Wanawake na wasichana Afghanistan kuzuiwa kujiunga Vyuo Vikuu
Na Angella – Rwezaula; - Vatican.
Uamuzi wa uongozi wa watalibani nchini Afghanistan wa kupiga marufuku wanawake na wasichana kujiunga na Vyuo Vikuu hadi itakapotangazwa tena, umelaaniwa vikali na Umoja wa Mataifa na wadau wake kwa kuzingatia kuwa unakwenda kinyume na haki za binadamu na vile vile unarudisha nyuma maendeleo ya jamii kwa ujumla. Kauli za kupinga hatua ya uongozi huo uliojiweka madarakani tangu mwezi Agosti mwaka jana wa 2021 unazingatia madhara yake kwa wanawake na wasichana ambapo Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Afghanistan, UNAMA pamoja na wadau wa kibinadamu kupitia taarifa yao iliyotolewa mji mkuu wa taifa hilo, Kabul unachambua athari za uamuzi huo.
kwa njia hiyo katika kuelekeza athari hizo taarifa ya pamoja na kuonesha mshikamano na mamilioni ya waafghanistan wanaopinga kauli hiyo, halikadhalika jamii ya kimataifa, inataka mamlaka za watalibani zitengue uamuzi huo. Pamoja na kutoa kauli hiyo, Umoja wa Mataifa na wadau nchini Afghanistan wanataka mamlaka hizo zifungue tena shule za wasichana kuanzia darasa la sit ana kuendelea na kuondokana na mikakati ya kuzuia wanawake na wasichana kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku za umma. Kuzuia wanawake wasijiunge na Vyuo Vikuu ni mwendelezo wa mfumo sera za kibaguzi zilizowekwa na watalibani dhidi ya wanawake. Tangu tarehe 15 mwezi Agosti mwaka 2021, mamlaka hayo yamezuia wasichana wasiendelee na elimu ya sekondari, wamedhibiti mienendo huru ya wanawake na wasichana, wameengua wanawake kutoka kwenye maeneo mengi ya nguvukazi, na wamepiga marufuku wanawake kwenda kwenye bustani za mapumziko, vyumba vya mazoezi ya viungo na mabafu ya umma. Vizuizi hivi vimesababisha wanawake na wasichana kusalia kwenye kuta nne tu za nyumba zao.
Umoja wa Mataifa na wadau wanasema kuzuia nusu ya idadi ya watu nchini Afghanistan wasichangie kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi kutakuw ana madhara makubwa kwa nchi nzima. Itasababisha Afghanistan kutengwa zaidi kimataifa, halikadhalika hali ngumu ya kiuchumi na machungu, na madhara hayo yatakumba mamilioni ya watu wengi zaidi miaka ijayo. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kuzuia wanawake wasifanye kazi kunaweza kusababisha hasara ya kiuchumi ya takribani dola bilioni 1. Kuzuia wanawake na wasichana wasijiunge na Vyuo Vikuu, wakiwemo wahadhiri na maprofesa wanawake kutasababisha hasara ya kiuchumi.
Elimu ni haki ya msingi ya binadamu. Kuengua wanawake na wasichana kwenye elimu ya sekondari ya elimu ya juu sio tu kunawanyima haki hii ya msingi, bali pia inainyima jamii ya Afghanistan manufaa ya jumla ya kupata mchango ambao ungalitolewa na wanawake na wasichana. Inaharibu mustakabli wa Afghanistan. Umoja wa Mataifa unasema hatua hii ya kuengua wanawake na wasichana kwenye elimu, ajira na maeneo mengine kunaongeza hatari ya ndoa za lazima, ndoa katika umri mdogo, ukatili na manyanyaso. “Kuendelea kubaguliwa kwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan kutakwamisha lengo la kuwa na jamii jumuishi ambamo kwayo kila mtu anaishi kwa utu na anafurahi fursa sawa,” imesema taarifa hiyo.
Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na wadau wa kibinadamu wanakumbusha watalibani kuwa kupora uhuru na utashi wa wanawake kuchagua hatma yao, kuwavunja uwezo wao na kuweka mfumo wa kuwaengua kwenye Nyanja zote za umma na kisiasa ni ukandamizaji na ni ukiukwaji wa haki za kimataifa za msingi zinazojenga jamii yoyote ile. “Uamuzi huu utakuwa na athari hasi kwa raia wa Afghanistani wanaoishi ughaibuni wanapofikiria kurejea nyumbani, na wakati huo utasababisha raia wengi zaidi kukimbia nchi yao,” imetamatisha taarifa hiyo.