Siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Tunachapisha maelezo na maelekezo yaliyo kwenye Tovuti ya UN Women, yaani ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalojikita na masuala ya wanawake, katika fursa ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ifanyikayo kila ifikapo tarehe 25 Novemba ya kila mwaka. Katika taarifa yao wanabainisha kwamba mabadiliko ya tabianchi yanachochea aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na tayari kuna mwenendo ulio dhahiri ambao bila shaka unazidi kupanuka kadri janga la tabianchi linavyozidi kuwa baya. Kasi ya meandeleo ya teknolojia nayo yanaongeza ukatili wa wanawake na wasichana kupitia mtandaoni na kuibua vitisho vipya dhidi ya haki za makundi hayo. Na wakati huo huo kumekuweko na ongezeko la harakati dhidi ya makundi yanayotetea haki pamoja na yale yanayosimamia masuala ya wanawake, na hivyo kurejesha nyuma sheria ambazo tayari zilikwisha tolewa kwa maendeleo ya utetezi wa haki za wanawake, halikadhalika kutishia mustakabali wa watetezi wa haki za wanawake, Katika muktadha huo, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kunaweza kuonekana kama hakuwezi kufanikiwa.
Kupungua kwa kiasi kikubwa cha ukatili dhidi ya wanawake kunaweza kufanikiwa kupitia harakati za utetezi wa masuala ya wanawake na uhamasishaji unaounganishwa na kuratibiwa kupitia haki, afya, fedha na sekta nyingine nyingi. Ushuhuda wa hivi karibuni unadokeza kuwa harakati thabiti na huru za utetezi wa masuala ya wanawake ni muhimu katika kuchocheea mabadiliko hayo. Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ni jukumu la kila mtu. Ndio maana katika siku hizi 16, ya sual hilo inayoongoza na kauli mbiu “onesha mshikamano wako na harakati za utetezi wa haki za wanawake na uchechemuzi duniani kote”. Iwe ni mwanaharakati wa msimu au ndio kwanza unaanza, kuna njia 10 ambazo unaweza kuchangia katika kutokomeza vitendo hivyo,” kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women.
Njia hizo 10 za kushiriki kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana awali ya yote ni kupaza sauti; Zungumza: Ukatili dhidi ya wanawake umetapakaa, lakini si kwamba hauwezi kuepukika, labda tunyamaze. Katika zama hizi za kuongezeka kwa harakati na vuguvugu za makundi ya utetezi wa haki za wanawake, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kupaza sauti na kuzungumza. Mila potofu zinazozingira ukatili wa kijinsia hupatia watendaji fursa ya kukwepa mkono wa sheria na kuzuia wanawake na wasichana kupata msaada wanaohitaji: Takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanaotafuta msaada baada ya kukumbwa na ukatili wa kijinsia ni chini ya asilimia 40 tu. Kwa maana hiyo hebu waoneshe manusura na wanaharakati kuwa uko nao. Paza sauti na simulizi zao. Fungua fursa ya mazungumzo iwe ya uso kwa uso au mtandaoni.
2. Fahamu tatizo pamoja na dalili: Ukatili dhidi ya wanawake hujitokeza katika njia tofauti tofauti. Inaweza kuwa kimwili, kingono au kifikra. Inaweza kufanyika mbele za watu, faraghani au mtandaoni na kutekelezwa na mpenzi au mtu mwingine yoyote. Bila kujali unafanyika vipi, wapi na umetekelezwa nani au ni kwa sababu gani? Ukatili dhidi ya wanawake una madhara makubwa ya muda mfupi au muda mrefu kwa wasichana na wanawake na huzuia ushiriki wao kikamilifu kwenye jamii zao.
3. Kemea unyanyasaji wa kijinsia: Kwa wanawake wengi, unyanyasaji wa kijinsia ni uzoefu wa kila siku. Iwe mtandaoni, mtaani, pahala pa kazi, kupuuzia tabia isiyo sahihi huendelea kukomaza au kushamirisha unyanyasaji wa kijinsia na kuonekana kuwa jambo la kawaida. Manyanyaso yaliyozoeleka kama vile uonevu mtandaoni, mazungumzo ya kingono, kupiga mluzi, vituko au vichekesho vya kingono hufanya wanawake na wasichana wajione hawakaribishwi au hawajisikii kuweko kwenye maeneo fulani au wajione hawako salama. Vitendo hivyo vinasaidia kuimarisha vitengo ya ubaguzi wa kijinsia na huchochea kuimarika kwa utamaduni wa ukwepaji sheria ambao hatimaye madhara yake huathiri wanawake. Kwa hiyo katika hilo jaribu kuweka mazingira salama mtandaoni na nje ya mtandao kwa kila mtu na hoji wana rika wenzako juu ya tabia zao na kemea yeyote yule anayevuka mipaka kwenye mazungumzo au saka usaidizi pindi unapohisi hauko salama.
4. Hoji mfumo dume: Mfume dume wenye sumu na uhachochea ukatili dhidi ya wanawake. Ushahudi unaonesha kuwa wanawake walio kwenye uhusiano na wanaume ambao tabia na imani zao zinabeba na kushinikiza ubabe wa kiume na ukosefu wa usawa wa kijinsia wako hatarini zaidi kukumbwa na ghasia kutoka kwa mpenzi. Fikra za kiutamaduni kuhusu ubabe wa kiume huchochea mienendo kama uonevu na udhibiti huku vikipuuza hisia za mtu, upendo, huruma na mambo mengine ambayo kitamaduni yanaambatana na masuala ya wanawake. Kwa maana hiyo tunaposhindwa kuhoji na kukemea imani na fikra hizi potofu, kila mtu anapata hasara. Hebu tafakari mawazo yako kuhusu mfumo dume na msimamo wako kuhusu wanawake na bonga bongo kuhusu taswira ya jinsia kwenye vyombo vya habari na tamaduni mbalimbali. Shikamana na wanaume na wavulana kwenye maisha yako kusongesha kujali na kuelezea mienendo mingine isiyopatia kipaumbele mfumo dume hatarishi.
5. Fadhili mashirika ya wanawake: Kuwekeza katika harakati za kusongesha wanawake kuna umuhimu mkubwa. Ushahidi unaonesha kuwa harakati huru na thabiti kuhusu wanawake ni muhimu katika kuchochea mabadiliko ya kisera kuhusu ukatili wa kijinsia. Lakini kadri siku zinavyosonga mashirika ya wanawake ambayo ni muhimu katika kuleta mabadiliko yanazidi kukosa ufadhili, yakienguliwa na kunyamazishwa kwenye mchakato wa kutoa maamuzi. Kuongeza ufadhili wa muda mrefu kwa mashirika hay ani jawabu la msingi la kuzuia na kuchukua hatua kukabili ukatili dhidi ya wanawake. Changia mashirika ya eneo lako yanayojengea uwezo wanawake, saidia manusura na songesha hatua na sera zinazolenga kuzuia ukatili wa kijinsia. Umoja huo wa wanawake wa UN Women kwa upande wake hushirikiana na mashirika ya wanawake duniani kote kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na kusaka haki sawa kwa wanawake na wasichana. Unaweza kuchangia hapa.
6. Paza sauti kwa hatua na huduma bora: Huduma kwa wanawake na wasichana wanaokumbwa na ukatili zinaweza kuleta tofauti kubwa kati ya uhai na kifo. Hii ina maana maeneo ya hifadhi, namba za simu za kutoa taarifa wakati wowote, ushauri nasaha na aina zozote za usaidizi ambao manusura wa ukatili wa kijinsia wanahitaji hata wakati wa majanga na dharura. Kila mwaka, kampeni ya siku 16 ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake husaka hatua za pamoja za kimataifa kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Ungana nasi kaitka kutoa wito kwa serikali kuondoa pengo la ufadhili na kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuhakikisha huduma zinapatikana na zinkuweko wakati wowote. Shiriki kwa kujitolea kwenye maeneo ya hifadhi ya manusura wanawake, changia nguo au vifaa, au pata mafunzo uwe mshauri nasaha kwenye makazi ya hifadhi ya wanawake manusura.
7. Tafuta takwimu zaidi: Harakati thabiti za kukabili ukatili wa kijinsia ni kutambua tatizo lenyewe. Takwimu sahihi ni muhimu katika kufanikisha hilo hasa katika kuzuia na kupatia manusura msaada sahihi. Hata hivyo kupata takwimu sahihi zilizonyumbuliwa kijjinsia bado ni changamoto na pia hakupatiwi kipaumbele na serikali. Ukatili wa kijinsia unavyoshamiri kutokana na janga la UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine, pengo la takwimu zenye mnyumbuliko wa kijinsia limekuwa dhahiri zaidi kuliko wakati wowote. Toa wito kwa serikali ziwewekeze kwenye ukusanyaji wa takwimu kuhusu ukatili wa kijinsia.
8. Hamasisha zaidi ili kuweko na sheria thabiti: Ni miaka 21 sasa tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake duniani. Dunia inahitaji mifumo thabiti zaidi ya ulinzi na kutokomeza ukatili, unyanyasaji, na vitisho na ubaguzi dhidi ya wanawake watetezi wa haki za binadamu na wawahamaishaji na wanaharakati wa masuala ya wanawake. Fahamu zaidi kuhusu sheria katika nchi yako kwa kubofya hapa. Na wakati huo huo toa wito kwa serikali yako iimarisha mifumo ya kisheria, na saidia kupaza sauti na uelewa kuhusu mapengo ya kisheria yaliyoko. Kwa njia hiyo anzia au unga mkono maandamano, saidia vikundi vya uhmasishaji, na jielimishe mwenyewe kuhusu misimamo ya wagombea wa kisiasa au wawakilishi kuhusu masuala ya wanawake.
9. Unga mkono uongozi wa wanawake: Wakatiwa janga la UVIKO-19, wanawake waliondolewa kwa kiasi kikubwa kwenye vikosi kazi vya kujikwamua baada ya janga la Uviko. Pengo hilo linadhihirika katika hatua za serikali kwenye masuala ya kijinsia kama vile kuongezeka kwa ghasia majumbani. Suala hilo ni vivyo hivyo kwenye hatua kwa tabianchi, ujenzi wa amani na mengine mengi ambako sauti zao hazisikiki. Hali hii inasababisha vyombo vya maamuzi kusahau mapengo muhimu yaliyoko kwenye utungaji wa sera na ufadhili. Uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya kupitisha maamuzi ni muhimu sana na husaidia kuhakikisha mahitaji ya wanawake na wasichana yanakuwa kitovu cha hatua zozote wakati wa dharura au majanga, mikataba ya amani na utungaji wa sera zozote. Na wakati huo huo, viongozi wanawake wanakabiliwa na hatari ya ghasia; katika mabara Matano, asilimia 82 ya wanawake wabunge wameripoti kukumbwa na aina ya ghasia za kisaikolojia wakati wa awamu zao za ubunge. Kwa sasa wito unazidi kutolewa kwa uwakilishi zaidi wa wanawake kwenye nafasi za uongozi. SAidia au unga mkono wagombea wanawake na mashirika au kampuni za wanawake. Au chukua jukumu wewe mwenyewe kwa kuwa kiongozi mwanamke unayependa kuona duniani.
10. Shikamana na harakati nyingine za kuinua wanawake: Umoja ni nguvu na mshikamano ni udhaifu. Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana una uhusiano na aina nyingine za vitendo vibaya na ukosefu wa haki, ikiwemo ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, umaskini na mabadiliko ya tabianchi. Kwa sababu hiyo jitahidi kuimarisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na makundi mengine ya harakati za kijamii na kisiasa ili pia kujumuisha wanaharakati kwenye makundi hayo katika kundi lako. Kwa pamoja, tunaweza kuzuia kurejeshwa nyuma kwa haki za wanawake na hatimaye kupaza sauti na matakwa ya harakati za utetezi wa masuala ya wanawake duniani kote na kisha ajenda ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ifanikiwe.
Sasisho tarehe 25 Novemba 2022 katika Siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake