Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Maaskofu kwa kufanikisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Maaskofu kwa kufanikisha tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Papa Francisko Awashukuru Wajumbe wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi za Maaskofu

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wawezeshaji wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Sinodi waliojisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanafanikiwa. Amemshukuru Padre Davide Piras aliyewaandalia Mababa wa Sinodi Andiko la Mtakatifu Basil. Amewataka Mababa wa Sinodi kuendelea kulitafakari Andiko hilo, kwani ni msaada mkubwa katika maisha na utume wao katika mapambazuko ya millenia ya tatu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita zaidi katika: Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma. Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Shukrani kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Sinodi za Maaskofu
Shukrani kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Sinodi za Maaskofu

Hii ndiyo njia hasa ya Sinodi ambayo Mwenyezi Mungu anaitarajia kutoka kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kristo Yesu ndiye tumaini la pekee kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 amehitimisha rasmi maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Jumamosi tarehe 28 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu amewakumbusha Mababa wa Sinodi kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Kwa kutumia njia ya mawasiliano katika Roho, wameshirikishana kwa unyenyekevu utajiri na umaskini wa jamii zao kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakitaka kuvumbua Roho Mtakatifu anataka kusema nini kwa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.

Papa Francisko amewashukuru Mababa wote wa Sinodi kwa ushiriki wao
Papa Francisko amewashukuru Mababa wote wa Sinodi kwa ushiriki wao

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wawezeshaji wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Sinodi waliojisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanafanikiwa. Amemshukuru Padre Davide Piras aliyewaandalia Mababa wa Sinodi Andiko la Mtakatifu Basil. Amewataka Mababa wa Sinodi kuendelea kulitafakari Andiko hilo, kwani ni msaada mkubwa katika maisha na utume wao. Amewashukuru: Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu pamoja na Kardinali Jean-Claude Holleric, Mwezeshaji mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu hawa ni watu waliokuwa mstari wa mbele katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Sr. Nathalie Becquart, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu; Askofu Luis Marín de San Martín, O.S.A. Katibu mkuu msaidizi. Wengine ni pamoja na Padre Giacomo Costa, Padre Riccardo Battocchio, Giuseppe Bonfrate. Lakini Sr. Maria Grazia Angelini pamoja na Padre Timothy Radcliffe wameendesha mafungo ya kiroho kwa Mababa wa Sinodi pamoja na kutoa tafakari za maisha ya kiroho kama sehemu ya ujenzi wa mawasiliano katika Roho. Baba Mtakatifu Francisko ametambua pia mchango mkubwa uliotolewa na watu “waliofichwa nyuma ya pazia”, wote wamejisadaka ili kufanikisha maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Wote hawa Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika sakafu ya moyo wake amewashukuru wote.

Sinodi Shukrani
29 October 2023, 14:37