Tafuta

Watu wakikimbia kutoka Khartoum kutokana na mapigano yanaoyoendelea Watu wakikimbia kutoka Khartoum kutokana na mapigano yanaoyoendelea  (AFP or licensors)

Mapigano nchini Sudan na idadi ya waathirika yaongezeka

Idadi ya waliofariki kutokana na mapigano yaliyozuka Jumamosi 15 Aprili nchini Sudan kati ya jeshi la serikali na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) iliendelea kuongezeka na majeruhi ni wengi wakati Mji mkuu wa Khartoum umeathiriwa zaidi.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu alielezea  wasiwasi wake kuhusu hali ya Sudan ambapo idadi ya vifo kutokana na mapigano kati ya wanajeshi wa nchi hiyo na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces imeongezeka hadi zaidi ya 50 waathiriwa. Ombi la Baba Mtakatifu ni kusali ili mazungumzo yaweze kuwepo na njia ya amani na maelewano ianze tena kwa pamoja. Wafanyakazi watatu wa WFP wauawa Darfur.  Na  wakati huo huo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu itafanya mkutano wa dharura mjini Cairo.

Kwa upande mmoja Jenerali Abdel-Fattah Burhan, kamanda wa vikosi vya jeshi, na kwa upande mwingine Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, mkuu wa kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces ndio makundi mawili ambayo yamekuwa yakipigania udhibiti wa Sudan tangu Jumamosi 15 Aprili. Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani ambao kwa pamoja walipanga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021 ambayo yalivuruga mageuzi ya kidemokrasia ambayo Sudan yalikuwa yakielekea baada ya utawala wa muda mrefu wa Omar al-Bashir, kuondolewa madarakani mwaka 2019. Kwa hiyo mapigano makali yaliripotiwa katika mji mkuu Khartoum, katika uwanja wa ndege wa kimataifa, katika mji wa Omdurman na katika maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na magari ya kivita, ndege na mashambulio makubwa ya mizinga. Jeshi na vikosi vinavyoongozwa na Dagalo vinasema vinadhibiti nafasi za kimkakati na majumba ya madaraka huko Khartoum na kwingineko katika jimbo hilo. Lakini haya ni madai ambayo hayawezi kuthibitishwa kwa kujitegemea.

Pande zote mbili kwa sasa haziko tayari kufanya mazungumzo. Jeshi la Burhan limetoa wito wa kuvunjwa kwa RSF, inayoitwa wanamgambo wa waasi. Kwa upande wake, Dagalo alifuta mazungumzo na kumtaka Burhan ajisalimishe. Khalid Omar, msemaji wa kambi inayounga mkono demokrasia, alionya kuwa ghasia za hivi karibuni zinaweza kusababisha vita na kusambaratika kwa nchi. Jana mchana, jeshi la Sudan na wanamgambo walitangaza nia yao ya kufungua kwa muda, kwa muda wa saa tatu au nne, korido za kibinadamu zilizoombwa na Umoja wa Mataifa, huku wakihifadhi haki ya kurudisha moto kutoka kwa upande unaopingana. Kwa kweli, saa moja na nusu tu baada ya makubaliano haya kuenea kwenye chaneli za kijamii, risasi ilianza tena.

Na diplomasia ya kimataifa inashinikiza kusitishwa kwa mapigano bila masharti. Marekani, EU, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu wanazitaka pande husika kusitisha mapigano. Umoja wa Afrika(UA), ambao mkuu wake, ni Rais Moussa Faki Mahamat, atakwenda mara moja nchini Sudan kushinikiza jeshi na wanamgambo kukubaliana juu ya kusitisha mapigano"pia uko kwenye mstari huo huo. Haya ndiyo yanaibuka kutokana na taarifa iliyopitishwa jana na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC) kuhusu hali ya nchi hiyo, na kutangaza ujumbe wake katika  nyanja ya kazi.

 

17 April 2023, 15:17