UN:Jukwaa la kudumu la watu wa asili ya Afrika kufanyika 30 Mei-2 Juni
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Jukwaa la pili la kudumu kuhusu watu wenye asili ya Afrika limezinduliwa tangu tarehe 30 Mei 2023 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani na litaendelea hadi tarehe 2 Juni 2023. Mada kuu zinazojadiliwa katika siku nne za jukwaa hilo zinajikita katika haki za binadamu zikimulika masuala ya haki ya upatanisho wa kimataifa, wa Waafrika kwa ajili ya utu, haki na amani, uhamiaji wa kimataifa, kutambua na kushughulikia ubaguzi wa kimfumo na kimuundo kwa kuzingatia takwimu na Ushahidi, na afya, ustawi, na kiwewe kilichodumu kati ya vizazi.” Lengo kuu la nada zinazojaliwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni kuchangia kwenye mchakato wa kutanabaisha uchagizaji wa azimio la Umoja wa Mataifa la kuchagiza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu za watu wenye asili ya Afrika.
Haki kwa watu wenye asili ya Afrika
Akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu wa jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema “Kuanzishwa kwa jukwaa hili na Baraza Kuu kulionyesha dhamira ya jumuiya ya kimataifa ya kuongeza kasi katika njia ya kuelekea usawa kamili na haki kwa watu wa asili ya Kiafrika kila mahali.” Ameongeza kuwa “Jumuiya ya asili ya Kiafrika ugahibuni imeongeza tija na kutajirisha jamii katika kila kona ya dunia na kuchangia pakubwa katika kila nyanja ya jitihada za binadamu. Na hicho ndicho tunasherehekea hapa leo.” Hata hivyo amesema pamoja na mchango wao mkubwa “Bado, tunafahamu kwa uchungu kwamba watu wenye asili ya Kiafrika wanaendelea kukabiliana na ubaguzi wa rangi uliokita mizizi na ubaguzi wa kimfumo. Karne nyingi za kivuli cha utumwa na unyonyaji wa kikoloni bado kinaharibu maisha yetu ya sasa.”
Wakati wa kurekebisha makosa ni sasa
Bwana Guterres amesisitiza kwamba “Wakati kutambua na kurekebisha makosa ya muda mrefu umepita. Ni lazima tuchukue hatua haraka zaidi sasa ili kuziondoa jamii zetu katika janga la ubaguzi wa rangi, na kuhakikisha ushirikishwaji kamili wa kisiasa, kiuchumi na kijamii wa watu wa asili ya Kiafrika kama raia sawa na wengine, bila ubaguzi.” Ameongezea kuwa na hilo ndilo lengo la Mpango Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Ubaguzi wa Rangi na Kukuza Utu kwa Wote. Amewashukuru aidha washiriki wa Jukwaa hilo kwa kujumuika pamoja ili kubadilishana mawazo na mikakati ya kusaidia ulimwengu kusonga mbele na kuachana na ubaguzi. Alihitimisha ujumbe wake kwa kusistiza kuwa: “Kwa pamoja, hebu hatimaye tutambue mustakabali wa utu, fursa, na haki kwa wote.”
Inahitajika mawazo na njia mpya za kuondokana na zama za ukoloni
Na wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema mawazo mapya na njia mpya za kuondokana na zama za ukoloni ni muhimu zaidi hivi sasa ili hatimaye kuweza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, (SDGs) katika maeneo 17 ambayo bado yanatawaliwa. Ni maneno yake aliyotoa kwa njia ya video kwenye semina ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuondokana na ukoloni, semina iliyofanyika mjini Bali, nchini Indonesia. Semina hiyo imefanyika sambamba na Juma la kuonesha mshikamano na watu na maeneo ambayo bado yanataliwa duniani inayomulikwa kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei ya kila mwaka!
Semina ya kikanda ya Kamati Maalum ya kuondokana na Ukoloni
“Lengo letu la pamoja ni kupatia kipaumbele kikubwa ajenda ya kuondokana na ukoloni na kuchochea kasi ya uchukuaji hatua,” amesema Guterres kwa wajumbe wa semina ya kikanda ya Kamati Maalum ya kuondokana na Ukoloni au C-24. Kamati hiyo ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1961, ikiwa na jukumu la kuchunguza maombi ya Azimio la kupatia uhuru nchi zinazotawaliwa pamoaj na watu wake. Tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945, zaidi ya makoloni 80 ya zamani yakiwa na jumla ya watu milioni 750 aymeshapata uhuru. Mchakato wa sasa unalenga maeneo 17 yasiyojitawala, yakiwa na watu tarkibani milioni mbili.
Kufikia maendeleo endelevu
Akimulika maudhui ya semina hiyo,ambayo inahamasisha Malengo ya Maendeleo Endelevu(SDGs) kwenye maeneo hayo, Katibu Mkuu amesema ikiwa imesalia nusu ya kufikia ukomo wa malengo hayo, “tunaacha nyumba zaidi ya nusu ya wakazi wa dunia.” “Maendeleo yamekwama, na katika maeneo mengine, maendeleo yamerudi nyumba,” ameonya Katibu Mkuu. Amesema kuwa SDGs ni njia ya amani na ustawi kwa wote kwenye sayari yenye afya; hakuna nchi inayoweza kukubali kuona malengo hayo yanashindikana.
Changamoto dhahiri
Hata hivyo Katibu Mkuu amesema kwa maeneo mengi ambayo bado yanatawaliwa, na ambayo ni nchi za visiwa vidogo vilivyo mstari wa mbele vikikumbana na dharura ya madhara ya tabianchi, hali ni dhahiri kabisa. “Kama jamii ya kimataifa, lazima tuhakikishe maeneo hayo yana rasilimali na msaada unaohitajika kupeleka mbele SDGs, kwa kujenga mafao na kuwekeza kwa ajili ya siku za usoni,” aliwaeleza wajumbe wa semina hiyo. Mchakato wa kutokomeza ukoloni lazima uongozwe na matamanio na mahitaji ya maeneo hayo kwa kuzingatia kila eneo lilivyo, amesema Katibu Mkuu akitoa shukrani zake kwa Kamati hiyo kwa kujizatiti kwake bila kuchoka kukamilisha utokomezaji wa ukoloni duniani.
Kubadili mwelekeo
“Nawategemea ninyi kuchochea mawazo mapya na kufungua njia mpya za ushirikiano thabiti kati ya maeneo, watawala na wadau wengine kwa mujibu wa maazimio husika" Aidha alisisitiza kuwa kwa pamoja wanaweza kubadili mwelekeo na kuchagiza njia mpya ya kufanikisha SDGs kwenye maeneo husika na kwingineko.