Sudan:moto ulihangamiza kiwanda cha kuzalisha vyakula vya tiba ya utapiamlo
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Licha ya juhudi za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ( UNICEF) za kujitolea, migogoro bado sana inaendelea kuwazuia watoto kupata matibabu; vile vile migogoro inaendelea kuharibu vituo vya afya; na sasa mzozo huo umeharibu njia ya maisha kwa watoto wa Sudan walio katika mazingira magumu zaidi. Kutokana na hiyo kiwanda cha Khartoum kinachozalisha chakula cha tiba kwa watoto wa Sudan wanaokabiliwa na utapiamlo hatari zaidi kimeteketezwa kwa moto. Moto huo uliteketeza masanduku 14,500 ya chakula kilicho tayari kutumika kwa matibabu (RUTF). Chakula hicho kilikusudiwa kusafirishwa hadi maeneo kwa ajili ya matunzo ya kuokoa maisha ya watoto 14,500. Hii ni picha mbaya na ya wazi zaidi, hadi sasa, jinsi mgogoro huu unavyotishia maisha ya watoto kwa njia nyingi. Ni pigo jingine kwa watoto walio katika mazingira magumu zaidi nchini Sudan. Mwaka jana, kiwanda cha SAMIL kilizalisha 60 % ya RUTF ilitumika kutibu watoto wanaougua utapiamlo mkali nchini Sudan.
Moto huo pia ulisababisha uharibifu kamili wa mitambo ya kiwanda, na kusimamisha kabisa uzalishaji. Hii itaathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa virutubisho kwa wakati kwa maelfu ya watoto. Katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo nchini Sudan, UNICEF kwa sasa ina: masanduku 34,000 ya RUTF katika shehena inayowasili kutoka Ufaransa; katoni nyingine 81,000 ziko tayari kutumwa kutoka Ufaransa mwishoni mwa mwezi. Kwa kiasi fulani kimiujiza hakika kishujaa, asilimia 80% ya programu za matibabu ya wagonjwa wa nje kwa sasa zinafanya kazi nchini Sudan. Hii ni shukrani kwa washirika wa UNICEF na wafanyakazi wa afya wa Sudan. Licha ya juhudi hizi za kujitolea, migogoro inaendelea kuwazuia watoto kupata matibabu; migogoro inaendelea kuharibu vituo vya afya; na sasa mzozo huo umeharibu njia ya maisha kwa watoto wa Sudan walio katika mazingira magumu zaidi."
Na wakati huo huo vita vya Sudan vimetimiza mwezi mmoja bila matumaini ya kumalizika. Hivi ni vita vya kuwania madaraka vimetimiza mwezi mmoja tangu vilipoanza, huku mapigano yakiendelea kuutikisa mji mkuu Khartoum. Wakati huo huo mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Jeddah nchini Saudi Arabia bado hayajazaa matunda ya kusitisha vita kabisa. Katika muktadha huo wa mapigano nchini Sudan, kama walivyosema wahanga kuwa zigombanpo fahali wawili ziumiazo ni nyasi hivyo ni familia na raia wa nchi hiyo ambao wanazidi kuteseka kutokana na vita kati ya majenerali wawili wanaozozana. Kutokana na hiyo kwa mwezi mmoja sasa raia wengi sana wamekuwa wakijaribu kukwepa risasi na kukimbilia usalama, lakini uhaba wa vyakula na mahitaji mengine ya msingi umeendelea kukithiri kwa watu wasio na hatia. Umeme unakatika kila mara. Mawasiliano yanatatizika na mfumuko wa bei pia umepanda. Kwa muda mrefu mji wa Khartoum wenye wakaazi milioni tano na ulioko karibu na Mto Nile, ulikuwa tulivu na tajiri, hata katika miongo ya vikwazo dhidi ya aliyekuwa rais wa zamani wa kiimla wa taifa hilo Omar al-Bashir. Lakini sivyo tena. Kwa sasa, mji huo ni kama mfano tu wa wakimbizi huku Mashambulizi ya makombora na ya angani yakiendelea kuzikumba sehemu mbalimbali.
Katika uwanja wa ndege wa Khartoum Khartoum ni mabaki ya ndege iliyoteketezwa moto. Kwenye mitaa ya Khartoum ni ofisi ambazo zimefungwa za ubalozi wa nchi mbalimbali, na kurudi makwao, hospitali zilizoharibiwa, maduka na mabenki ambayo yamefungwa pamoja na maghala ya nafaka ambayo yameporwa. Ndiyo taswira unayokumbana nayo ambayo imesababishwa na vita vilivyoanza tangu tarehe 15 Aprili 2023 kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anayekiongoza kikosi chenye nguvu cha wanamgambo Rapid Support (RSF). Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia machafuko yanayohusisha silaha kama bunduki ACEDP) mapigano hayo tayari yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 750. Maelfu Zaidi pia wamejeruhiwa na tayari takriban watu milioni moja wameyakimbia makwao. Wengine wakikimbilia nchi iirani kama Misri, Ethiopia, Chad na Sudan Kusini, ambayp licha ya matatizo yao ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, wanazidi kurundikana wakimbizi wengine. Machafuko hayo yamewaacha kwenye mateso zaidi ya raia milioni 45, wa nchi hiyo ambayo ni kati ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni.