moyo, kuwarudishia tena furaha ya imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Lourdes na waendeleze karama za Roho Mtakatifu kwa ajili ya utekelezaji wa huduma kwa watu wa Mungu nchini Ufaransa.