Tanzania:Mkutano kuhusu nishati wafanyika Tanzania Januari 27-28!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hatimaye Wageni waliotarajiwa nchini Tanzania, wamefika na wanaendelea na Mkutano huo wa siku mbili Jijini Da Es Salaam katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo kutokana na taarifa za ndani zinabainisha kwamba mji wa Dar Es Salaam umetulia kwa mizunguko ya magari kwa sababu ya kuacha nafasi kwa ugeni huu, hasa maeneo ya katikati ya Jiji la Dar Ess Salaam kwa siku mbili hata shule kufungwa. Si kwa bahati mbaya hata hivyo Mkutano huo umefanyika katika Siku ya Kimataifa ya Nishati Safi inayoadhimishwa kila ifikapo Januari 27.
“Idadi ya Wakuu wa Nchi watakaoshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliopangwa kufanyika nchini 27 na 28, Januari 2025 ni rekodi nyingine” alikuwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maandalizi akitumia mitandao ya kijamii kutoa ujumbe kwa njia ya video.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kuwa Wakuu wa Nchi 25 na Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Naibu Mawaziri Wakuu 10 wanafanya idadi ya viongozi wa ngazi ya juu kuwa 35 ambao Tanzania tokea izaliwe haijawahi kupokea idadi kubwa ya viongozi kama hao katika tukio moja. “Tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999 na Wakuu wa Nchi 15 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, mkiangalia idadi ya Wakuu wa Nchi katika mkutano huu ni kubwa ukilinganisha na matukio hayo mawili yaliyopita,” Balozi Kombo alisema kabla ya tukio hilo. Alizitaja nchi ambazo Wakuu wa Nchi zao zimethibitisha kushiriki kuwa ni Pamoja na; Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.
Kwa njia hiyo Makamu wa Rais wanaoshiriki ni kutoka Gambia na Benin. Mawaziri Wakuu kutoka Ivory Cost, Uganda, São Tomé na Príncipe na Guenea ya Ikweta na Naibu Mawaziri Wakuu ni kutoka Eswatine na Namibia. Waziri Balozi Kombo aidha alisema kuwa “mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla.” Aliongeza kusema kuwa “mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil mnamo Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.”
Siku ya Kimataifa ya Nishati safi
Na katika atika Siku ya Kimataifa ya Nishati Safi inayoadhimishwa kila ifikapo Januari 27, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana António Guterres, alisisitiza hatua muhimu katika mwelekeo wa nishati duniani. Kwa mara ya kwanza, vyanzo vya nishati mbadala vinatarajiwa kuzidi vyote kuwa chanzo kikuu cha uzalishaji wa umeme duniani mwaka huu. Alisema hayo tarehe 26 Januari 2025 katika kuelekea kilele cha siku hiyo Bwana Guterres alisherehekea mafanikio haya, akieleza jinsi gharama za teknolojia mbadala zinavyoshuka kila siku. Hata hivyo, anatambua changamoto zilizopo, akihimiza hatua za haraka na za haki katika kuhamasisha mabadiliko kutoka kwa nishati ya mafuta kwenda kwa nishati safi. "Enzi ya mafuta ya kisukuku inaisha," Guterres alisema kupitia ujumbe wake mahususi kuhusu siku hii. "Lakini serikali lazima ziharakishe na kuhakikisha mabadiliko haya ni ya haki. Hii ni muhimu kuzuia athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha kila mtu anaunganishwa na nishati safi, hatua inayoinua mamilioni kutoka kwenye umasikini."
Katibu Mkuu alisisitiza kuwa mwaka huu unatoa fursa ya kipekee kwa mataifa kulinganisha malengo yao ya tabianchi na mikakati ya nishati na maendeleo. Alikumbusha serikali ahadi yao ya kuhuisha mipango ya kitaifa ya hatua za tabianchi ili kuzuia kupanda kwa joto duniani zaidi ya nyuzi joto 1.5 za Selsiasi. Bwana Guterres alihimiza mipango hii ijikite katika kupunguza gesi zote chafuzi, kupanga upunguzaji wa matumizi ya mafuta ya kisukuku kwa njia ya haki, na kusaidia lengo la kimataifa la kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala ifikapo 2030. Alitoa wito kwa mataifa ya G20, kama nguvu kubwa za kiuchumi na wachangiaji wakubwa wa hewa chafuzi, kuongoza juhudi hizi, akisisitiza kanuni ya "wajibu wa pamoja lakini tofauti." Katibu Mkuu pia alitaja changamoto za kifedha zinazozikumba nchi zinazoendelea katika kupitisha nishati mbadala. Alitoa wito wa ongezeko la mikopo kutoka kwa benki za maendeleo ya kimataifa, kupunguza gharama za mtaji, na kuchukua hatua madhubuti kuhusu deni. "Katika Siku ya Kimataifa ya Nishati Safi, tujitolee kwa enzi mpya ya kimataifa ya nishati safi yenye kasi, haki, na ushirikiano kama msingi wake," Bwana Guterres anahitimisha. Wito huu unasisitiza haja ya mshikamano wa kimataifa na hatua madhubuti ili kuhakikisha mustakabali endelevu na wa haki wa nishati kwa wote.