Wasafiri wamefika kutoka Tigray katika Uwanja wa Kimataifa wa Bole -Addis Ababa. Wasafiri wamefika kutoka Tigray katika Uwanja wa Kimataifa wa Bole -Addis Ababa. 

Ethiopia:Makubaliano kati ya serikali na viongozi wa Ethiopia na Tigray

Ethiopia na Tigray wamefikia makubaliano muhimu.Serikali imeahidi kurejesha kikamilifu huduma za kitaasisi na kukarabati miundombinu katika maeneo yote ya mkoa huo.Ethiopia na vikosi vya waasi wa Tigray wamekubaliana kuunda chombo cha pamoja cha ufuatiliaji ili kuhakikisha makubaliano ya amani na ndege zinaanza safari tena.

Na Angella Rwezaula; - Vatican.

Vyombo vya habari vya Ethiopia vilielezea mijadala ambayo imefanyika katika siku za hivi karibuni kati ya wajumbe kutoka Addis Ababa na viongozi wa chama cha Popular Front for the Liberation of Tigray (TPLF) kuhusu kuondolewa kwa vikosi vya Eritrea kutoka eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ni kama makubalino ya kihistoria. Baada ya kuwasili huko Mekelle Jumatatu tarehe 26 Desemba 2022, ujumbe wa serikali na viongozi wa Tigray walijadili masuala kadhaa ya dharura yanayohusiana na misaada ya kibinadamu, huduma msingi, biashara na uondoaji wa vikosi vya Eritrea na Amhara.

Mshauri wa Rais wa Tigray, Reda:Majadiliano yenye ufanisi yalifikiwa

Kwa mujibu wa Bwana Getachew Reda, mshauri wa rais wa Tigray, ambaye pia alitia saini mkataba wa amani na serikali ya Ethiopia kwa niaba ya TPLF, alisema: majadiliano yenye ufanisi yalifanyika na makubaliano muhimu yalifikiwa. Tutaendelea kukuza maendeleo tunapokabiliana na changamoto zijazo.”

Kuingia kwa jeshi la Ethiopia mji mkuu wa Tigray

Serikali imeahidi kurejesha kikamilifu huduma za kitaasisi na kukarabati miundombinu katika maeneo yote ya mkoa huo. Ethiopia na vikosi vya waasi wa Tigray wamekubaliana kuunda chombo cha pamoja cha ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini nchini Afrika Kusini mnamo Novemba 2 iliyopita, yenye lengo la kumaliza vita vya umwagaji damu, yanaheshimiwa na pande zote. Masharti ya makubaliano hayo pia yanajumuisha hakikisho la ufikiaji wa kibinadamu na kuingia kwa jeshi la Ethiopia katika mji mkuu wa Tigray.

Shirika la Ndege la Ethiopia kurejesha safari hadi Mekelle

Huu ni ujumbe wa kwanza kutoka kwa serikali kuu ya Ethiopia kutembelea eneo hilo miaka miwili baada ya mzozo ni kuanza kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwezi uliopita. Shirika la Habari za Kimisionari (Fides), limebainisha kwamba zaidi ya hayo, Jumanne tarehe 27 Desemba 2022 shirika la ndege la taifa, (Ethiopian Airlines), lilitangaza uamuzi wa kurejesha safari za ndege hadi Mekelle, ili kuruhusu familia kuungana na kuwezesha kurejeshwa kwa shughuli za kibiashara, kuchochea mtiririko wa watalii na kuleta fursa muhimu kwa jamii husika. Huku safari za ndege zikipangwa kwenda mji mkuu wa eneo hilo kila siku, shirika hilo la ndege lilisema litaongeza masafa kulingana na mahitaji ya njia.

29 December 2022, 10:25