Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 700 waliuawa katika mapigano nchini DRC
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kulingana na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, anabainisha kuwa watu 2,800 wamejeruhiwa, huku waasi wa M23 - wakiungwa mkono na Rwanda - wakiuteka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Msemaji wa Umoja wa Mataifa alionya kwamba idadi ya vifo itaongezeka zaidi, akiongeza takwimu za majeruhi zilitokana na tathmini iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani na washirika wake. Mzozo wa mashariki mwa DR Congo ulianza miaka ya 1990 lakini umeongezeka kwa kasi tangu mwanzoni mwa mwaka huu. M23, ambayo inaundwa na kabila la Watutsi, inasisitiza kuwa inapigania haki za waliowachache, wakati serikali ya DR Congo inasema waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wanajaribu kudhibiti eneo hilo la utajiri wa madini. Kwa hiyo Mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaendelea kuongezeka kwa raia ambao wamenaswa na mapigano makali.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, hali inazidi kuwa mbaya zaidi huku watu wakikosa chakula na vifaa vingine. Wafanyakazi muhimu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada na washirika wake wamesalia chini mashariki mwa DR Congo, lakini hali bado si shwari tangu kundi hilo la waasi kuchukua udhibiti wa maeneo mengi ya Goma tangu kuingia katika mji huo siku ya Jumatatu 27 Januari.
Jean-Pierre Lacroix, wasiwasi wa UN
Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Operesheni za Ulinzi wa Amani Jean-Pierre Lacroix amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kidiplomasia ili kumaliza mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuzuia uwezekano wa mzozo huo kusambaa zaidi. Bwana Lacroix aliyasema hayo Ijumaa tarehe 31 Januari 2025 , akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kufuatia ziara yake huko Damascus, Siria wakati huu ambapo kundi la waasi wa M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) wakiendelea na harakati zao kuelekea mji wa Bukavu, jimboni Kivu Kusini, baada ya kuchukua udhibiti wa Goma, mji mkuu wa jimbo Kivu Kaskazini, mapema Juma hili.
“Tuna wasiwasi sio tu kuhusu hali ya mashariki mwa DRC, bali pia, tukizingatia historia, hali hii imekuwa na uwezekano wa kusababisha mzozo mpana wa kikanda,” amesema Lacroix, akiongeza kuwa, “hivyo basi, ni muhimu sana kwamba juhudi zote za kidiplomasia zielekezwe katika kuzuia hali hii na kuleta kusitishwa kwa mapigano.” Kauli ya Lacroix ilikuja wakati inaelezwa kuwa M23 wako takriban kilomita 60 kaskazini mwa Bukavu na “wanaonekana kusonga kwa kasi kubwa.” Alitoa taarifa kuhusu hali ya Goma, ambako hali inaendelea kuwa ya wasiwasi na tete, ingawa utulivu umeanza kurejea taratibu. Maji na umeme vimeanza kurejea, ingawa mabaki ya vilipuzi visivyolipuliwa yanaendelea kuwa “kikwazo kikubwa kwa uhuru wa watu kutembea na kusafiri.
Umoja wa Mataifa una ujumbe wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, na baadhi ya kambi zake zimepokea tena vifaa muhimu, jambo ambalo amesema ni la msingi kwani “idadi kubwa” ya watu pia wanatafuta hifadhi katika maeneo haya. “Kipaumbele cha ujumbe huu kimeendelea kuwa ulinzi wa wafanyakazi wake, mali zake, na, bila shaka, raia wengi wanaotafuta hifadhi ndani ya vituo vyake; raia pamoja na wapiganaji waliosalimisha silaha. Wote wanalindwa na MONUSCO kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu,” alisema Lacroix. Aidha aliripoti kuwa maeneo hayo ya hifadhi yamekuwa katika shinikizo kubwa katika utoaji wa maji ya kunywa, huduma za usafi, na msaada mwingine kwa wale waliomo ndani.
Wakati huohuo, uongozi wa MONUSCO umeongeza mazungumzo ya kisiasa na serikali ya DRC ambapo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na mkuu wa ujumbe huo, Bintou Keita, amefanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu, akiwemo Waziri Mkuu na viongozi wa jeshi na polisi. Kikundi cha pamoja cha serikali na MONUSCO kimeanzishwa ili kuratibu masuala mbalimbali, yakiwemo yale ya usalama, haki za binadamu, masuala ya kibinadamu na mawasiliano, pamoja na hadhi ya kisheria ya maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23 na jeshi la Rwanda, RDF. Bwana Lacroix alisisitiza juu ya "kuongezeka" kwa shughuli za kidiplomasia kusaka jawabu la mgogoro huu, ikiwemo mikutano miwili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, mwingine wa jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, na mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika.
Muungano wa Ulaya, pamoja na Uingereza, Marekani na wengineo, pia wamechangia juhudi hizi. "Hadi sasa, juhudi hizi hazijazaa matunda katika kusitisha mapigano," alibainisha, akisema kuwa "M23 na RDF kwa sasa wanaendelea kusonga kuelekea kusini, kuelekea Bukavu, jambo ambalo bila shaka linatia wasiwasi."