Afrika Kusini:Mkutano mkuu 15 wa BRICS na hoja ya kupanua wigo
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Miito ya kupanua ukubwa wa kundi la BRICS linaloundwa na mataifa ya China, Brazil, Urussi, India na Afrika Kusini, ndiyo ilitawala ajenda za mkutano mkuu wa 15. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 23 Agosti ni kwamba nchi 12 duniani zimeomba kujiunga na kundi la BRICS, ambalo hivi sasa linawakilisha nusu ya idadi ya watu duniani na robo ya thamani ya uchumi wa ulimwengu. Mkutano huo wa 15 wa BRICS ulianza tangu tarehe 22 Agosti na unamalizika 24 Agosto 2023 huko Johannesburg nchini Afrika Kusini. Mkutano huo umeudhuriwa na Wakuu wote wa serikali za nchi wanachama isipokuwa rais Vladimir Putin, wa Urussi ambaye hakuwepo kwa sababu ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Rais Xi Jinping wa China, Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi walihudhuria wenyewe mkutano huo.
Katika Mjadala wa tarehe 23 Agosti 2023 ulijikita na mada ni jinsi jumuiya hiyo inavyoweza kuwasajili wanachama wapya wakati huu ikijipambanuwa kama taasisi ya kiulimwengu mbali ya zile zinazodhibitiwa na mataifa ya Magharibi. China, ambayo ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye umoja huo, ilitaka kuandikisha wanachama wapya kuharakishwe wakati huu ushindani na Marekani ukizidi. Brazil na Afrika Kusini zinaunga mkono utanukaji huo, ambapo Rais Lula da Silva wa Brazil alisema yuko tayari kuipokea Argentina. Mataifa mengine yaliyo mbioni kujiunga ni Saudi Arabia, Algeria, Ethiopia na Iran. Asilimia 40 ya watu wote waliopo ulimwenguni wanaishi sasa kwenye mataifa matano waanzilishi wa BRICS, ambayo kwa pamoja yanahodhi robo nzima ya uchumi wa dunia. Katika maelezo yao yabanianisha wazi kuwa Afrika Kusini na China wana maoni yaliyo sawa ya kutaka kupanua BRICS.
Kwa hiyo Viongozi wa kundi la mataifa yanayoendelea kiuchumi la BRICS wamekubaliana kuongeza idadi ya wanachama na kuidhinisha masharti kwa nchi nyingine kujiunga na kundi hilo. Lengo lake la kutanua uwanachama ni kuiruhusu jumuiya hiyo kuyaleta pamoja mataifa yenye chumi kubwa ama ndogo, yenye serikali za kidemokrasia ama kidikteta ili kujenga chombo mbadala kinachofuata utaratibu tafauti wa kilimwengu na ule uliowekwa na kusimamiwa na mataifa ya Magharibi. Hapo awali tumesema kuwa Rais wa Urussi Vladimir Putin, hakuwepo kwa sababu ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Jinai lakini katika hotuba yake iliyorushwa kwa njia ya video katika ukumbi wa mikutano jijini Johannesburg, Putin aliwaalika wawakilishi wa mataifa mengine wanachama wa BRICS: Brazil, India, China na mwenyeji wakaribishwa kwa wakati huu, Afrika Kusini, kwenye mji wa Kazan mwezi Oktoba mwakani.
Ingawa tarehe maalum haijatajwa, Rais Putin alitangaza kwamba kutakuwa na matukio zaidi ya 200 ya kisiasa, kiuchumi na kijamii chini ya uwenyekiti wa nchi yake kwa BRICS mwaka ujao. Hati ya kumkamata Putin iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa shutuma za kuhusika na uhalifu nchini Ukraine inamaanisha kuwa kiongozi huyo angekabiliwa na uwezekano wa kukamatwa kama angelihudhuria mkutano nchini Afrika Kusini, kwani nchi hiyo ni mwanachama Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inayotumika kushitaki uhalifu ikiwamo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita. Ilianzishwa kuisaidia kazi mifumo ya kitaifa ya mahakama za nchi tofauti.