Siku ya Afrika:Tunasherehekea ahadi kubwa na tuulinde umoja
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kila tarehe 25 Mei ni siku ya Siku ya Afrika, ambapo tunapoelekea katika kilele cha siku hiyo tunasherehekea ahadi kubwa na uwezo wa bara la Afrika lenye ari na nguvu. Bara ambalo licha ya kuwa kubwa na rasilimali zake muhimu, ni bara ambalo linawindwa na linaporwa mali zake. Watu wanaishi utafikiri hawana malighafi na zenye thamani hasa. Kwa hiyo kuadhimisha Siku ya Afrika, ni kujivunia uafrika wetu, uzalendo wetu, umoja wetu, licha ya migawanyiko na vita vya kisilaha, itikadi kali na malumbano ya kidini. Haya yote sio asili ya utamaduni wa kiafrika, ambao umekuwa ni mshikamano wa mababu zetu, kwa lugha nyingine "Falsafa ya Ubuntu", bali ni virusi vilivyongilia kati katika bara la Afrika.
Papa Mstaafu Benedikto XVI alikuwa amesema kuwa "Afrika ni pafu la kiroho la mwanadamu kwa shida ya imani na matumaini". Vile vile katika maneno ya kwanza ya Papa Francisko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati wa ziara ya Kitume barani Afrika hivi karibuni alisema kuwa:“Nchi hii na bara hili zinastahili kuheshimiwa na kusikilizwa, zinastahili nafasi na umakini: mikono itolewe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mikono iwe mbali na Afrika!” Anatambua vyema historia yake.
Wakati wa hotuba yake kwa Mamlaka, Mashirika ya Kiraia na Kikosi cha Wanadiplomasia huko DRC, Papa alisema: “Acheni kukandamiza Afrika: si mgodi wa kunyonywa au ardhi ya kuporwa. Afrika iwe mhusika mkuu wa hatima yake! Dunia ikumbuke majanga yaliyotokea kwa karne nyingi kwa hasara ya wakazi wa huko na bila kusahau nchi hii na bara hili la Afrika, tabasamu na matumaini ya dunia, ni muhimu zaidi: ikiwa itazungumzwa zaidi, itakuwa na uzito na uwakilishi zaidi kati ya Mataifa!”.
Katika fursa hii ya Siku ya Afrika, ni vema kukumbuka maneno hayo muhimu na tujivunie afrika na tutitetee na kuilinda sisi wenyewe, kwani hakuna atakayetoka nje kulinda bara hili zaidi ya kulipora. Nikirudi tena kwenye hotuba ya Papa ambayo ilikuwa na mguso sana kwa kile kinachoendelea nchi ile na bara la Afrika kwa ujumla alisema: “Almasi huinuka kutoka ardhini halisi lakini mbaya, inayohitaji kusindika. Hivyo basi, hata almasi za thamani zaidi za ardhi ya Congo, ambao ni watoto wa taifa hili, lazima waweze kutumia fursa halali za elimu, ambazo zinawawezesha kutumia kikamilifu talanta nzuri walizonazo. Elimu ni ya msingi:ni njia ya siku zijazo, njia ya kuchukua ili kupata uhuru kamili katika nchi hii na bara la Afrika.
Baba Mtakatifu Francisko alikazia kusema kuwa "Ni haraka kuwekeza ndani yake, kuandaa jamii ambazo zitaunganishwa tu ikiwa zimeelimika vyema, zinazojitawala tu ikiwa zinafahamu kikamilifu uwezo wao na wenye uwezo wa kuiendeleza kwa uwajibikaji na uvumilivu. Lakini watoto wengi hawaendi shuleni: ni wangapi, badala ya kupata elimu inayofaa, wananyonywa! Wengi sana wanakufa, wakifanya kazi ya utumwa migodini. Juhudi zimeepushwa kukemea janga la utumikishwaji wa watoto na kukomesha hilo. Ni wasichana wangapi wanaotengwa na kudhulumiwa utu wao! Watoto, wasichana, vijana ni wakati wa sasa wa matumaini, na ni matumaini: tusiruhusu kufutwa, lakini tuikuze kwa shauku!” Kwa hakika elimu ndiyo msingi wa Yote na tusherehekee pamoja 25 Mei Siku ya Afrika.