Baa la njaa nchini Somalia bado ni tishio pamoja na ulinzi na usalama
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni tarehe 22 Februari limejulishwa kuwa hali ya ukame na ukali wake nchini Somalia si ya kawaida huku mahitaji ya kibinadamu yakiendelea kuongezeka kila siku. Bi Anita Kiki Gbeho, Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, alisema hayo akihutubia Baraza hilo lililokutana sio tu kwa ajili ya kupatiwa taarifa kuhusu hali ya Somalia, bali pia kufanya mashauriano. Bi. Gbeho alisema takribani watu milioni 8.3 nchini Somalia watahitaji usaidizi wa kibinadamu na ulinzi kwa mwaka huu wa 2023, idadi ambayo ni takribani nusu ya wananchi wa Somalia. “Ingawa baa la njaa limeweza kuzuilika kwa sasa, bado linasalia tishio iwapo mvua za mwezi Aprili hadi Juni hazitakuwa za kutosha kwa kuwa hakuna uhakika wa usaidizi wa kibinadamu,” alisema kiongozi huyo.
Asilimia 60 ya watu nchini Somalia wameuawa kati ya 2017-2022
Kuhusu amani na usalama, Naibu Mwakilishi huyo alisema kikundi cha Al-Shabaab kinaendelea kuwa tishio kubwa kwa amani na usalama nchini Somalia. “Mwaka 2022 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa raia tangu mwaka 2017 kutokana na ongezeko la asilimia 60 la idadi ya raia waliouawa kwenye mashambulizi ikilinganishwa na mwaka 2021. Katika miezi michache iliyopita, serikali kuu imekuwa na maendeleo makubwa katika kukabili vitisho vya kikundi hicho kwa kulenga operesheni za kijeshi na kifedha na kauli zao za kiitikadi,” alisema Bi. Gbeho.
Mkurugenzi mtendaji wa masuala ya wanawake katika UN
Na kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake UN Women, Bi Sima Bahous aliliomba Baraza lichukue hatua kuhakikisha kuna ushiriki thabiti wa wanawake kwenye michakato yote nchini Somalia. “Mara kwa mara mmetoa wito wa ushiriki wa wanawake. Lakini tunanaka ninyi muwe makini zaidi kuhusu ni nini mnataka na ni nini mnatarajia. Wajumbe wa Baraza mmeibua umuhimu wa asilimia 30 kutengwa kwa ajili ya wanawake, halikadhalika suala la sheria mpya kuhusu ukatili wa kingono,” alisema Mkuu huyo wa UN Women.
Vitendo vya ukatili vinaongezeka dhidi ya wanawake
Hata hivyo alibainisha kuwa kisemwacho sio kitekelezwacho kwani, “kiwango hicho cha asilimia 30 hakikufikiwa, uwakilishi wa wanawake umepungua, ukatili wa kingono umeongezeka na Sheria ya makosa ya kujamiiana ilipitishwa na Baraza la Mawaziri miaka mitano iliyopita lakini bado haijapitishwa na Bunge. Badala yake wapinzani wa sheria hiyo wanashinikiza sheria mbadala ya kuhalalisha ndoa za utotoni, na kuondoa kipengele cha umri, kupunguza ushaidi na kuondoa haki za manusura.” Aliweka wazi. Na kama hiyo haitoshi, aliongeza kusema kuwa licha ya ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono na ukwepaji sheria wa mashambulizi yanayolenga wanawake, hakuna hata moja ya uhalifu huo uliorodheshwa kwenye Kamati ya Vikwazo dhidi ya Somalia tangu mwaka 2014. “Kamati imeendelea kufumbia macho masuala ya jinsia," alisisitiza kiongozi huyo.