Tanzania:Mkutano kuhusu muafaka wa upatikanaji wa nishati barani Afrika!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Januari 2025 ameshiriki pamoja na wakuu wa nchi nyingine za Afrika katika majadiliano ya pamoja kwenye Mkutano kuhusu “Nishati barani Afrika" katika siku ya Pili ya mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia (27-28 Januari 2025).
Katika siku ya Kwanza ya Mkutano huo Jumatatu 27 Januari, mijadala ilihusisha Mawaziri wa mataifa mbalimbali, viongozi wa sekta binafsi, wadau wa masuala ya maendeleo ya nishati na fedha. Na kwa kuhitimisha Jumanne tarehe 28 januari na wakuu wa nchi kuwa sehemu ya mkutano huo.
Hata hivyo tarehe 28 Januari, wakuu nchi mbalimbali waliendelea kuwasili nchini Tanzania, asubuhi kwa ajili ya siku ya pili ya mkutano huo. Baadhi ya marais waliowasili ni pamoja na Rais wa Sierra Leone, Malawi, Somalia, Zambia, Ethiopia, Djibout, Madagascar, Mauritania, Gambia, Burundi, Congo,Comoros, Ghana, Botswana.
Wakati viongozi hao wakiendelea kuwasili katika jiji la Dar es Salaam, na hali ya usalama iliendelea kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji. Ikiwa ni pamoja na shughuli mbalimbali zilizositishwa zikiwemo za elimu mashuleni na huduma zingine za kiserikali huku watumishi wa umma wakitakiwa kufanya kazi wakiwa majumbani.
Jumatatu 27 Januari 2025, akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Doto Biteko alisema kuwa “baada ya kupata uhuru mwaka 1960, nchi za Afrika zilipiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao lakini bado kuna uhitaji mkubwa.” Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati wa nchi ya Tanzania alisema kuwa, "Idadi ya Waafrika ambao hawana umeme inakadiriwa kuwa milioni 571.” Kutokana na hali hii, “mkutano huu uliitishwa ukiwa na lengo kubwa lakini linaloweza kufikiwa la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa angalau watu milioni 300 barani Afrika katika miaka mitano ijayo, alisema."